NMB yazipiga tafu ya madawati shule mkoani Mara

NA FRESHA KINASA

BENKI ya NMB imekabidhi msaada wa madawati 100 yenye thamani ya Shilingi Milioni 10 katika Shule ya Msingi Nkende iliyopo kKta ya Nkende na Shule ya Msingi Soroneta iliyopo Kata ya Nyarero katika Wilaya ya Tarime mkoani Mara kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha sekta ya elimu.

Madawati hayo yamekabidhiwa leo Februari 17, 2022 na Benki ya NMB kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime katika shule ya Msingi Nkende na Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa ambapo shule ya Msingi Nkende imepata mgao wa madawati 50 na Shule ya Soroneta madawati 50.
Akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo, Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Baraka Ladislaus amesema kuwa, benki hiyo imetoa msaada huo kama sehemu ya mwendelezo wake wa kurudisha faida kwa wananchi ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya elimu.

Amesema kuwa, benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na serikali ikiwemo utoaji wa elimu bure kuanzia mwaka 2015 hadi sasa. 
 
Hivyo itaendelea kuwa mdau mkubwa nchini katika kusaidia sekta ya afya na elimu na zaidi ya Shilingi Bilioni 2.8 kati ya Bilioni 289 ambazo ni faida walizopata zitarudishwa kama faida kusaidia huduma za jamii katika sekta ya elimu na afya.
"Tunatambua elimu ni nguzo kuu katika maendeleo ya Taifa letu, NMB hatuwezi kuiachia Serikali ifanye mambo yote na ndio maana tumeendelea kugusa sekta ya elimu na afya kwa kurudisha faida kwa wananchi ambao ni wateja wetu. 
 
"Ttutaendelea kufanya hivyo ambapo kwa sasa tumeanza utaratibu wa kutoa ufadhili kwa watoto wanaohitimu kidato cha nne na kufaulu wanaoishi mazingira magumu tunawaendeleza na pia wanaoenda vyuo vikuu wakitokea mazingira magumu tunawawezesha pia kufikia malengo yao,"amesema Baraka.
Akipokea msaada wa madawati hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Marwa ameishukuru NMB kwa msaada huo, ambapo amesema utasaidia kwa kiwango kikubwa kutatua changamoto ya uhaba wa madawati kwa wanafunzi ambao walikuwa wakikaa chini na kusaidia kusoma katika mazingira mazuri.

Kaimu Afisa elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini, Tumaini Musoma amesema kuwa, madawati hayo yataongeza hamasa kwa wanafunzi kusoma kwa bidii pamoja na kuwezesha mahudhurio kuimarika tofauti na awali.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Soroneta, Ester Nyeriga amesema kuwa, shule hiyo ina wanafunzi 790, walimu 9. Huku upungufu wa madawati shuleni hapo akisema ni 43 hivyo ameomba wadau mbalimbali kusaidia kuwezesha kumaliza tatatizo hilo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nkende, Juma Steven amesema shule hiyo ina wanafunzi 2,100, walimu 36, ambapo madawati yanayohitajika ni 593, yaliyopo ni 406 kwa sasa.

Ester Paul ni Mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya Msingi Nkende ambapo amesema kuwa, madawati hayo yatawawezesha kuondokana na kukaa chini wakati wa masomo.

Post a Comment

0 Comments