Prof.Kahyarara:Kupanga bei ni kosa la jinai, Serikali inafuatilia na itachukua hatua

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Prof. Godius Kahyarara amefafanua kuwa licha ya Serikali kutopanga bei, hata wafanyabiashara hawaruhusiwi kupanga bei na nguvu ya soko inayozingatia uhalisia wa gharama za uzalishaji, usambazaji na kiasi cha faida ndio mfumo wa upatikanaji bei na si genge la wafanyabiashara au wasambazaji kupanga bei.

Hayo yameelezwa kupitia taarifa iliyotolewa leo Februari 15, 2022 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara, Bi.Suzan C. Mshakangoto.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Prof. Kahyarara ameeleza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kwa mujibu wa sheria zinazosimamiwa na Serikali katika kulinda maslahi ya wadau wa soko.

Ameeleza kuwa, Sheria ya Ushindani ndiyo sheria mama inayotumika kudhibiti vitendo vya namna hiyo.

"Kifungu cha 9 (1) cha Sheria ya Ushindani Na. 8 ya 2003 (Fair Competition Act, No. 8
of 2003) kinazuia makubaliano ambayo malengo, matokeo au matokeo tarajiwa yake ni washindani (a) kupanga bei (b) kufanya mgomo (c) kukubaliana katika manunuzi, na (d) kuzuia uzalishaji.

"Aidha, kutokana na Kifungu hicho, Sheria zingine zote za mambo ya udhibiti katika soko zimerejea Sheria ya Ushindani kushughulikia mambo ya ushindani nchini. Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Petroli, Na. 21 ya Mwaka 2015, Sheria ya “EWURA” Sura ya 414 –Sheria ya TCRA, Na. 12 ya 2003 – Kifungu cha 19 na Sheria ya TCAA, Sura ya 80.

"Sheria zote hizi zimeweka vifungu ambavyo vinaelekeza kuwa ukiukwaji wa mambo yote yahusuyo ushindani yanapaswa kushughulikiwa kwa kufuata Sheria ya Ushindani, Na. 8 ya 2003,"amesema Prof. Kahyarara kupitia taarifa hiyo.

Prof. Kahyarara pia amesema mara baada ya mwaka mpya kulitokea uhaba wa vinywaji baridi na sababu mbalimbali zilitolewa ikiwemo ukosefu wa sukari ya viwandani kwa sababu ya kupungua kwa makontena ya kubeba mizigo kwa wamiliki wa meli.

"Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na Wizara ulibaini kuwa sababu hizo hazikuwa na ukweli, kwani licha ya makontena kuadimika bado mizigo ilikuwa inasafirishwa nje ya makontena na kwa kipindi hicho, Wizara ilibaini kuwa tani 25,000 za sukari ya viwandani ziliingia nchini.

"Wazalishaji wa vinywaji baridi walionesha kuwa changamoto ilikuwa ni kwa wasambazaji na si ya uzalishaji. Bidhaa nyingine ambazo bei yake imekuwa juu kuliko uhalisia ni za vifaa vya ujenzi ambapo baadhi ya maeneo ilifikia mfuko mmoja wa saruji kuuzwa kwa shilingi 25,000.

"Mafuta ya kula ya alizeti yanauzwa mpaka shilingi 196,000 kwa ndoo ya lita ishirini na sukari ni kati ya shilingi 2,800 hadi 3,000,"ameongeza.

Prof. Kahyarara amemaliza kwa kusema kuwa bei hizo ziko juu ya wastani wa bei zinazotozwa katika nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika na hazitafumbiwa macho.

Amesisitiza kuwa, wizara haitamuonea mtu wala kumnyamazia yeyote atakayebainika kutoza bei ambazo hazina uhalisia na akatoa wito kuwa licha ya Serikali kuwa tayari kulinda viwanda vya ndani pia ina jukumu la kulinda maslahi ya walaji hasa wa kipato cha chini, hivyo ameahidi kushirikiana na wadau wote katika biashara hususan suala la usimamizi wa soko.

Post a Comment

0 Comments