Tanzania na China kuimarisha uhusiano katika michezo,sanaa na utamaduni

NA JOHN MAPEPELE

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa amesema Serikali ya Tanzania inakwenda kufufua mpango wa miaka mitatu wa maendeleo ya sekta za utamaduni, sanaa na michezo ulioingiwa na Serikali ya China.
Akizungumza Februari 4, 2022 jijini Dar es Salaam na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian katika kikao maalum kwenye sherehe za uzinduzi wa michezo ya msimu wa baridi ya Olympic 2022 amesema tayari wizara yake imeandaa andiko kwa ajili ya mpango huo litakalowasilishwa hivi karibuni.

Katika kikao hicho, Mheshimiwa Waziri aliambatana na Katibu Mkuu wake, Dkt. Hassan Abbasi.

"Tunatarajia kuwasilisha mpango wetu ambao tutaingia makubaliano ili utekelezaji wake uanze mara moja," amefafanua Mhe. Mchengerwa.

Kwa upande wake, Balozi Chen amesema ni wakati mwafaka wa kufufua na kuendeleza sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kuinua uchumi wa nchi zote baada ya kushuka kutokana na ugonjwa wa UVIKO- 19.

Amesema, Serikali yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu kupitia mafunzo mbalimbali.

"Awali watu wetu walikuwa wanapata fursa ya kuja Tanzania na watanzania kwenda China, lakini kutokana UVIKO tulishindwa sasa ugonjwa umepita. Tunajipanga tuinue sekta zetu kwa pamoja," ameongeza Mhe. Balozi Chen.

Amempongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa msimamo wake wa kuendelea kuenzi na kuendeleza uhusiano mzuri uliojengwa na viongozi waasisi wa mataifa haya mawili kwa muda mrefu.

Post a Comment

0 Comments