Mwalimu Orenda:Rais Samia anaiheshimisha Sekta ya Elimu nchini

NA ANNETH KAGENDA

SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imemwagiwa sifa zaidi kutokana na namna inavyotoa kipaumbele kikubwa katika sekta ya elimu nchini.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mbondole mkoani Dar es Salaam, Juma Boniface Orenda ameyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi.

"Nikiri kweli akina mama wanaweza, na mfano huu unajidhihirisha kwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan, kwani kwenye upande wa elimu kweli kafanya mambo makubwa sana kiasi kwamba toka enzi hizo haijawahi kutokea, hivyo tuna haki ya kumpongeza sana na akina mama wanaweza,"amesema Mwalimu Juma na kuongeza;

"Lakini pia nimshukuru yeye na Serikali yake kutokana na kwamba mfano Ilala pekee imejengewa madarasa 255 yenye thamani ya sh. Bilioni 5.1,"amesema.
Aidha, alipoulizwa kuhusu shule yake kuonekana ikipata mafanikio makubwa kwenye ufaulu tofauti na awali amesema kuwa hiyo imetokana na mazingira wezeshi yalitotengenezwa na Rais wa Awamu ya Sita.

"Mafanikio haya yanatokana na mazingira wezeshi yaliyotengenezwa na Rais Samia kwa walimu na wanafunzi wa kike, kwani wanafunzi wa kike walikuwa na shida sana ikiwemo kutembea mwendo mrefu, wakati mwingine utoro kutokana na sababu mbalimbali lakini hilo mama aliliona na sasa wanafunzi 120 wa kike wanalala bwenini," amesema Mwalimu Mkuu.

Amesema, bweni hilo wanalolala wasichana lina vitanda 60 na limejengwa kwa thamani ya sh. Milioni 300 huku wasichana hao wakiwa na matroni, wanalishwa na Serikali na kupata matibabu bure.
"Lakini haikuishia hapo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji ametujengea madarasa manne kwa fedha za ndani yenye thamani ya sh. Milioni 60 hivyo kufanya watoto kukaa vizuri," amesema Mwalimu Juma.

Amesema pia Shule ya Sekondari Mbondole imekuwa na ushirikiano mzuri na viongozi wa dini zote mbili kwani wamekuwa wakipata huduma ya maji bure kutoka msikiti uliopo jirani na shule chini ya Sheikh Masoud J Natosa.
"Lakini pia kwa upande wa Kanisa la TAG Mbondole chini ya Mchungaji Nestory A Gotha wametufanyia wayaringi kwenye vyumba viwili vya madarasa kongwe yaliyojengwa toka mwaka 2007,"amesema.

Post a Comment

0 Comments