Rais Dkt.Mwinyi atoa maagizo kwa watendaji serikalini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka watendaji wa Serikali kuwa wabunifu na kuja na njia mbadala ya kutafuta fedha nje ya Bajeti ya Serikali, ili kufanikisha utekelezaji wa mipango ya Serikali.

Mheshimiwa Dkt. Mwinyi amesema hayo leo Februari 4, 2022 katika Ufunguzi wa Mafunzo ya Upangaji wa Vipaumbele, yalioandaliwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Tony Blair pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), yanayofanyika Chuo cha Utalii Maruhubi jijini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi alipokuwa akitoa hotuba yake wakati akiyafungua mafunzo ya Upangaji wa Vipaumbele na Uandaaji wa Mipango ya maendeleo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Tony Blair pamoja na Shirika la Maendeleo la UNDP katika Ukumbi wa Chuo cha Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Kampasi ya Maruhubi, kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria Utumishi na Utawala Bora, Mhe.Haroun Ali Suleiman na Katibu wa Baraza la Mapinduzi pia Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said (katikati). (Picha na Ikulu).

Amesema, Serikali imekuwa ikishindwa kutekeleza vyema mipango yake ya maendeleo kutokana na watendaji wa taasisi kutokuwa na utamaduni wa kutayarisha maandiko ya miradi (project write-ups), hata kwa miradi ambayo Mashirikia ya Kimataifa hutoa misaada kwa nchi mbalimbali na hivyo kubaki zikiwa tegemezi.

Mheshimiwa Rais amesema, katika kipindi hiki ambapo makusanyo ya Serikali yameshuka kwa kiasi kikubwa kutokana na athari za maradhi ya UVIKO -19, viongozi wa taasisi wamekuwa wakilalamika kwa kutokuingiziwa fedha na Serikali, bila wao kuja na mbinu nyingine ya kuzitafuta. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi (katikati) akisalimiana na viongozi mara baada ya kuwasili katika Chuo cha Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Kampasi ya Maruhubi leo kufungua Mafunzo ya Upangaji wa Vipaumbele na uaandaaji wa Mipango ya maendeleo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Tony Blair pamoja na Shirika la Maendeleo la UNDP.
Dkt.Mwinyi amesema bado hajaridhishwa na utekelezaji wa mipango ya Serikali na kubainisha kuwa mipango inahitaji uharaka wa utekelezaji, maamuzi ya haraka pamoja na ufuatiliaji.

Ameeleza kuwa, taratibu za kiutendaji zimeghubikwa na urasimu na kusema kuwepo kwa utamaduni wa kuoneana muhali pamoja na baadhi ya sheria ziliopo kuwa za amani na kutokidhi mahitaji ya wakati. 

Rais Dkt.Mwinyi amesema, kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa mipango ya Serikali kumemfanya aone umhimu wa kuwepo kitengo maalum ndani ya serikali kitakachoshughulikia ufuatiliaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo inayowekwa (Delivery Unit).Watendaji na Maafisa mbali mbali katika Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakiwa katika ufunguzi wa mafunzo ya Upangaji wa Vipaumbele na uaandaaji wa Mipango ya maendeleo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Tony Blair pamoja na Shirika la Maendeleo la UNDP katika Ukumbi wa Chuo cha Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Kampasi ya Maruhubi mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi. 
Watendaji katika Wizara mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakiwa katika ufunguzi wa mafunzo ya Upangaji wa Vipaumbele na uaandaaji wa Mipango ya maendeleo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Tony Blair pamoja na Shirika la Maendeleo la UNDP katika Ukumbi wa Chuo cha Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Kampasi ya Maruhubi leo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi. 

“Kasi ya kufuatilia na kutekeleza mambo yanayopangwa na Serikali na kutolewa maagizo ni ndogo sana katika ngazi zote,”amesema. 

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema, mafunzo hayo ni muhimu sana kwa viongozi hao, ikizingatiwa kuwepo kwa mahitaji mengi ya wananchi, wakati ambapo rasilimali ziliopo ni chache.

“Lazima tuwe na mbinu na mikakati imara ya kupanga na kuchagua pamoja, kipi kianze na kipi kifuate kwa kuzingatia rasilimali zitakazokuwepo,”amesema. 

Amesema, utekelezaji wa mipango hiyo inahitaji mbinu imara ya kutoa vipaumbele kwa mujibu wa upatikanaji wa rasilimali na nyenzo ziliopo na kubainisha hatua iliofanywa na viongozi wa Taasisi ya Tony Blair ya kuipitia mipango hiyo, kuwa ina umuhimu mkubwa.
Wawakilishi wa Taasisi ya Tony Blair wakiwa katika ufunguzi wa mafunzo ya Upangaji wa Vipaumbele na uaandaaji wa Mipango ya maendeleo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Tony Blair pamoja na Shirika la Maendeleo la UNDP katika Ukumbi wa Chuo cha Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Kampasi ya Maruhubi mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi. 

Pia amesema mipango ya Maendeleo imeelezwa vyema katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, Mpango wa Maendeleo ya Zanzibar 2021-2026, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2050, ahadi za Viongozi wakuu pamoja na Mipango ya Maendeleo ya kimataifa. 

Ametoa shukurani kwa Taasisi ya Tony Blair na Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) kuiwezesha Serikali kuandaa mafunzo hayo muhimu na kuytoa rai kwa washiriki kutumia vyema taaluma waliyoipata kwa kupanga vizuri mipango ya maendeleo na kuwa na njia bora ya kuitekeleza. 

Nae, Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Cristine Musisi amewataka washiriki wa mafunzo hayo kubadilika kifikra na kuamini kuwa Dira ya Serikali ya 2050 na mipango ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati. 

Aidha, Mwakilishi wa Taasisi ya Tony Blair Ronald Osubi, pamoja na mambo mengine alibainisha mihimili minne ya mipango ya kipaumbele itakayotekelezwa, kuwa ni pamoja na mabadiliko ya kiuchumi, uendelezaji wa rasilimali watu, miundo mbinu endelevu pamoja na Utawala Bora.

Mapema, Waziri wa Nchi (OR) Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa makini na wasikivu, akibainisha umuhimu wao kwa mustakabli wa maendeleo ya Zanzibar. 

Aidha, Katibu Mkuu Wizara ya Nchi (OR) Fedha na Mipango, Dkt.Malik Akil amesema mafunzo hayo yanalenga kutayaratisha vipambele, ikiwa ni matunda ya Serikali kwa kazi iiofanyika kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa. 

Mafunzo hayo ya siku nne yamewashirikisha watendaji mbalimbali wa Serikali, wakiwemo Makatibu Wakuu wa Wizara, Maofisa wadhamini, wakuu wa Taasisi na Mashirika ya umma.

Post a Comment

0 Comments