DCEA yajiimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imeeleza kuwa,itaendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kuzuia dawa za kulevya nchini ili kuhakikisha nchi inakuwa salama muda wowote.

DCEA ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015. Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya ambapo kuanzishwa kwa mamlaka kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.

Aidha, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu Februari 17, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.
Hayo yamebainishwa Februari 10, 2022 na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Gerald Kusaya wakati wa mahojiano na runinga ya Taifa ya TBC kupitia kipindi cha Jambo Tanzania.

"Jukumu letu la msingi ni kuzuia, maana yake ni kwamba hatutaki dawa za kulevya ziingie nchini. Katika kuzuia dawa za kulevya nchini, ndiyo maana tunatumia neno maarufu sana la kupambana, tunapambana kuhakikisha nchi yetu ipo salama na hakuna dawa za kulevya zinaingia nchini.

"Tumefanikiwa hasa tukiangalia kipindi cha kuanzia Januari 2021 hadi sasa..katika suala zima la mapambano dhidi ya dawa za kulevya, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini imefanya vizuri sana, pamoja na uchanga wetu, kwa maana ya kipindi cha miaka mitano, hata ukitazama umri wa binadamu bado ni umri mdogo,lakini mamlaka tumefanya vizuri,"amesema Kamishna Jenerali Kusaya.

Amesema,mamlaka kipindi kilichopita cha mwaka 2021 jumla ya kilo 950.8 za dawa za kulevya ambazo zinatoka nje na kuingia nchini zilikamatwa kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama. 

"Katika hizo kilo ni aina mbili za dawa ambazo ziliingia kutoka nje ya nchi ikiwemo heroine kilo 520.2 na kilo 430.6 ilikuwa ni dawa mpya aina ya Methamphetamine,"ameongeza Kamishna Jenerali Kusaya.

Katika hatua nyingine amesema kuwa, waraibu waliojisalimisha na kupatiwa matibabu kwa ukamilifu katika vituo tiba kwa ajili ya waathirika wa dawa za kulevya (MAT Clinics) ili kuachana na matumizi ya dawa za kulevya wataanza kupelekwa vyuo vya ufundi stadi kwa ajili ya kupatiwa ujuzi wa fani mbalimbali nchini.

Amesema, mpango huo utatekelezwa na mamlaka yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo wanatarajia kuwafikia waraibu ambao wamemaliza dawa na hali zao zinaendelea vizuri.

Kwa mujibu wa Kamishna Jenerali Kusaya amesema kuwa,inakadiriwa kuwa hapa nchini kuna watumiaji wa dawa za kulevya zaidi ya 500,000 ambao wanatumia aina mbalimbali za dawa za kulevya huku wengi wao wakiwa wamejificha na hawataki kujitokeza.

Amesema, kati ya idadi hiyo, inayokadiriwa ni waraibu hao 10,600 pekee waliojisalimisha na ndiyo wapo kwenye tiba ya methadone hadi sasa.

Amesema, waraibu wote waliokamilisha dawa wameshaulizwa wanapenda kujihusisha na kazi gani, hivyo watapelekwa vyuo vya ufundi ili kila mmoja aweze kusoma kile anachohitaji kwa kuwa mamlaka kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu wamejipanga kufanikisha hilo.

Amesema, ikiwa wapo ambao wanapenda kujifunza ushonaji baada ya kuhitimu mafunzo watapatiwa vyerehani kwa ajili ya kwenda navyo kuanza maisha mapya huko uraiani na wataanza mwaka huu kwa vijana zaidi ya 200.

Elimu

Pia amesema kuwa, mamlaka imejipanga kuhakikisha inatoa elimu ili kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya kwa kuwaelimisha Watanzania kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari na elimu ya juu pamoja na vyuo ili kuhakikisha kila mmoja anawajibika katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Kamishna Jenerali Kusaya amesema kuwa, elimu hiyo ni jumuishi katika makundi mbalimbali ya Watanzania na kila inapotokea shughuli ya umma wamekuwa wakiomba nafasi ili kufikisha ujumbe kuhusiana na elimu juu ya dawa za kulevya.

Akijibu moja ya swali la mtazamaji,kuhusu wanapopeleka dawa za kulevya ambazo huwa wanakamata, Kamishna Jenerali Kusaya amesema kuwa, dawa yoyote ya kulevya ikikamatwa, lazima kwanza ihifadhiwe katika chumba maalumu na wakati wa kuiteketeza huwa wanafanya wazi kwa kuyashirikisha makundi mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari.

"Dawa yoyote ikikamatwa lazima kwanza ihifadhiwe, ikishahifadhiwa kwenye chumba maalumu, baadaye hukumu ikishatoka, ndipo dawa sasa inaruhusiwa kwenda kuangamizwa.Ni jukumu la mamlaka kwenda kuteketeza dawa hizo. Dawa yoyote lazima iangamizwe katika utaratibu mzuri. Na mara nyingi wakati wa kuziangamiza lazima tutumie wale wenzetu wa viwanda vya saruji, kwa sababu kule ndipo sehemu salama pa kuteketezea,"amesema.

Majukumu ya DCEA

Pia majukumu ya mamlaka ni kufafanua, kuhamasisha, kuratibu na kutekeleza hatua zote zinazoelekezwa katika udhibiti wa dawa za kulevya. Katika kutekeleza majukumu hayo mamlaka inafanya kazi zifuatazo;

i.Kusimamia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa, maazimio na makubaliano katika kudhibiti dawa za kulevya.

ii.Kuandaa na kutekeleza mpango wa Taifa wa kudhibiti dawa za kulevya.

iii.Kutengeneza miongozo inayoelezea tatizo la dawa za kulevya na madhara yake katika jamii;

iv.Kuboresha na kurekebisha sheria na kanuni za udhibiti wa dawa za kulevya;

v.Kuhamasisha udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya ikiwemo kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya, kusambaza taarifa kwa umma na juhudi nyingine za udhibiti;

vi.Kuchukua hatua stahiki za kupambana na biashara ya dawa za kulevya zikiwemo kukamata, kupekua na uchunguzi wa masuala yanayohusiana na dawa za kulevya.

vii.Kuzuia, kupeleleza na kuchunguza uchepushaji wa dawa za tiba zenye madhara ya kulevya pamoja na kemikali zilizosajiliwa kutoka kwenye vyanzo halali wakati huo huo kuhakikisha dawa hizo zinapatikana kwa matumizi ya tiba, biashara na mahitaji ya kisayansi;

viii.Kuanzisha mfumo thabiti wa ukusanyaji taarifa na uchambuzi katika ngazi ya taifa kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya;

ix.Kuhamasisha, kuratibu na kuhakikisha jitihada za ushirikiano wa kimataifa katika kudhibiti wa dawa za kulevya zinaimarishwa;

x.Kufanya, kuwezesha na kuratibu tafiti zinazohusiana na dawa za kulevya;

xi.Kuratibu na kuwezesha wadau wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya;

xii.Kuelimisha na kuhamasisha jamii kushiriki katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya;

xiii.Kutoa mafunzo kwa watendaji wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya, fedha haramu na kemikali bashirifu.

xiv.Kufanya uchunguzi wa sayansi jinai

Post a Comment

0 Comments