Miaka 45 ya CCM, Arusha wajivunia kasi ya maendeleo Karatu

NA SOPHIA FUNDI 

MAADHIMISHO ya miaka 45 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha yamefanyika wilayani Karatu kwa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo.
Miradi hiyo iliyotembelewa na Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Arusha ni pamoja na miradi ya elimu katika Shule ya Sekondari Karatu na Ganako ambayo ni baadhi tu ya miradi katika wilaya hiyo kati ya miradi 60 ya ujenzi wa vyumba vya madarasa iliyotekelezwa kwa fedha za mpango wa Uviko-19 shilingi bilioni 1.2.

Mwenyekiti wa CCM  Mkoa wa Arusha, Zellote Steven amesema kuwa chama kinajivunia kuadhimisha miaka 45 ikiwa na mafanikio makubwa kwa wananchi wake kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kamati hiyo ya siasa ilitembelea pia majengo ya hospitali ya wilaya iliyofikia hatua ya mwisho ya ujenzi.
Mwenyekiti huyo wa Mkoa aliuagiza uongozi wa Wilaya ya Karatu kuhakikisha hospitali hiyo inaanza mara moja kutoa huduma kwa wananchi wake, kwani kiu ya wananchi ni kuona wanaanza kupata huduma katika hospitali hiyo na si kusikia kila siku ujenzi unaendelea.

"Mheshimiwa Rais alikuwa kwenye ziara mwezi Oktoba alitoa maagizo ujenzi wa hospitali hiyo ukamilike, hivyo uongozi wa wilaya hakikisheni hospitali hiyo inaanza kutoa huduma kwa wananchi hatutapenda kusikia tena Rais anakuja Arusha akakuta maagizo yake hamjayatekeleza,"amesema Zellote. 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Dadi Kolimba amewataka wananchi kuwapeleka watoto wote waliofaulu kwenda shule ambapo amesema wataanza msako wa nyumba kwa nyumba,kata kwa kata kuwabaini wanafunzi ambao hawajaripoti shuleni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news