Rais Dkt.Mwinyi ataja umuhimu wa kuanzishwa kituo cha utatuzi wa migogoro ya kibiashara

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema wakati umefika kwa Zanzibar kuanzisha kituo kwa ajili ya utatuzi wa migogoro ya kibiashara (arbitration center) ili kwenda sambamba na hatua ya Serikali ya kuvutia wawekezaji katika miradi mikubwa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akiwa na viongozi wengine wakisimama wakati Wimbo wa Taifa ukipigwa katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar yaliyofanyika leo Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu).

Dkt. Mwinyi amesema hayo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria Zanzibar, hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil, Kikwajuni Jijini Zanzibar.

Amesema, wakati Zanzibar ikivutia Wawekezaji kwa ajili ya kuanzisha miradi mikubwa, haitokuwa busara kwa migogoro inayojitokeza kusikilizwa katika mahakama za kawaida au kwenye vituo vilioko nje ya nchi, hivyo akashauri kuanza kutungwa sheria juu ya jambo hilo.
Amwsema, ni vyema kuwepo sheria na mifumo ya utoaji haki itakayoweza kuvutia wawekezaji na kuweka vitega uchumi vyao hapa nchini na kutoa ajira kwa wananchi.

Aidha, aliitaka Mahakama kujenga mifumo itakayohakikisha kunakuwepo usikilizaji wa haraka wa mashauri Mahakamani pamoja na taasisi nyingine za utoaji wa haki.

Amesema, sio jambo linalopendeza kwa wananchi na Wawekezaji kuchukua muda mrefu Mahakamani pamoja na kwenye taasisi nyengine za utoaji wa haki.
Dkt. Mwinyi alieleza kuwa kumekuwepo malalamiko mengi yanayowasilishwa kwake kupitia Mtandao wa Sema na Rais, kuhusu ucheleweshaji wa utoaji haki unaofanywa na baadhi ya viongozi wa taasisi za Serikali, hivyo akatumia fursa hiyo kuwahimiza viongozi kuongeza bidii katika usimamizi wa haki za wananchi kwa kuzingatia sheria.

Aidha, akatoa wito wa kupiga vita vitendo vya rushwa na vitendo vyote vya kifisadi.

Rais Dkt. Mwinyi alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuimarisha mazingira ya utoaji wa haki, ikiwemo kufanikisha ujenzi wa majengo ya kisasa ya taasisi hizo na kuzipatia nyenzo kwa kadri hali ya fedha na uchumi inavyoruhusu.
Sambamba na hayo, alitumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Zanzibar pamoja na taasisi zote za utoaji haki nchini na kubainisha maeneo mbalimbali ya ushirikiano; ikiwemo matumizi ya lugha ya Kiswahili, mifumo ya TEHAMA, mafunzo kwa watumishi na namna bora ya kupambana na dawa za kulevya pamoja na usuluhishi wa migogoro.

Dkt. Mwinyi amempongeza Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Rmadhan Abdalla kwa kuleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika kipindi kifupi, na hivyo akawataka watendaji na watumishi wa mhimili huo kuunga mkono juhudi hizo.

Mapema, Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla alisema kauli mbiu ya maadhimisho hayo isemayo "Usimamizi wa haki ni msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii”, imezingatia hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kujenga Uchumi wa Buluu, na kusema unaendana na umuhimu uliopo katika usimamizi wa haki.
Alisema pamoja na mafanikio yaliokwisha kupatikana katika utekelezaji wa dhana hiyo bado kumekuwa na mwamko mdogo kwa wafanyabiashara wa Zanzibar kufungua kesi katika Mahakama ya Biashara.

Alisema, katika mwaka 2021 kulikuwa na jumla ya mashauri 11 pekee yalioripotiwa Mahakamani, hivyo akatoa ahadi ya kuendelea kuitangaza Mahakama hiyo kwa jamii ili itumike kikamilifu.

Alieleza miongoni mwa mafanikio yaliopatikana katika usimamizi wa haki ni kuwepo kwa mahakimu sita wanaosikiliza kesi za Udhalilishaji na Mahakimu watatu wa kusikiliza kesi za dawa za kulevya.

Alisema kwa mujibu wa utaratibu Mahakimu hao hawapangiwi kesi za aina nyingine, huku muda wa kusikiliza kesi ukiongezwa hadi saa 11, ikiwa ni hatua ya kumaliza mashauri hayo kwa haraka na kutoa fursa kwa wnanachi kufanya kazi nyingine.
"Nimewaagiza Mahakimu kupanga mashauri kwa muda, ikiwa ni hatua ya kuwasaidia wananchi wasipoteze muda mwingi mahakamani,"amesema.

Kuhusiana na ongezeko la mahabusu katika Magereza Kisiwani Pemba, Kaimu Jaji Mkuu alisema amewaagiza Mahakimu kutoa dhamana kwa mahabusu wa kesi zote zenye dhamana pamoja na kuongeza nguvu ya usikilizaji kwa kesi ambazo hazina dhamana, huku Mahakama ikizingatia mfumo wa kutekeleza adhabu katika jamii.

Jaji Khamis alitoa wito kwa jamii kuondokana na tabia iliyojitokeza ya kuwepo ushirikiano kwa lengo la kuharibu kesi, hususan za udhalilishaji kwa wadhuriwa (victims) wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi miaka 17.

Nae, Waziri wa Wizara Nchi (OR) Katiba, Sheria , Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman alisema kuna mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika shughuli za kimahakama na kubainisha kuwepo kwa mashirikiano makubwa kwa watendaji wa usimamizi wa haki, ikiwemo Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Jeshi la Polisi, Mahakama pamoja na Mawakili.

Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dkt. Mwinyi Talib Haji alisisitiza umuhimu wa dhana ya uchumi wa buluu kuzungumzwa mara kwa mara.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Mashtaka Salma Ali Khamis alisema changamoto kubwa inayokwaza utekelezaji wa usimamizi wa haki ni ile ya wananchi kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi, hususan katika kesi za udhalilishaji, hivyo akabinisha umuhimu wa kuwepo mabadiliko ya kiutendaji na kisera.

Sambambana hilo Mkurugenzi huyo alisema kumeanza kuonyesha dalili katika jamii ya kushirikiana katika kesi za udhalilishaji kwa lengo la kukomoana na kutumika kama kitega uchumi cha watu kujipatia kipato.

Vile vile, Rais wa Chama cha Mawakili Zanzibar, Dkt. Slim Abdalla aliishauri Serikali kuweka mkazo katika utatuzi wa migogoro ya kiuchumi, kifedha pamoja na kibiashara.

Alisema kuna umuhimu wa Zanzibar kuanzisha kituo cha utatuzi wa migogoro ya kibiiashara na kutoa mifano ya nchi mbali mbali Duniani zilizofanya hivyo, ikiwa ni hatua ya kuvutia Wawekezaji wakubwa.

Siku ya Sheria Zanzibar huadhimishwa kila ifikapo Februari 2, ya kila mwaka, ikiashiria kuanza kwa mwaka mpya wa Mahakama. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news