BREAKING NEWS: Rais Dkt.Mwinyi atengua uteuzi wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB)

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametengua uteuzi wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Salum Yussuf Ali ili kupisha uchunguzi wa kina wa upotevu wa fedha za makusanyo ya mapato zilizopotea.
Rais Dkt. Mwinyi amefikia maamuzi hayo leo wakati akiwa katika Ofisi za Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Mazizini Zanzibar ambapo alipata fursa ya kuzungumza na uongozi wa Mamlaka ya Bodi ya Mapato pamoja na uongozi wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa ofisi za mamlaka hiyo.

Wakati huo huo, taarifa maalum iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said imeeleza kuwa, utenguzi wa kiongozi huyo wa ZRB, Rais Dkt. Mwinyi ameufanya leo Februari 17, 2022.

Pia, Rais Dkt. Mwinyi akiwa katika ofizi hizo za Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ameiagiza Bodi ya Mamlaka hiyo kumsimamisha kazi na kupisha ukaguzi wa kina wa maelekezo ya Mkurugenzi wa Usajili, Ukaguzi na Upelelezi wa Walipa Kodi, Hashim Kombo Haji kupisha ukaguzi wa kina wa maelekezo yake ya kuondoa taarifa za ukaguzi ambazo hatimaye hazikupelekwa kwenye bodi.

Sambamba na hayo, aliiagiza Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kufanya uchunguzi kwa kushirikiana na watendaji waliofanya uchunguzi pamoja na kushirikiana na vikosi vyote vya ulinzi na usalama watakavyovihitaji ili kujua fedha hizo zimeenda wapi.

Amesisistiza haja ya taarifa zote za Kitengo cha Uchunguzi, kufanyiwa uchunguzi, zifuatiliwe ili kujua ripoti zilizotolewa na kitengo hicho hatima yake ni kitu gani.

Pamoja na hayo, ametaka uchunguzi ufanywe wa lita za mafuta zenye gharama ya Shilingi Milioni 58, ushuru wake umelipwa wapi huku akiiagiza Bodi kutokana na unyeti wa Kitengo cha Usajili, Ukaguzi na Upelelezi wa Walipa Kodi, kitengo hicho kijitegemee na kiwe chini ya Kamishna Mkuu na kisiripoti sehemu nyingine yeyote.

Ameeleza kwamba, ukaguzi maalum ufanyike kuchunguza utendaji wa mfumo wa ukusanyaji mapato ambao unaonekana unahujumiwa huku akitaka kufuatiliwa kwa akauti za benki ambazo mlipa kodi hulipa ada ya bandari ili kujua hizo fedha za kaampuni ya usafiri wa meli zimeingia katika akaunti gani.

Ameongeza kuwa, hatua hizo ndizo zinazopelekea utendaji wa kazi ufanyike kwa kiwango cha chini na kusema kwamba hatomuonea mtu na ndio maana anataka kufanywe uchunguzi na ikithibitika kwamba waliotuhumiwa hawana kosa haki itatendeka na ikithibitika kwamba wana makosa lazima sheria ifuate mkondo wake.

Katika maelezo yake, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa amepokea taarifa za kusikisha kutoka kwa Kitengo cha Uchunguzi cha Mamlaka ya Bodi hiyo ambapo jukumu lake ni kufanya uchunguzi wa ulipaji wa kodi na kikishafanya uchunguzi ni jukumu la ZRB kufanya uchunguzi zaidi wa taarifa hiyo, lakini kinachotokea ni kuzimwa kwa uchunguzi huo.

Akieleza miongoni mwa mifano ni uchunguzi uliofanywa wa moja ya kampuni ya meli ya usafirishaji wa abiria ambapo kunaonesha tofauti ya ulipaji wa Bilioni 9.65 ambazo hazikulipwa ambapo uchunguzi ulifanyika na ikaonekana kwamba muhusika kalipa lakini fedha hazikuonekana.

Akiendelea na mifano hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa Mkurugenzi wa Usajili, Ukaguzi na Upelelezi wa Walipa Kodi, Hashim Kombo Haji aliamuru ripoti hiyo iondolewe na isipelekwe katika uongozi lakini hata hivyo, ripoti hiyo ilipelekwa kwenye uongozi na kilichofuata ripoti haikupelekwa kwenye Bodi ambapo uongozi kwa kibali cha Kamishna Mkuu haikupeleka ripoti hiyo kwenye Bodi ya Mamlaka hiyo.

Ameongeza kwamba, kuna kampuni zilikwenda kukaguliwa na kuonekana kwamba hazikulipa kodi kutoka mwaka 2016 hadi 2021 ambapo ripoti ilipekekwa lakini Kamishna huyo alitoa kauli na kusema mambo ya nyuma yaachwe na badala yake kuangaliwa zaidi taarifa za 2021.

Aidha, alisema kwamba kuna kampuni ya mafuta haikulipa kodi ya lita zenye gharama ya Shilingi Milioni 58 huko Tanzania Bara ambapo uchunguzi ulifanywa na TRA maelezo ya kampuni hiyo ni kwamba fedha hizo haziwezi kulipwa Bara kwa sababu mafuta hayo yameletwa Zanzibar, lakini baada ya Rais kuagiza kufuatiliwa kama kweli fedha hizo zimelipwa Zanzibar ilionekana kwamba fedha hizo hazikulipwa sehemu zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa Mamlala ya Mapato ndio moyo wa Serikali kwani ufanisi wa mamlaka ndio unaopelekea Serikali kuweza kutekeleza majukumu yake ya kimaendeleo na uendeshaji wa Serikali.

Amesema kuwa, ufanisi ukiwa mzuri ndio Serikali inapoweza kutekeleza majukumu yake na kukiwa na tatizo katika Mamla hizo Serikali nzima hufeli katika majuukumu yake.

Mapema Rais Dt.. Mwinyi alipokea taarifa kutoka kwa uongozi wa ZRB lakini hata hivyo alisema kwamba changamoto zote za Bodi zilizoelezwa jukumu bado linabaki katika Mamlaka hiyo husika katika kuzitatua.

Rais Dkt. Mwinyi alisema kuwa tatizo lilitokea wakati wa janga la UVIKO 19 ambapo dunia nzima iliathirika na tayari hivi sasa hali hiyo imeanza kutengamaa lakini hata hivyo, bado kumekuwepo kwa visingizio vya janga hilo katika ukusanyaji wa mapato.

Post a Comment

0 Comments