Rais Samia amlilia Dkt.Mwele Ntuli Malecela

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameelezea kupokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyopewa Kipaumbele katika Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), Dkt.Mwele Ntuli Malecela.

"Nimesikitishwa sana na kifo cha Dkt.Mwele Ntuli Malecela, mwana wa Afrika ambaye ameitumikia vyema Tanzania ndani na nje ya mipaka. Pole zangu zimfikie Mzee John Malecela na familia yake yote wakati huu wa majonzi mazito. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, Amin,"ameeleza Rais Samia.

Dkt.Mwele ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu mstaafu,Mheshimiwa John Malecela, aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kabla ya kuvuliwa wadhifa huo na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli mwezi Desemba 17, 2016.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika familia ya Mzee Malecela na WHO,Dkt.Mwele Ntuli Malecela amefariki dunia Februari 10, 2022 mjini Geneva, Uswisi wakati akipatiwa matibabu.

Aidha,kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyopewa Kipaumbele wa WHO, Dkt. Mwele alikuwa Mkurugenzi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Espen), wa Shirika la Afya Duniani (WHO) katika Kanda ya Afrika.

Post a Comment

0 Comments