Mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia: Sekta ya Habari na Mawasiliano yatajwa kustawi kwa kasi nchini

NA GODFREY NNKO

WADAU mbalimbali wa Sekta ya Habari na Mawasiliano nchini wamekiri kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeonesha uthabiti na nia njema inayolenga kuvisimamia vyombo vya habari viweze kutimiza majukumu yake ya kutoa habari, kuelimisha na kuburudisha.

Sambamba na kuvipa uwanda mpana vyombo hivyo viweze kuchapisha na kutangaza habari mbazo zitakuwa na mwelekeo chanya kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Vyombo vya habari nchini zikiwemo redio, magazeti, majarida, televisheni,mitandao ya kijamii, filamu, video, intaneti, picha, vipeperushi, katuni na mabango kadri wasimamizi wake wanavyovitumia kwa weledi na umakini vimekuwa vikitoa mchango mkubwa katika kuunganisha jamii, Taifa na hata kusaidia kuharakisha maendeleo kupitia vipindi na taarifa mbalimbali.
Hayo yamebainishwa Februari 19,2022 kupitia mjadala wa Kitaifa kuhusu Maendeleo katika Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ulioratibiwa na Watch Tanzania kwa ufadhiliwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Mjadala huo jumuishi ukiangazia kuelekea mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani kupitia Zoom uliwakutanisha kwa pamoja viongozi, wadau wa Sekta ya Habari na Mawasiliano,wananchi, wanataaluma kutoka ndani na nje ya Tanzania huku ukirushwa mubashara kupitia runinga mbalimbali za mitandaoni.

Katika mjadala huo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia alichukua nafasi hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa mageuzi makubwa kupitia sekta hiyo.

"Natoa pongezi za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunganisha Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Ofisi ya Habari Maelezo, maana kilikuwa kilio cha watu wengi.

"Mafanikio mengine ni kwamba tumeanza kutoa semina kwa wanahabari na wahariri kuongeza ufanisi zaidi katika kazi zao, kikao cha kwanza cha semina tulifanya pale TCRA na semina zingine zitaendelea kutolewa,"anafafanua Mheshimiwa Waziri Nape.

Joyce Mhavile

Miongoni mwa washiriki na wachangiaji katika mjadala huo ni Mkurugenzi Mtendaji wa ITV na Redio One, Bi.Joyce Mhavile amesema kuwa,kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia kuna mengi ya kujivunia kupitia Sekta ya Habari na Mawasiliano.

"Mwanzo wa urais wa Samia Suluhu Hassan umeonesha nia na dhamira thabiti ya kuona nchi yetu inaongozwa kwa kuzingatia sheria zilizopo, lakini bila kwenda kinyume na misingi ya utawala bora na ubinadamu kwa ujumla, tunamshukuru sana. Upande wetu sisi kama vyombo vya habari binafsi mengi mazuri yameonekana, ikiwa ni pamoja na Serikali kutoa maamuzi ambayo yameleta ahueni kwa vyombo vyetu kwa ujumla na wanahabari.

"Ni ukweli usiopingika kwamba Rais Samia ameonesha uthabiti na nia njema ya Serikali yake pamoja na yeye mwenyewe binafsi kuvifungua minyororo vyombo vya habari nchini,"amesema Bi.Mhavile.

Bi.Mhavile anafafanua kuwa,Mheshimiwa Rais Samia amekuwa msikivu kwa hoja, "kwa mfano sheria za vyombo vya habari ameonesha usikivu sana, kiasi cha kuagiza marekebisho yafanyike pale anapoona kweli marekebisho ni muhimu na hiyo ifanyike kwa kuwashirikisha kadri inavyowezekana wadau wote husika na matokeo chanya yameanza na yanaendelea kuonekana.

"Kwa maana hiyo kiongozi Samia (Rais Samia) amejipambanua kama ni kiongozi anayeamini katika kuthamini uongozi wa pamoja kwa maana ya hekima na maoni ya watu mbalimbali,"amefafanua Bi.Mhavile.

Wakati huo huo, Bi.Mhavile ameonesha kufarijika zaidi na uongozi wa Rais Samia kwani anasema mbali na usikivu wa kiongozi huyo pia Serikali yake imekuwa ikitekeleza inachosema.

"Serikali iliahidi kulipa madeni yote kwa vyombo vya habari ambavyo vilikuwa vinadai wizara,taasisi na mashirika mbalimbali ya umma ambayo yamehakikiwa na yamekwishakulipwa. Sasa hivi tunashuhudia wizara na taasisi na mashirika ya umma yameanza kuleta matangazo na vipindi mbalimbali vya kulipia kwenye vyombo binafsi vya habari, hii ni hatua njema,"anasema.

Askofu Gamanywa

Kwa upande wake Baba Askofu Sylvester Gamanywa ambaye ni Rais wa WAPO Mission International amesema kuwa,kuelekea mwaka mmoja wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan yeye kama mdau muhimu wa Sekta ya Habari na Mawasiliano nchini anakiri wazi kuwa, Mheshimiwa Rais Samia ameonesha njia na anaendelea kuonesha njia katika sekta hiyo.

"Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameonesha umahiri mkubwa katika uongozi wake na kumudu changamoto zilizokuwepo ambazo yeye sio mwasisi wake, hiki si kitu kidogo,"amesema.

Amesema kuwa, Rais Samia katika utendaji wake wa kazi amekuwa akielekeza na kuagiza maeneo yote ambayo yalikuwa na mgongano na mitazamo hasi ndani na nje yasuluhishwe mara moja.

"Na sisi viongozi wa taasisi mbalimbali tumekuwa mashahidi, utekelezaji unafanyika.Sisi WAPO International tunahakikisha pia tunasimamia maadili ya nchi, hivyo tunaangalia pale maadili yanapovunjwa katika ngazi ya familia, jamii na nchi. Basi sisi tunaelimisha Watanzania njia iliyo bora na inayofaa,"anafafanua Baba Askofu Gamanywa.

Diaspora wanasemaje?

Naye Mwanadiaspora kutoka Marekani, Bw. Mubelwa Bandio anasema kuwa, kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia kuna mambo mengi ya kujivunia kupitia Sekta ya Habari na Mawasiliano.

Anasema, miongoni mwa mambo hayo ni uendeshaji wa vyombo vya habari umebadilika sana. "Hili tunaliona hata nyumbani unaona kuna baadhi ya magazeti, lakini kuna magazeti yanajiendesha kidigitali, kwa hiyo kuwa na uwezo wa kufanya hivyo ni hatua ambayo tayari sisi tumeanza kupiga na nchi nyingine zimepiga katika kujikuza na kujisimamisha kimaudhui,kiuchumi na mengineyo,"anasema.

Bw.Bandio anatumia jukwaa hilo kuwamegea mbinu wadau wa Sekta ya Habari na Mawasiliano ili kuifanya sekta hiyo kustawi kwa kasi kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.

"Jambo ambalo sijaliona sana Tanzania, lakini naliona nchi za wenzetu ambalo linasaidia sana katika uchumi na matumizi ya chombo cha habari na wakati huo huo ni zile nguzo tatu ambazo ni kuelimisha,kuburudisha na kufundisha na kushirikisha kutoka sehemu zote za nchi na vyombo vya habari havilazimiki kumiliki mwandishi wa habari kila sehemu na hivyo kukosekana baadhi ya habari katika eneo husika hasa hasa vijijini,"anasema.

Mwanadiaspora huyo anafafanua kuwa, vyombo vya habari vikijiwekea mikakati ya kuwa na wawakilishi wao katika maeneo mbalimbali hususani vijijini watasaidia kuwa na maudhui nyingi za uhakika na haraka kadri zinavyojiri huko, hivyo kuvijengea heshima na kustawi kwa haraka.

Pia anatumia nafasi hiyo kushauri kuwa, habari za kimaeneo na kitaasisi,kurugenzi za mawasiliano hazitakiwi kutoka njia ya taarifa kwa umma.

"Kwa sababu viongozi wetu kama Rais, mawaziri wanafanya kazi kubwa. Siamini kama kazi anayofanya kwa siku nzima inaweza kutosha kwenye press release (taarifa kwa umma) moja. Vile vitengo vilibidi viwe media houses (vyombo vya habari) kamili, kwamba tovuti ya wizara fulani taarifa zote za picha, video na maandishi vinaweza kupatikana huko,"anashauri Bw.Bandio.

Balozi Dkt.Bana

Wakati huo huo, Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Mheshimiwa Dkt.Benson Bana anasema kuwa, kuelekea mwaka mmoja wa Rais Samia kupitia sekta ya habari na mawasiliano kuna mafanikio mengi.

"Teknolojia ya Habari na Mawasiliano imetusaidia sana katika upande wa diplomasia kwa kupeleka ujumbe kwa wale tunaowakusudia. Rais wetu kwa kuanza kufungua nchi imebadilisha mitazamo ya watu wengi sana na mataifa mbalimbali jinsi walivyokuwa wanatuchukulia.

"Na hii imetusaidia kuanza kupokea misaada mbalimbali kwa washirika wetu ikiwemo IMF na mashirika mengine,"anasema Balozi Dkt.Bana.

Anafafanua kuwa, kupitia mfumo huo unaotumika kuwasilisha ujumbe chanya umewezesha diplomasia ya Tanzania na nchi nyingine kuimarika siku baada ya siku.

"Diplomasia yetu na nchi nyingine imezidi kuimarika sana hasa katika kipindi cha Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwani kama Mwanadiplomasia namba moja ameweka mkazo wa kutosha kuhakikisha Balozi za Tanzania zinatekeleza kwa vitendo mkakati wa kidiplomasia.

"Ukiangalia katika hotuba za Mheshimiwa Rais samia katika vikao mbalimbali vya ndani na nje ya Tanzania hasa hotuba yake ya Umoja wa Mataifa inaonesha msimamo wa nchi yetu katika masuala ya kidunia,"anafafanua Balozi Dkt.Bana.

TEF

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw.Deodatus Balile mbali na mambo mengine anatumia mjadala huo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuvipa vyombo vya habari nchini thamani.

"Tunamshukuru Rais wetu (Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) kwa kuagiza vyombo vya habari bianfsi na vya Serikali kupata matangazo kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi.

"Kwani, baadhi ya vyombo vya habari vilikuwa vimeshaanza kufa kwa kukosa fedha za matangazo. Pia tunamshukuru Waziri Nape Nauye kwa kuagiza kuundwa kwa kamati ya pamoja ya wataalam wa intaneti na wadau wa vyombo vya habari ili kufanya mchakato wa kurekebisha baadhi ya kanuni na sera katika sekta hii,"anasema Bw.Balile.

Bw.Balile anabainisha kuwa,kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia, huru wa kujieleza na haki ya kupata habari na mawazo umeongezeka kwa kiwango kikubwa nchini.

DSTV

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa DSTV, Bi.Jacqueline Woiso anasema kuwa, kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia kuna mambo makubwa yamefanyika katika Sekta ya Habari na Mawasiliano nchini.

"Sisi kama 'TV operator' (waendeshaji wa runinga) kitu cha kwanza ambacho tumekiona katika mwaka mmoja wa Rais Samia ni kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya habari.

"Kama mnajua makampuni yamewekeza katika sekta ya habari na ni uwekezaji endelevu, hiyo ni kutokana na usimamizi thabiti wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na taasisi nyingine aliouonyesha.Pia uwekezaji kwenye 'local contents' (maudhui za ndani) umeendelea kuongezeka.

"Si tu hapo, lakini mabadiliko ya kanuni za sasa hivi zinazoruhusu chaneli ziweze kuonekana kwenye mfumo wa satelite, zimeleta upanuzi zaidi, watu waweze kuona bidhaa za viwanda zinazozalishwa Tanzania kwa sababu tuna njia za matangazo ambayo yamefunguka,"anafafanua Bi.Woiso.

Mkurugenzi huyo anasema kuwa, DSTV peke yake inaonekana katika nchi 36 barani Afrika hiyo ikiwa na maana kwamba kitu kinachoonekana kwenye jukwaa hilo kinafika mbali hivyo kupanua fursa nyingi kutoka nchini.

TCRA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),Dkt.Jabir Bakari anasema kuwa, kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia kuna mafanikio makubwa ambayo sekta hiyo imeyapata.

"Sekta ya mawasiliano ndio nguzo kuu ya uchumi huu wa Kidijitali na ndio kiini cha mapinduzi ya nne ya viwanda.Jukumu kubwa la TCRA ni kusimamia sekta ya mawasiliano ikiwemo utoaji wa leseni na kusimamia watoa huduma wote katika sekta ya mawasiliano,"anasema Dkt.Jabir.

Pia Dkt.Bakari amesema kati ya nchi 155 duniani, Tanzania inashika nafasi ya 21 kwa unafuu wa gharama za kununua GB 1 kwa maana ya intaneti huku ikishika nafasi ya sita kwa unafuu zaidi wa gharama ya data kati ya nchi 55 barani Afrika.

"Tanzania ni miongoni wa nchi ambazo gharama za mitandao ni bei ndogo sana mfano ukiangalia tafiti zilizofanywa kwa nchi za Afrika sisi ni nchi ya sita kwa gharama ndogo za intaneti,"anasema Mkurugenzi Mkuu wa TCRA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news