Serikali yatoa msisitizo kuhusu ujenzi wa barabara za vijijini na mijini kupitia TARURA

NA MWANDISHI MAALUM, OR-TAMISEMI

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kasism Majaliwa Majaliwa amesema hakuna barabara ya vijijini wala mjini itakayokwama kujengwa kwa kukosa fedha kwa sababu Serikali imeelekeza fedha nyingi kwa ajili ya uboreshaji wa barabara za ujenzi wa miundombinu hiyo.
Mhe. Majaliwa ameyasema hayo wakati wa kufungua kikao kazi kati ya Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na wakandarasi kilichofanyika jijini Dodoma.

Amesema, Serikali imefanya juhudi katika kuijengea uwezo TARURA ili iweze kutekeleza makujumu yake na kuiongezea fedha kutoka shilingi bilioni 247.5 ilipoanzishwa mwaka 2017 hadi kufikia shilingi bilioni 719.61. 
“Fedha hizi zinajumuisha shilingi bilioni 127.50 kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali, shilingi bilioni 243 kutoka Mfuko wa Barabara, shilingi bilioni 322.15 kutoka katika tozo ya shilingi 100 kwa lita ya mafuta ya petroli na dizeli na shilingi bilioni 30.44 kutoka kwenye ushuru wa maegesho wa magari na hizi zote ni kutoka katika fedha za ndani tu, ambayo ni ongezeko la asilimia 204.3,"amesema Waziri Mkuu.

Mhe. Majaliwa amesema, kwa sasa takribani shilingi trilioni moja zimeelekezwa kwenye barabara za mijini na vijijini kutoka Serikali kuu, OR-TAMISEMI, Mfuko wa Barabara, tozo ya mafuta, maegesho ya magari na fedha zinazotolewa kwenye miradi inayotekelezwa na wadau wa maendeleo kama DMDP, Rise, Tactic na Agri business.
“Niwahakikishie wakandarasi wanaopewa kazi na Serikali kuwa hakuna changamoto ya fedha, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inajitahidi kutafuta fedha, hivyo mkipewa kazi mtalipwa kwa wakati, na hakuna barabara itakwama, ukisaini mkataba kazi lazima ianze.

“Zile kauli za wakandarasi wanazosema ukitaka ufilisike fanyakazi na Serikali hazitakiwi kuwepo kwa sababu fedha zipo na mtalipwa kwa wakati,"amesema.
Aidha, Mhe. Majaliwa alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakandarasi wa ndani kuungana ili waweze kupewa kazi kubwa na kuwa hali ya sasa ya kila mkandarasa kufanya kazi kivyake inawanyima fursa na kusisitiza kuwa haipendezi kazi kubwa zikatolewa kwa wakandarasai wa nje ambapo wa ndani wangeungana wangeweza kufanya kazi hiyo.

Kwa upande wake,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa amesema Serikali ina matumaini makubwa kupitia watendaji hao na kwamba changamoto zote zinazowakabili hazina budi kufanyiwa kazi kwa wakati ili waweze kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Amesema, wahakikishe kila mmoja anatekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa weledi na kwa viwango vinavyotakiwa ili barabara wazazosimamia zinapitika kwa wakati wote. “Hayo ndio maono ya Mheshimiwa Rais Samia.”

Waziri Bashungwa ameagiza asilimia 60 ya kazi za TARURA zitangazwe mapema, bila kusubiri mpaka mwaka wa fedha uanze ili pale mwaka wa fedha unapoanza iwe ni wakandarasi kuanza kazi.

Naye Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni pamoja na baadhi ya makandarasi kuomba kazi nyingi na wakati mwingine kupata kazi nyingi kuliko uwezo wao, hivyo hulazimika kusubiri hadi kazi iishe eneo fulani ndipo wapeleke vifaa na kuanza kazi eneo jingine.

Post a Comment

0 Comments