DCEA yafichua mbinu chafu za kusafirisha dawa za kulevya, ni Watanzania waliokuwa wanadai kwenda kutibiwa India

NA VERONICA MHETA

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kelevya nchini (DCEA) imesema kuwa katika kipindi cha ugonjwa wa UVIKO-19 baadhi ya Watanzania walitumia mwanya huo kujifanya wagonjwa na kwenda kutibiwa nchini India ilhali wakiwa wamebeba dawa za kulevya.
Hata hivyo licha ya kutumia mbinu ya kupata vibali vya kutibiwa nje ya nchi walikamatwa kutokana na intelijensia ya wakaguzi kutoka nchi mbalimbali zinazodhibiti dawa hizo.

Akizungumza jijini Arusha wakati wa utoaji mafunzo kwa watumishi wa idara mbalimbali za Serikali ikiwa ni Uhamasishaji wa Mradi wa Upunguzaji Madhara kwa watumiaji wa Dawa za Kulevya mkoani Arusha, Kamishna Jenerali wa DCEA,Gerald Kusaya amesema wasafirishaji wa dawa za kulevya wana mbinu mbalimbali za kusafirisha dawa hizo, lakini mamlaka hiyo imedhibiti.

Amesema, katika wimbi la ugonjwa wa UVIKO-19 mwaka jana wasafirishaji walilitumia kusafirisha dawa hizo huku wakijifanya wanaumwa wanakwenda kutibiwa nchini India ilhali wakijua kuwa wana dawa wanazipeleka huko.
Aliomba watumishi wa afya kuwa makini wanapotoa vibali vya wagonjwa kusafiri kwani inapotokea msafirishaji wa dawa hizo anakamatwa na dawa za kulevya huku amepata kibali cha matibabu kwenda nje ya nchi unashangaa.

"Haiwezekani mtu anaomba kibali kwenda nje ya nchi anapewa halafu katika ugonjwa wa Covid-19 anaenda kutibiwa, ukimwangalia huyo mgonjwa mwenyewe unajiuliza sana watu wa afya mtusaidie katika hili maana watumiaji wa dawa za kulevya au wasafirishaji wana mbinu nyingi na ukiondoka hata Tanzania salama utakamatwa nje ya nchi na dawa zako na kifungo ni maisha au miaka 20 na 30 jela,"amesema Kamishna Jenerali Kusaya.
Amesema, mamlaka hiyo hadi sasa imeshakamata wafanyabiashara wakubwa kadhaa na wengine wanatumikia vifungo magerezani na kusisitiza kuwa mamlaka hiyo ipo macho usiku na mchana kudhibiti dawa hizo kuingizwa nchini.

Pia amesema kuwa, mwaka jana dawa za kulevya kilo 859 zilikamatwa na kusisitiza kuwa mamlaka hiyo imejipanga vema kukamata dawa mbalimbali zinazoingia nchini ikiwemo bangi na mirungi na ndio maana elimu inatolewa vyuoni na shuleni ili kudhibiti dawa za kulevya vinazoathiri akili.

Wakati huo huo,Mkuu wa Mkoa wa Arusha,John Mongella alitoa rai kwa jamii kuhakikisha wanatokomeza dawa hizo zinazoua nguvu kazi kwa vijana na kusisitiza kuwa Arusha bado kuna changamoto ya kilimo cha bangi maeneo ya milimani, lakini vyombo vya ulinzi na usalama vinapambana ili kudhibiti kilimo hicho sanjari na  kudhibiti maeneo ya mipakani ikiwemo kwenye njia za usafirishaji kupitia mabasi.
Naye mmoja kati ya warahibu wa dawa hizo,Antony Mambepo alishukuru serikali kwa kuweka vituo vya marahibu ili kuwasaidia kupata dawa na kuachana na dawa hizo mbalimbali kwani si athari kubwa kwa jamii ikiwemo familia zao kwani unaweza ukawa mwizi na kusisitiza watumiaji wa dawa hizo wakienda kwenye vituo watapona na kutoa rai kwa jamii kutowatenga watu hao bali washirikishwe katika ujasiriamali ili kujikwamua kiuchumi.

Dkt.Jesca Temu ambaye anatoa ushauri wa watumiaji wa dawa za kulevya kwa warahibu amesema, Mkoa wa Arusha ni mkoa inayoongoza kwa kesi 189 zilizoripotiwa kwa mwaka 2020 kutokana na hali ya jografia iliyopo kutokana na ulimaji wa dawa za kulevya aina ya mirungi huku athari za dawa za kulevya ikiwa kubwa ikiwemo ukimwi,homa ya ini na Uviko -19,ikiwemo athari za uchumi wa kijamii
Ametoa rai kwa jamii kuhakikisha elimu zaidi inatolewa kuhusu athari za dawa hizo ikiwemo viongozi wa dini ili kudhibiti tatizo hilo linaloleta athari kwa jamii ikiwemo vijana wasomi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news