DAWASA watoa mamilioni ya fedha kupeleka maji Makurunge

NA ROTARY HAULE

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetoa shilingi milioni 147 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji katika Kitongoji cha Makurunge kilichopo Kata ya Kiluvya Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani.
Aidha,kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha zaidi ya wananchi 500 pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Makurunge waliopo katika Kitongoji hicho ambao wamekuwa wakiishi bila huduma ya maji safi na salama kwa muda mrefu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maji katika kitongoji hicho, Ivan Rutatina,amesema kuwa wamekuwa wakiishi eneo hilo bila maji kwa miaka 19 lakini kupatikana kwa ufumbuzi huo ni faraja kwao.
Rutatina,amesema kuwa kutokana na hali hiyo mwaka 2019 waliamua kuunda kamati ya ufuatiliaji wa maji katika Kitongoji hicho kupitia kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo pamoja na DAWASA.

Amesema kuwa,baada ya kupeleka maombi hayo Serikali ilitoa ushirikiano mkubwa na hivyo DAWASA kufika katika eneo hilo kufanya tathimini ya mradi huo na kupata milioni 147.

Amesema,gharama hiyo ilikuwa kubwa kiasi ambacho wananchi walishindwa kumudu na hivyo kuendelea kuishi bila maji jambo ambalo lilikuwa kero kubwa kwa wakazi wa eneo hilo.
Rutatina,amesema Serikali ya Awamu sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inafanya kazi kubwa na imetambua changamoto ya ukosefu wa maji kwa wananchi hao ndio maana imetoa fedha za kutekeleza mradi huo.

Amesema,juhudi zilizofanywa na Serikali kutoa fedha hizo ni kubwa na kwamba wananchi wa Kitongoji hicho wapo tayari kuchangia nguvu kazi ya kuchimba mtaro wa kulaza mabomba ya kupeleka maji hayo.

Amesema,mtaro huo utachimbwa ukiwa na umbali wa kilomita nne kutoka sehemu ya maungio ya maji mpaka kufika katika Kitongoji hicho na kwa maelekezo ya Mhandisi mtaro unatakiwa kwenda chini mita 1.2.
"Tunamshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huu mkubwa wa maji katika Kitongoji cha Makurunge imani yetu kukamilika kwa mradi huu utakuwa mkombozi kwetu," amesema Rutatina.

Mhandisi wa Maji kutoka DAWASA, Zainabu Mwangubi amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo unaanza mara moja kwa kushirikiana na wananchi ambapo mara baada ya kukamilika kwa mtaro huo mabomba yatalazwa kwa ajili ya kupeleka maji.

"Kazi kubwa ni kuchimba mtaro wa kulaza mabomba ya maji ambayo inafanywa na nguvu kazi za wananchi lakini sisi tunashirikiana nao kuhakikisha mtaro unaochimbwa unakidhi vigezo na vifaa vyote tayari vimepatikana na vipo saiti(Site),"amesema Mwangubi.

Diwani wa Kata ya Kiluvya, Aidan Kitare , amemshukuru Rais Samia kwa hatua kubwa ya kupeleka fedha za kutekeleza mradi huo huku akisema adhma yake ya kumtua ndoo mama kichwani inatimia.

Kitare,amewataka wananchi wa Kitongoji hicho kuhakikisha wanatunza miundombinu ya maji ya mradi huo na kwamba wawe tayari kutoa taarifa pale wanapoona mtu anahujumu miundombinu hiyo.

Mmoja wa wananchi wa Kitongoji hicho akiwemo Nyamizi Yassin, amemshukuru Rais Samia kwa kupeleka maji katika Kitongoji hicho na kusema maji wanayotumia sasa ni machafu na wanayapata katika kisima vifupi.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Makurunge Hassan Lusehe amesema, changamoto kubwa katika Shule yake ni maji ambapo kwasasa wanatumia maji ya visima yanayosababisha wanafunzi kuugua magonjwa ya matumbo na ngozi.

Lusehe ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kwa hatua kubwa ya kupeleka maji Shuleni hapo na kusema mradi utakapokamilika utaondoa kero ya maji shuleni hapo na hivyo kufanya wanafunzi wasome katika mazingira bora.

Post a Comment

0 Comments