Rais Samia kufungua Chuo cha Uongozi cha Julius Nyerere mjini Kibaha

NA ROTARY HAULE

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Chuo cha Uongozi cha Julius Nyerere mjini Kibaha mkoani Pwani.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewaambia waandishi wa habari ofisini kwake kuwa, Rais Samia atafungua chuo hicho Februari 23,  mwaka huu siku ya Jumatano.

Kunenge amesema, katika uzinduzi huo Rais Samia ataambatana na Makatibu wakuu wa vyama vyote ambavyo vilikuwa vinashirikiana katika harakati za masuala ya ukombozi wa kupigania uhuru.

Amesema,kabla ya Rais kuzindua chuo hicho kutatanguliwa na ufunguzi wa barabara ya lami ya kilomita mbili kutoka kwa Mfipa mpaka chuoni hapo, barabara ambayo ilijengwa mahususi kwa ajili ya kufika chuoni hapo.
Kunenge amesema, barabara hiyo itazinduliwa Februari 22,mwaka huu na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo kwa kushirikiana na Makatibu wakuu wa vyama shiriki vya chuo hicho kutoka nchi mbalimbali .

Amesema,Makatibu wa vyama hivyo vya siasa wanatoka katika Chama cha SWAPO (Namibia),FRELIMO (Msumbiji), ZANU PF( Zambia),MPLA (Zimbambwe),ANC (Afrika Kusini).

"Mkoa wa Pwani tumepata heshima kubwa ya ujio wa Rais Samia kwa ajili ya kufungua Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere Kibaha, kwa hiyo ni fursa pia kwa wananchi wetu kujitokeza kushiriki siku hiyo,"amesema Kunenge.
Kunenge amesema kuwa, CCM ndio chama kilichounda Serikali na Rais Samia ndio mwenyekiti wa CCM na kwamba ufunguzi wa chuo hicho utakwenda kufungua fursa ya uchumi kwa wananchi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.

"Ufunguzi wa chuo hiki kutahudhuriwa na Makatibu wakuu mbalimbali wa vyama vya siasa kutoka nchi shiriki hivyo niwatoe wasiwasi kuwa mkoa upo salama na tunajipanga zaidi kuimarisha usalama ili wageni wetu waishi kwa amani ndani ya mkoa wetu ,"ameongeza Kunenge.

Kunenge ametoa rai kwa wakazi wa Mkoa wa Pwani kujitokeza kwa wingi katika kumlaki Rais Samia pamoja na wageni wengine watakaokuja Pwani kwa ajili ya ufunguzi huo.

Post a Comment

0 Comments