DC Serera apokea tani 78.2 za chakula,mafuta ya kula lita 2,220 kutoka World Vision kusaidia shule tisa

NA MARY MARGWE

MKUU wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Dkt.Suleiman Serera amepokea tani 78.2 za chakula pamoja na mafuta ya kula lita 2,220 kutoka World Vision Tanzania kwa ajili ya kuzipatia shule tisa za Kata ya Ruvuremiti na Lobosoit wilayani humo huku vikiwa na thamani ya Shilingi milioni 148.2.

Akizungumza mbele ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngage, Andrea Daniel Ndikoye, mratibu wa mradi wa Shirika la World Vision Tanzania, Gloria Mashingia, wakati akikabidhiwa chakula hicho katika Shule ya Msingi Ngage Kata ya Loibosoit chini ya diwani wake Siria Baraka Koduya, Mkuu huyo amelishukuru shirika hilo kwa msaada huo wa chakula uliolenga kuzisaidia shule tisa za Kata ya Ruvuma na Loibosoit.
Dkt.Serera amesema, Shirika la World Vision Tanzania limetoa chakula jumla ya tani zipatazo 78.2 za chakula, na kubainisha kuwa kati ya hizo tani 50.6 ni za mahindi na tani 27.6 za maharage huku mafuta ya kupikia yakiwa ni lita 2,220.

Amesema, msaada huo utatolewa kwa kipindi cha miezi mitatu mitatu, ambapo jumla ya wanafunzi wapatao 3,696 watanufaika na msaada wa chakula.

Aidha, amesema msaada huo umeletwa kufuatia Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo kuandika barua kwa shirika hilo ikiomba kusaidiwa chakula cha wanafunzi shuleni katika kata zilizoathirika zaidi na suala la ukame, kipindi ambacho wafugaji wengi wamepoteza mifugo yao.

"Kama mnavyofahamu wale wakulima, mnaweza kwenda shambani kulima mkiwa na njaa, wale wafugaji mnaweza kwenda kuchunga huku mkiwa na njaa, au tujiulize mimi na wewe unawezaje kufanya shughuli yoyote ile ngumu tena inayohitahi kutumia zaidi akili kufanya ukiwa na njaa si huwezi kufanya hivyo, tena hakuna kazi ngumu kama kusoma, hivyo watoto wanapokua wamepata chakula shuleni kutasaidia kuwajenga kiakili na hatimaye kuongeza bidii ya kusoma na kuinua kiwango cha ufaulu shuleni," amesema Dkt. Serera.
Aidha, amefafanua kuwa akili na mwili ukichoka watoto hawataweza kusoma na kuelewa, watakua wanaomba tu muda wa vipindi uishe ili waweze kurudi majumbani kwao, huku wakiwa hakuna walichoingiza vichwani mwao, ambapo hata walimu nao watawezaje kufundisha watoto wakaelewa ili hali hawapati chakula.

"Jitihada iliyofanyika na World Vision Tanzania itawezesha sasa kuhakikisha kwamba changamoto hii inatatuliwa na sasa tunaweza kufika mbali zaidi, nitoe rai tu kwenu World Vision Tanzania msiishie hapa, kwani natambua kuwa mradi huu unaishia mwaka 2023, hivyo tuendelee kushirikiana na nikiangalia pale naona mna nembo yenu katika darasa pale," aliongeza Mkuu huyo wa wilaya.

Kupitia Mradi wa Ruvu Remit, World Vision iliona ni vyema ikatoa msaada wa chakula shuleni hususani shule zilizopo tarafa ya Ruvu Remit ili kuhakikisha watoto wanapata chakula katika kipindi hiki ambacho wafugaji wengi wamepoteza mifugo yao.
Aidha, aliwahakikishia shirika hilo kuwa serikali inatambua mchango mikubwa inayotolewa na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo World Vision Tanzania , na hivyo itaendelea kushirikiana nao kikamilifu katika jitihada mbalimbali za kuhakikisha mambo yote yaliyopangwa yanaenda kama ilivyotarajiwa na si vingevyo.

"Nipo hapa sio kwa sababu hii tu, lakini pia kuonyesha kwamba serikali yenu chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ipo kazini na kazi inaendelea, inathamini kikamilifu jitihada na mchango mkumbwa unaotolewa na wadau mbalimbali wa maendeleo kama ninyi World Vision, hivyo nitakuwa mkali sana nitakapobaini chakula hiki kimetumika ndivyo sivyo, si mnafahamu kuwa chakula hiki kimeletwa kwa ajili ya kutumika na wanafunzi na kusaidia kuchangia kukabiliana na upungufu wa chakula waliokua nao," alisisitiza Dkt.Serera.
Kufuatia makabidhiano ya chakula hicho,aliwataka wanafunzi sasa kuhakikisha wanaongeza bidii katika masomo ili kuweza kuwatia moyo wazazi, walezi walimu na hata wadau kama hao wanaojitolea kuwasaidia chakula, kwani serikali inaendelea kuboresha mazingira mazuri ya kusoma, hivyo watakapofaulu wote mambo yatakua mazuri zaidi.

Akisoma taarifa fupi kwa Mkuu huyo wa Wilaya Mratibu wa Mradi huo,Gloria Mashingia alisema Ofisi ya Mkurugenzi Wilaya ya Simanjiro iliandika barua kwa World Vision kupitia mradi wa Ruvu Remit kuomba kusaidiwa chakula cha wanafunzi shuleni.

"Uongozi wetu wa shirika waliweza kuwatembelea viongozi wa wilaya ili kujadili hii changamoto na jinsi ya kukabiliana nazo. Moja ya changamoto zilizoelezwa ni wazazi kushindwa kuchangia chakula shuleni kwa wakati kwa sababu ya mifugo kufa, hali iliyopelekea kipato cha kaya kupungua, hivyo World Vision kupitia Mradi wa Ruvu Remit iliona ni vyema ikatoa msaada wa chakula shuleni hususani shule zilizopo tarafa ya Ruvu Remit ili kuhakikisha watoto wanapata chakula katika kipindi hiki ambacho wafugaji wengi wamepoteza mifugo yao," amesema Mashingia.

Aidha, Mashingia amesema mradi huo umetoa msaada wa chakula shuleni kwa miezi mitatu katika shule tisa (shule saba za msing na shule mbili za sekondari) zilizopo tarafa ya Ruvu Remit, ambapo kila mwezi mradi utatoa mahindi tani 16.9, maharage tani 9.2 na mafuta ya kula lita 740 hivi vyote vina thamani ya sh.milioni 49,416,000.
"Msaada huu tutatoa kwa miezi mitatu ambayo ni mwezi wa tatu, mwezi wanne na mwezi wa tano, kwa miezi yote mitatu tutatoa kiasi cha tani 50.7 za mahindi, tani 27.6 za maharage na lita 2,220 za mafuta ya kula, Msaada huu wote kwa miezi mitatu una thamini ya Shilingi milioni 148,248,000. Jumla ya watoto 3696 watanufaika na msaada wa chakula,"ameongeza Mratibu huyo.

Hata hivyo, alisema Shirika la World Vision Tanzania linajihusisha pia na kusaidia kupambana na majanga mbalimbali kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa maendeleo.

Post a Comment

0 Comments