Miaka 45 ya CCM, Rais Samia ataja mambo mazito

NA FRESHA KINASA

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema kwa miaka 45 ya kuzaliwa kwa chama hicho maendeleo mbalimbali yametekelezeka nchini.

Sambamba na kudumisha amani, demokrasia na utawala bora huku akipongeza kazi kubwa ya kizalendo na ya heshima iliyofanywa na waasisi wa Taifa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Aman Karume.
Ameyasema hayo leo Februari 5, 2022 katika kilele cha maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi ambayo kitaifa yamefanyika uwanja wa Kumbukumbu ya Karume Mjini Musoma mkoani Mara. 

Pia amebainisha kwamba chama hicho kimeleta mageuzi makubwa ya kimaendeleo nchini na kitaendelea kutekeleza ilani yake ya uchaguzi kwa masilahi mapana ya Watanzania. 

Mheshimiwa Samia amesema, maendeleo yaliyopatikana ni pamoja na kuimarisha shughuli za uwekezaji. 

Uhakika wa huduma ya nishati, kuendeleza na ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. 

Kuimarisha sekta ya usafiri na usafirishaji, kuendeleza ujenzi wa reli ya kisasa. 

Viwanja vya ndege, kuimarisha usafiri katika maziwa, kutengeneza meli za abiria na mizigo, kuimarisha mazingira bora ya utoaji wa elimu ili kila mtoto apate haki ya elimu.

Mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na kuimarisha huduma za afya kwa kuimarisha utoaji wa vifaa tiba, upatikanaji wa dawa, kudhibiti janga la ugonjwa wa Corona huku akisistiza watanzania kuendelea kuchanja. 

Pia kujenga miundombinu na usambazaji wa maji vijijini na mijini, uendelezaji wa uvuvi na Kilimo. 

Aidha, Mheshimiwa Samia amesema kuwa, Tanzania ilifanikiwa kufikia uchumi wa Kati kabla ya miaka sita kama ilivyotarajiwa jambo ambalo ni la kujivunia, na akabainisha kwamba chama kimeendela kuaminika kwa Watanzania kutokana na utekelezaji wa ilani za chama hicho na pia chama hicho kimeendelea kukuza uwezo wake wa kiuchumi, kupandisha mishahara ya wafanyakazi wake na kulipa madeni mengi. 

Aidha, Mheshimiwa Samia amewataka wanachama wa chama hicho kushiriki katika uchaguzi ndani ya chama hicho kwa uadilifu mkubwa na kwamba jicho la chama litafuatilia kila hatua katika uchaguzi huo. Huku akishukuru chama hicho kufuatilia utekelezwaji wa ilani maeneo mbalimbali nchini na kwamba matembezi ya Mshikamano yaliyofanyika yamekusanya Shilingi Milioni 300 ambazo zitatumika kutengeneza kadi za kielektroniki.

Pia, amewataka Watanzania kuimarisha ulinzi wa nchi kwa kudumisha amani na utulivu.

Sambamba na kushiriki kikamilifu katika sensa na kufanya kazi kwa bidii kupambana.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amesema kuwa, wakati chama hicho kinazaliwa mwaka 1977 kilikuwa na wanachama 500,000. Ambapo kwa sasa chama kina wanachama milioni 12.

Ameongeza kuwa, katika kuendana na teknolojia Halimashauri Kuu ya Chama hicho iliazimia kuingia kwenye mfumo wa kutumia kadi za kielektroniki ambapo mpaka sasa wanachama waliojiandikisha ni zaidi ya milioni mbili na zitakuwa na faida ikiwemo kutoa takwimu sahihi za wanachama, kuongeza mapato kutokana na ulipaji wa ada kwa wanachama, kuwasaidia kupata huduma mbalimbali na kuwatambulisha katika jamii. Huku akibainisha kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu kwa kushushwa ngazi za chini.

Amesema kuwa, kila baada ya miaka mitano sherehe hizo zitakuwa zikifanyika na kwa kila mwaka zitakuwa za kawaida.

Amesema, lengo la kufanya maadhimisho haya ya miaka 45 kitaifa mkoani Mara ni kusherehekea miaka 100 ya kuzaliwa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere na pia kuenzi mchango wa waasisi wanne waliotokea Mara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news