Mwaka mmoja bila Maalim Seif, Rais Dkt.Mwinyi atoa neno

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad ataendelea kukumbukwa kutokana na uongozi wake madhubuti.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika salamu za pole alizozituma kwa familia, ndugu jamaa na marafiki, wananchi pamoja na wanachama na viongozi wa Chama cha ACT Wazalendo kwa kutimia mwaka mmoja tangu kutokea kifo cha marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Katika salamu zake hizo za pole, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa anaungana na ndugu, jamaa na marafiki, wananchi pamoja na wanachama na viongozi wa Chama cha ACT Wazalendo katika siku hii ya leo kwa kuendelea kumuombea dua kiongozi huyo ili Mwenyezi Mungu amuondoshee adhabu za kaburi na kumuweka mahala pema peponi, Amin.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameendelea kusisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kumuenzi Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad yeye pamoja na familia yake kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii hapa nchini.

Hadi mauti yanamfika marehemu Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa Mwenyekiti wa Chama Cha ACT Wazalendo.

Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad aliyezaliwa Oktoba 22, 1943 na alifariki dunia mnamo Februari 17, 2021 katika Hospitali Kuu ya Muhimbili jijini Dar-es-Salaam ambako alikuwa amelazwa tokea tarehe 9 Februari, 2021 akipatiwa matibabu.

Post a Comment

0 Comments