Mifuko ya udhamini Benki Kuu inavyosomesha wanafunzi kwa kulipia gharama zote bila kurejesha mkopo

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa wito kwa vijana wote wa kitanzania hasa wanafunzi wa kike kusoma kwa bidii ili waweze kufaulu kwa kiwango cha juu na hatimaye kupata ufadhili masomo ya elimu ya juu katika maeneo mbalimbali hususani fani za Uchumi na Fedha.
Afisa Mkuu Rasilimali Watu, Kurugenzi ya Utumishi na Maendeleo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Kashindye Sekule Phelician ameyasema hayo leo Februari 17, 2022 katika siku ya nne ya mafunzo kwa waandishi wa habari za uchumi na biashara yanayoendelea katika Ukumbi wa Benki Kuu tawi la Mbeya.

Ni mafunzo ya siku tano yanayoratibiwa na Benki Kuu ambapo Bi.Phelician alikuwa akiwasilisha mada ya Maendeleo ya Mifuko ya Udhamini wa Elimu ya juu inayodhaminiwa na Benki Kuu ya Tanzania ambapo amesema, bidii yao itawawezesha kunufaika na udhamini wa asilimia 100.

"Hii inawezekana kama tulivyoona kwa vipindi vya miaka ya hivi karibuni ufaulu wa wanafunzi wa kike kwenye fani za sayansi na hisabati, na nyinginezo ya mitihani ya taifa kidato cha sita umekuwa ukiongezeka. Jambo la kufurahisha ni kwamba, ufadhili huu ni asilimia 100 na sio mkopo, na mnufaika hatatakiwa kufanya marejesho yoyote mara atakapomaliza masomo.

"Ombi kwa wazazi na walezi tuwawekee vijana wetu mazingira mazuri yatakayowawezesha kufanya vizuri katika masomo yao bila kujali jinsia.Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikitoa misaada kwa shughuli mbalimbali za kijamii nchini Tanzania ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji kwa jamii inayoizunguka (Corporate Social Responsibility),"amefafanua Bi.Phelician.

Anasema kuwa, misaada imekuwa ikitolewa kwa njia ya udhamini wa elimu ya juu kwa kutambua umuhimu wa elimu katika maendeleo ya nchi yetu kupitia mifuko miwili ya udhamini inayosimamiwa na Benki Kuu:

Bi.Phelician ameitaja mifuko hiyo kuwa ni Mfuko wa Udhamini wa Gilman Rutihinda (The Gilman Rutihinda Trust Fund) na Mfuko wa Udhamini wa Elimu ya Juu wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

Mfuko wa Udhamini wa Gilman Rutihinda

Akizungumzia kuhusu Mfuko wa Udhamini wa Gilman Rutihinda amesema, ulianzishwa Machi Mosi,1994 kwa lengo la kumuenzi aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu wa Awamu ya Tatu marehemu Gilman Rutihinda kutokana na mchango wake wa kitaalamu katika maendeleo ya kiuchumi nchini, kwa kuleta mageuzi ya Sekta ya Fedha.
"Mfuko huu unaendeshwa kwa kutumia bajeti ya Benki Kuu ya mwaka iliyotengwa kwa uwajibikaji wa taasisi kwa jamii (Corporate Social Responsibility),"anasema.

Lengo

Afisa huyo anabainisha kuwa,lengo la mfuko ni kutoa udhamini wa elimu ya chuo kikuu kwa shahada za uzamili kwa wanafunzi waliopata ufaulu wa juu kupitia fani za Uchumi na Fedha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Sambamba na kuendesha mihadhara ya kitaaluma ya kumbukumbu ya Gilman Rutihinda inayohusu uchumi na sekta ya fedha.

Walengwa ni nani?

Kwa mujibu wa Bi.Phelician anasema,ufadhili hutolewa kila mwaka kwa wanafunzi wawili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliomaliza shahada ya kwanza katika fani ya Uchumi na Fedha na kupata ufaulu wa juu.

Anafafanua kuwa, ufadhili hutolewa kwa ajili ya kuendelea na masomo ya shahada ya uzamili kwenye fani hizo.

"Majina ya wanafunzi wenye ufaulu wa juu katika fani hizo huchukuliwa moja kwa moja toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwenye vitengo husika. Ufadhili ulianza rasmi kutolewa kwa wanafunzi bora katika kipindi
cha mwaka 1995/96,"anasema Bi.Phelician.

Je kuna mafanikio?

"Ndiyo, yapo mafanikio mbalimbali. Hadi sasa, jumla ya wanafunzi 39 wenye ufaulu wa juu daraja la kwanza na la pili katika fani za Uchumi na Fedha wamekwishanufaika na mfuko katika masomo yao ya shahada za uzamili.

"Kati yao wanufaika saba tu ni wanawake, na wanufaika 32 ni wanaume ambapo tayari wanufaika 35 wameshakamilisha masomo hayo kwa ufaulu wa juu na wanalitumikia taifa katika njanja mbalimbali.

"Kati yao, wanufaika saba ni waajiriwa wa Benki Kuu ya Tanzania wakiwemo wakurugenzi, mameneja na wataalamu ambao ni maafisa katika ngazi mbalimbali,"anasema Bi.Phelician.

Pia anasema kuwa, mihadhara mbalimbali ya kumbukumbu za Gilman Rutihinda imekuwa ikifanyika toka mwaka 1995 na mada mbalimbali za kiuchumi kujadiliwa.

"Hadi sasa jumla ya mihadhara saba inayohusu mada mbalimbali za kiuchumi na fedha imeendeshwa katika vipindi tofauti tofauti,"anasema.

Mfuko mwingine

Akizungumzia kuhusu Mfuko wa Udhamini wa Elimu ya Juu wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius K. Nyerere (Mwalimu Julius K. Nyerere Memorial Scholarship Fund), Bi.Phelician anasema,ulianzishwa na Benki Kuu tarehe 12 Oktoba, 2009 kwa ajili ya kuenzi mafanikio ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika sekta ya elimu.

"Mfuko huu ulianza kwa kuchangiwa fedha na Benki Kuu ya Tanzania na taasisi zingine za fedha, viongozi wastaafu, wafanyakazi wa Benki Kuu na wananchi wengine kupitia harambee.

"Fedha hizo ziliwekezwa kwenye Dhamana za Serikali (Treasury Bill na Bond) ili mfuko uwe endelevu na faida inayopatikana tu ndiyo inayotumika kufadhili wanafunzi katika vyuo vikuu hapa nchini.

"Mfuko ulizinduliwa rasmi mwaka 2012 na kuanza kutoa ufadhili katika kipindi cha mwaka 2013/14,"afafanua Bi.Phelician.

Pia anasema, ufadhili huo unatarajia kuongeza hamasa kwa wanafunzi wa kike hapa nchini wenye ufaulu wa juu katika masomo ya Hisabati na Sayansi, ili kujiendeleza kwenye masomo ya shahada na uzamili.

"Hii ni kwa sababu idadi ya wanafunzi wa kike kwenye masomo hayo imekuwa chini kwa muda mrefu. Hivyo ilichukuliwa wanafunzi kike kama kundi lenye uhitaji.

"Ufadhili huu utasaidia kuhamasisha wanafunzi hasa wa kike kufanya vizuri kwenye masomo hayo, na hivyo kuleta usawa au uwiano wa kijinsia kitaaluma kwenye masomo haya muhimu yanayochangia maendeleo ya taifa,"anasema Bi.Phelician.

Anasema, ufadhili huo unajumuisha gharama zote za ada, pesa za kujikimu,mafunzo ya vitendo na vifaa vya kujifunzia ikiwemo kompyuta mpakato (laptop).

Anaendelea kufafanua kuwa,ufadhili unatolewa kwa wanafunzi raia wa Tanzania wenye ufaulu wa kiwango cha juu waliosajiliwa vyuo vikuu nchini vinavyotambulika na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

"Idadi ya wanafunzi wanaofadhiliwa na mfuko huu umeongezeka toka wanafunzi sita kama ilivyokuwa hapo awali hadi wanafunzi 10 kuanzia mwaka huu wa fedha wa 2021/2022,"anasema.

Bi.Phelician anasema asilimia 50 ya ufadhili wa masomo Shahada ya Kwanza ni kwa ajili ya wanafunzi wa kike tu kwa masomo ya Hisabati na Sayansi.

Huku asilimia 50 nyingine ya ufadhili kwa masomo ya Shahada ya Kwanza ikiwa ni kwa wanafunzi wa kike na kiume katika Masomo ya Hisabati, Sayansi, Uchumi, TEHAMA, Uhasibu na Fedha.

"Ufadhili kwa masomo ya Shahada ya Pili (Uzamili) unawalenga wanafunzi wa kike na kiume katika masomo ya Hisabati, Sayansi, Uchumi, TEHAMA, Uhasibu na Fedha,"anaeleza Bi.Phelician.

Vigezo

Anasema, vigezo vya udhamini kwa shahada ya kwanza ambapo asilimia 50 ya ufadhili inawahusu wanafunzi wa kike raia wa Tanzania, wanapaswa kuwa na ufaulu wa juu wa daraja la kwanza miongoni mwa wanafunzi kumi bora kitaifa wa kidato cha sita kwenye masomo ya Hisabati na Sayansi kwa mwaka husika.

"Pia wawe wamepata udahili kwa masomo ya shahada ya kwanza fani za Hisabati na Sayansi katika vyuo vilivyopo nchini (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) na vinavyotambulika na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU),"anasema Bi.Phelician.

Wakati huo huo akizungumzia, vigezo vya udhamini kwa Shahada ya Uzamili (Master’s Degree) anasema kuwa, inawahusu wanafunzi wa kike na wa kiume raia wa Tanzania wenye umri usiozidi miaka 35.

Anasema, wanafunzi hao wanapaswa wawe wenye ufaulu wa juu katika shahada ya kwanza (GPA 4.0 na zaidi) kwa kozi za Hisabati, Sayansi, Uchumi, TEHAMA, Uhasibu na Fedha.

Pia wawe wamepata udahili wa kusoma fani hizo katika vyuo vilivyopo nchini (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) na vinavyotambulika na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).

Muundo

Akizungumzia kuhusu muundo wa uendeshaji wa mfuko anasema, ili kuhakikisha kuwa udhamini unatolewa kwa ufanisi, mfuko unaendeshwa na Bodi ya Wadhamini (Board of Trustees) inayoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ambaye ni Gavana wa Benki Kuu, yenye jukumu la kutoa mwongozo wa shughuli za mfuko kwa kuzingatia sera za mafunzo nchini.

Wengine ni Kamati ya Kutoa Udhamini (Scholarship Awards Committee) inayosimamia mfuko,kuratibu utoaji wa udhamini na kupendekeza kwa Bodi ya Wadhamini.

"Pia Sekretarieti ni sehemu ya majukumu ya Benki Kuu inayoratibu utekelezaji wa kazi za mfuko pamoja na kutoa ripoti mbalimbali.Na kuna Mweka Hazina wa Mfuko (Fund Treasurer).

"Wajumbe wengine wa Bodi (Board of Trustees) pamoja na Kamati (Scholarship Awards Committee) za mfuko ni pamoja na Naibu Gavana (EFP) na Viongozi wengine toka Benki Kuu ya Tanzania akiwemo mwakilishi toka Taasisi ya Mwalimu Nyerere, mwakilishi toka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (Tanzania Bara).

"Mwakilishi toka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (Zanzibar),Mwakilishi toka Chama cha Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), Mwakilishi toka Tume ya Vyuo Vikuu (TCU),Mwakilishi toka Bodi ya Mikopo ya Elimu (HESLB)
na Mwakilishi toka Familia ya Mwalimu Nyerere,"anasema.

Nitapataje taarifa?

Bi.Phelician anasema, matangazo ya ufadhili hutolewa katika vyombo ya habari ikiwemo magazeti, radio, televisheni, mitandao ya kijamii (YouTube, Twitter na Facebook) na tovuti ya Benki Kuu.

Kwa upande wa Shahada ya Kwanza anasema, orodha ya wanafunzi 10 bora kidato cha sita kwa mwaka husika huchukuliwa toka Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA).

Huku kwa upande wa Shahada ya Uzamili (Masters) anasema, maombi ya ufadhili kwa shahada ya uzamili hukaribishwa ambapo fomu za maombi hupatikana kwenye tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania(www.bot.go.tz).

Kuna mnufaika yeyote?

Bi.Phelician anasema, tangu kuanzishwa kwa mfuko huo mwaka 2013/14, jumla ya wanafunzi wa Kitanzania 62 wamepata ufadhili.
Anasema, kati yao 43 ni wanawake na 19 ni wanaume ambapo kati yao wanafunzi 16 wamepata ufadhili wa masomo ya fani ya Udaktari.

"Huku wanufaika 37 wamekwishamaliza kozi zao na 25 wanaendelea na masomo yao katika vyuo vikuu vinavyotambulika katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,"anasema.

Benki inawafuatilia?

Bi.Phelician anasema, benki imekuwa ikifuatilia maendeleo ya wanafunzi wanufaika wanaofadhiliwa na mfuko kwa kuomba taarifa za maendeleo (academic progress) toka vyuoni kila baada ya muhula kuisha.

"Ufuatiliaji unafanyika ili kuhakikisha wanufaika wa mfuko wanasoma kwa bidii na wanapata ufaulu wa juu, ambao si chini ya alama ‘B’.Pia wanasoma kozi iliyoidhinishwa kwa ufadhili tu, na wanakuwepo chuoni na kuhudhuria masomo muda wote,"anasema.

Changamoto na matarajio

Anasema miongoni mwa changamoto ni kwamba, zoezi la uchambuzi huchukua muda mrefu, kwa vile uchambuzi unahusisha maombi yote yaliyopokelewa na mfuko ambayo ni mengi yakiwemo yaliyokidhi na yasiyokidhi vigezo.

"Hivyo, benki inafikiria kuboresha mchakato huu siku za mbeleni kwa kutumia njia ya kielektroniki, kwa kujifunza toka taasisi zingine za Serikali ambao tayari wameanza kutumia mifumo ya kielektroniki katika kupokea na kuchambua maombi ya wanafunzi,"anasema Bi.Phelician.

Pia anasema, elimu kuhusu mifuko hiyo bado ipo kwa kiwango cha chini nchini, kwani bado kunauhitaji hamasa kwa wanafunzi wa madaraja ya chini kuongeza bidii katika masomo yao ili kuweza kupata fursa ya ufadhili.

"Kwa kuliona hilo, benki itaendelea kuelimisha umma kuhusu miongozo na taratibu za mifuko hii ya udhamini wa elimu ya juu kwa kutumia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa matangazo ya ufadhili katika vyombo mbalimbali vya habari.

"Miongoni mwa vyombo hivyo ni magazeti, radio, televisheni na mitandao ya kijamii kama YouTube, Twitter na Facebook ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania.

"Sambamba na kuendelea kutoa machapisho na vipeperushi mbalimbali juu ya udhamini wa mifuko hii inayodhaminiwa na Benki Kuu na kuvisambaza hadi shule za sekondari ikiwemo za kata,"anasema Bi.Phelician.
Akizungumzia changamoto nyingine, Bi.Pheliciana anasema, nafasi za udhamini zinazotolewa bado ni chache ukilinganisha na idadi ya wanafunzi wenye ufaulu wa juu waliokidhi vigezo vya kupata udhamini kwa sababu ya ufinyu wa bajeti.

Kutokana na changamoto hiyo, anasema Benki Kuu itaendelea kuwekeza kwenye Dhamana za Serikali (Bonds and Treasury Bills) ili kuongeza uwezo wa kifedha wa Mfuko wa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na itafanya tathmini ya uwezo wa mfuko ili kuongeza nafasi za ufadhili kulingana na mapato ya uwekezaji uliofanyika.

Pia anasema, benki inatafuta njia nyingine mbadala zitakazosaidia kuuongezea mfuko uwezo wa kifedha ili kuongeza idadi ya ufadhili kwa wanafunzi wenye ufaulu wa juu kama harambee.

Anasema, wanatamani kuona wanatoa ufadhili kwa wanafunzi wenye uhitaji zaidi. "Pamoja na kutoa ufadhili kwa wasichana kama kundi lenye uhitaji mfuko utaendelea kutoa kipaumbele kwa wanafunzi toka shule za Serikali wenye ufaulu wa juu, pale wanapopata ufaulu wenye uwiano sawa na wale wa shule binafsi.

"Pamoja na kuhamasisha shule za wanafunzi wenye uhitaji na kuwapa kipaumbele wanafunzi bora wenye uhitaji. Benki Kuu itaendelea kutekeleza mifuko hii ya ufadhili kama sehemu ya kusaidia huduma kwa jamii,"anasema.

Bi.Phelician anasema, changamoto nyingine ni kwamba Benki Kuu haina jukwaa la mawasiliano linalowaunganisha wanataaluma mbalimbali walionufaika na mifuko hiy ya ufadhili ili kuwawezesha kupata maoni kwa ajili ya maboresho.

Anasema, kutokana na hali hiyo, benki ipo kwenye mchakato wa kutengeneza na kutekeleza mfumo wa kielektroniki wa mawasiliano wa kitaaluma kwa kuwaunganisha pamoja wanufaika wa mifuko (ALUMNI).

"Benki Kuu itaanza kuwashirikisha wanufaika wote waliomaliza masomo yao kwenye shughuli zote za mifuko ikiwa na lengo la kutoa hamasa kwa wanafunzi wa sekondari na vyuo kusoma kwa bidii na kupata ufaulu wa juu ili waweze kupata ufadhili,"anasema.

Maboresho

Bi.Phelician anasema, mifuko hiyo imefanyiwa maboresho kutokana na maoni ya wadau mbalimbali kwani nafasi za ufadhili wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere zimeongezwa kutoka wanafunzi sita hadi kufikia wanafunzi 10 na utekelezaji wake umeanza mwaka huu wa fedha.

"Ikiwemo kutumia zaidi mitandao ya kijamii kama YouTube, Twitter na Facebook kama mojawapo ya njia za kuelimisha umma na kutoa matangazo mbalimbali ya ufadhili. Hii imesaidia wadau wengi kupata habari ikiwemo wanafunzi bora.

"Pia kuwatumia wanufaika katika kuelimisha umma kama 'documentary' kwenye vyombo vya habari kuhusu ufadhili na Maonesho ya Sabasaba na Nanenane. Tumeandaa rasimu ya mwongozo na taratibu za ufadhili wa Mfuko wa Gilman Rutihinda na mara zitakapoidhinishwa wanufaika wa mfuko watarudisha fadhila kwa benki na umma,"anasema Bi.Phelician.

Post a Comment

0 Comments