Maagizo sita ya Serikali kwa wazalishaji, wazambazaji, wafanyabiashara vifaa vya ujenzi, vinywaji baridi nchini

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt.Ashatu Kijaji (Mb) ametoa maagizo sita kwa wazalishaji, wasambazaji na wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi na vinywaji baridi nchini huku akisisitiza kwamba yule ambaye atakaidi maagizo hayo hatua zaidi zitachukuliwa.
"Mosi, ninawaelekeza wazalishaji, wasambazaji na wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi kushusha mara moja bei za bidhaa hizo walizopandisha kiholela na kuuza bidhaa hizo kwa kuzingatia gharama halisi za uzalishaji na usambazaji. Agizo hili linahusu pia bei za vinywaji baridi.

"Pili, ninazielekeza mamlaka zote za udhibiti kuchukua hatua dhidi ya walimbikizaji na wauzaji kupitia mlango wa nyuma wanaosababisha bei za bidhaa kupanda sokoni, ili kuhakikisha kuwa bidhaa zinafika sokoni kwa wakati na kwa bei shindani.

"Tatu,kwa kuwa kitendo cha kupanga bei kati ya washindani ni uhujumu uchumi, ninazielekeza mamlaka husika kuchukua hatua kali dhidi ya wote watakaobainika kupanga bei kwa bidhaa kwa mujibu wa sheria za nchi.

"Nne, ninawaelekeza wazalishaji kuzalisha bidhaa hizo kulingana na uwezo wa viwanda uliosimikwa ili kukidhi mahitaji ya soko,

"Tano, ninawaelekeza wazalishaji wa vifaa vya ujenzi kuweka mifumo mizuri ya usambazaji wa vifaa hivyo ili kuzuia kupanda bei kunakoweza kuzuilika; na

"Sita, ninawaelekeza maafisa biashara wa mikoa kote nchini waendelee kufuatilia kwa karibu mwenendo wa bei za bidhaa mbalimbali kwenye maeneo yao na kuwasilisha taarifa hizo mara kwa mara Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, kupitia Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa ili itakapobidi hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati;

Dkt. Kijaji ameyabainisha hayo jijini Dodoma kupitia taarifa aliyoitoa inayoangazia tathimini ya mwenendo wa uzalishaji, usambazaji na bei za vifaa vya ujenzi na bidhaa nyingine muhimu nchini kwa kipindi kinachoishia leo Februari 7, 2022.

"Gharama halisi za uzalishaji wa saruji haiakisiwi katika bei ya saruji iliyopo sokoni ikilinganishwa na uwiano huo katika nchi jirani na kwingineko duniani.

"Ongezeko la bei ya saruji na nondo halina uwiano halisi na gharama za usafirishaji na usambazaji, bei ya saruji iliyopo sokoni haina uhusiano na mwenendo wa nguvu za utashi wa mlaji na ugavi, na kuna ucheleweshaji wa makusudi wa utoaji wa saruji kutoka viwandani kwenda kwa wasambazaji na wanunuzi wa ndani.

"Hususani wale wadogo, waliokwishalipia saruji husika tofauti na wanunuzi wa nje ambao hupatiwa saruji kwa urahisi zaidi. Pamoja na mambo mengine, hali hiyo hupelekea wasambazaji hao kupandisha bei za saruji ili kufidia gharama zilizotumika kuchukua mzigo,"amefafanua Waziri Dkt. Kijaji.

Kwa mujibu wa Waziri Dkt. Kijaji amesema, taarifa hiyo aliyoitoa leo imejikita kuelezea matokeo ya uchunguzi uliofanywa na wizara kuhusu mwenendo wa uzalishaji na usambazaji wa vifaa vya ujenzi katika kipindi cha mwezi Novemba 2021 hadi Februari 2020.

"Aidha, mtakumbuka kuwa Januari 23, 2022 nikiwa mkoani Shinyanga, nilitoa taarifa kwa umma kuhusu kuadimika kwa vinywaji baridi na hatua zilizochukuliwa na Serikali kudhibiti hali hiyo ambazo napenda kuwataarifu kuwa zimezaa matunda,"amesema Waziri Dkt.Kijaji.

Saruji

Waziri Dkt.Kijaji amesema kuwa, kwa sasa nchi ina viwanda 17 vya saruji vyenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya saruji hapa nchini.

"Hata hivyo, matokeo ya uchunguzi yamebainisha kuwa viwanda vya saruji nchini vinazalisha kwa takribani asilimia 58 tu ya uwezo uliosimikwa wa viwanda hivyo.

"Hii inaashirika kuwa, bado viwanda vya ndani vina uwezo wa kuongeza uzalishaji wa saruji ili kukidhi mahitaji ya ndani ya nchi na kuweka bei shindani ya saruji sokoni,"amesema Waziri Dkt.Kijaji.

Nondo

Kwa upande wa nondo, Waziri Dkt.Kijaji amesema kuwa, hapa nchini kuna viwanda 16 vinavyozalisha nondo na vyenye uwezo wa kuzalisha tani 1,082,788 za nondo za ukubwa mbalimbali.
"Hii ni kwa maana ya nondo za ukubwa wa 16mm, 12mm,10mm na 8mm. Hata hivyo, uchunguzi umeonesha kuwa, uzalishaji wa nondo viwandani kwa sasa hauzidi tani 750,000 pekee,"amebainisha Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji.

Aidha,kwa mujibu wa tathimini iliyofanywa na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Tume ya Ushindani nchini (FCC) juu ya uhaba wa vifaa vya ujenzi nchini na upandaji wa bei kiholela ilibainika kuwa ingawa nondo na bidhaa zinazotokana na chuma zinapatikana kwa uchache, bei zake zimeongezeka sana.

Waziri amesema kuwa,tathmini iliyofanywa imebaini ongezeko la bei za vifaa vya ujenzi hususani saruji na nondo nchini linasababishwa na wazalishaji husika kufanya uzalishaji banifu.

Sambaba na kutokuwa na mfumo wa wazi katika usambazaji wa bidhaa hizo ambapo kuna mnyororo mrefu wa usambazaji wa bidhaa kutoka kiwandani mpaka kumfikia mlaji wa mwisho.

Wakati huo huo, waziri, Dkt.Kijaji amesema kuwa, mwelekeo wa sera za uchumi wa kuachia nguvu za soko huria katika uendeshaji wa biashara ikiwa ni pamoja na Serikali kuachana na jukumu la kupanga bei hauna maana ya kuondoa jukumu la msingi la Serikali kusimamia ushindani wa haki kwenye soko.

"Sisi kama Serikali tuna wajibu wa kudhibiti mienendo hadaifu au kandamizi ya wazalishaji wa bidhaa na wafanyabiashara kwenye soko ikiwa ni pamoja na upandishaji holela wa bei.

"Hivyo basi, Serikali haitavumilia tabia ya wafanyabiashara wachache kuanzia wazalishaji hadi wasambazaji wenye dhamira ovu ya kuwaumiza wananchi kwa kujiamulia kupandisha bei za bidhaa bila kufuata taratibu kwa manufaa yao binafsi,"amefafanua Waziri Dkt.Kijaji.

Post a Comment

0 Comments