Majahazi ya mizigo Bandari ya Kipumbwi wilayani Pangani yatumika kusafirisha abiria kwenda Zanzibar, TASAC yatoa onyo kali

NA HADIJA BAGASHA

BANDARI ya Kipumbwi iliyopo wilayani Pangani mkoani Tanga imetajwa kusafirisha abiria kwa kutumia majahazi ya mizigo kutoka Pangani hadi Zanzibar jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa watu wanaosafiri, hivyo watakaobainika kuendelea na tabia za namna hiyo watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kutozwa faini ya shilingi laki tano au kifungo cha miaka mitatu jela. 
Kutokana na hali hiyo, Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesema kwamba hawatasita kuwachukulia hatua kali manahodha wanaoendesha vyombo vya kubebea mizigo iwapo watabainika wanapakia abiria kwenye vyombo hivyo. 

Takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwaka jana watu nane walifariki dunia walipokuwa wakitumia usafiri wa aina hiyo.
Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) limepiga marufuku usafiri wa majahazi ya mizigo ambayo yamekuwa yakitumiwa katika eneo hilo kubeba abiria kwa kile walichodai ni hatari kwa maisha ya watu na ni kinyume cha sheria.
Kauli hiyo imetolewa Februari 9,2021 na Ofisa Mkaguzi na Mdhibiti Mfawidhi wa Shirika hilo mkoani Tanga,Kapteni Christopher Shalua wakati wa kikao chake na wavuvi wanaofanya shughuli zao katika maeneo ya Kipumbwi na Mkwaja wilayani Pangani ambapo amesema lazima sheria zilizopo kwa vyombo vya usafiri majini vifuate sheria zilizowekwa na mamlaka husika. 
Shalua amesema, vitendo vya kusafirisha watu kuchanganya na mizigo vimekuwa vikishamiri sana hasa eneo la Kipumbwi huku akieleza watahakikisha wanakomesha tabia hizo ambazo zimekuwa wakati mwingine zikigharimu maisha ya watu. 

"Leo tumekuja hapa Kipumbwi na Mkwaja kwa lengo la kutoa elimu ya kujikinga na kujua usalama wenu na namna ya kujiokoa kwa kutumia vifaa maalumu mnapokuwa baharini, jambo kubwa niwasihi mfuate sheria za leseni zenu, "amesisitiza Shalua. 

Aidha, amesema pia ambao watabainika kuendelea na tabia za namna hiyo watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kutozwa faini ya shilingi laki tano au kifungo cha miaka mitatu jela. 

Ameongeza kuwa, "tukikukamata chombo chako kimebeba abiria badala ya mizigo faini ni laki tano au tunakupeleka mahakamani au vyote mahakama tunakupa kifungo kisichozidi miaka mitatu,"amesema 

Kwa upande wake Kapteni Hamis Mohamed Ali ambaye ni ofisa mkuu wa vyombo vidogo na mabaharia kutoka Mamlaka ya Usafiri baharini Zanzibar (ZMA) amesema kuwa ajali zimekuwa nyingi kwa vyombo vya mizigo ambavyo vinapakia abiria huku akithibitisha watu nane waliofariki kwa ajali ya kutumia vyombo hivyo wakati wa kusafiria. 

Kapteni Hamis amewasisitiza manahodha kuhakikisha wanatumia vyombo vyao katika matumizi yaliyokusudiwa huku akiwataka wahakikishe wanasajili vyombo vyao ili kuweza kujua takwimu sahihi ya vyombo vya uvuvi, mizigo na utalii ambapo hali hiyo itasaidia katika kuweka takwimu za nchi. 
Hata hivyo, amwwataka watumiaji wa vyombo vya majini kuacha tabia ya kutumia vilevi pindi wawapo baharini ikiwemo sigara, bangi na pombe. 

"Watumiaji wa vilevi mchukue tahadhari kwani upo uwezekano mkubwa wa kupata majanga mnapotumia ulevi muwapo baharini jihadharini ili kuhakikisha mnalinda usalama wenu, "amesisitiza Kapteni Hamis. 

Kwa upande wake wananchi wa Kipumbwi wameomba serikali kupelekewa boti ya abiria watakayoitumia kwa kile walichodai eneo hilo lipo karibu na Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments