Tanzania, Qatar kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali, Waziri Prof.Ndalichako afafanua

NA MWANDISHI MAALUM

TANZANIA imekusudia kuendeleza uhusiano uliopo kati yake na nchi ya Qatar, sambamba na kukuza mahusiano ya kibiashara, uchumi na fursa za ajira.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na ugeni kutoka Qatar ukiongozwa na Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Kazi ya Qatar Mhe. Mohamed Hassan al Obaidali Februari 18, 2022 jijini Dar es Salaam. Viongozi hao wamejadili juu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Qatar katika sekta ya Uwekezaji, Biashara na uhusiano wa kimataifa

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako alipokuwa na mazungumzo na ugeni kutoka nchi ya Qatar ambapo kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Mkutano uliopo hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam Februari 18, 2022.
Waziri Ndalichako ameeleza kuwa, Tanzania na nchi ya Qatar zimekuwa na mahusiano mazuri kwa muda mrefu na mataifa hayo yamekuwa yakishirikiana katika mambo mengi ikiwemo Biashara, Uwekezaji na shughuli nyingine nyingi zenye manufaa kwa nchi hizo mbili.

“Nipongeze Nchi ya Qatar kwa kuonyesha dhamira ya dhati katika utekelezaji wa makubaliano tuliyoingia tangu mwaka 2014 ambao umelenga kuimarisha uhusiano wa nchi zetu katika Nyanja mbalimbali zenye maslahi ya pande zote mbili,” alisema Profesa Ndalichako.
Sehemu ya ugeni kutoka nchi ya Qatar wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (hayupo pichani) walipokutana kwa majadiliano katika ukumbi wa Mkutano uliopo hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam Februari 18, 2022.

Aliongeza kuwa, Tangu Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aingie madarakani amekuwa akionyesha dhamira yake ya dhati katika kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na mataifa mengine na pia amekuwa akifungua fursa za uwekezaji nchini, ufanyaji wa biashara sambamba na kuwezesha watanzania kushirikiana na nchi rafiki katika nyanja mbalimbali.
Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Kazi ya Qatar Mhe. Mohamed Hassan al Obaidali akieleza jambo wakati wa kikao hicho cha Majadiliano kilichofanyika katika ukumbi wa Mkutano uliopo hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam Februari 18, 2022.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Jamal Katundu akieleza jambo wakati wa kikao hicho cha Majadiliano kilichofanyika katika ukumbi wa Mkutano uliopo hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam Februari 18, 2022.
Kikao hicho cha Majadiliano kikiendelea katika ukumbi wa Mkutano uliopo hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam Februari 18, 2022.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akiteta jambo na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Nchini, Dkt. Anna Makakala (kulia).

Sambamba na hayo Mheshimiwa Ndalichako alieleza kuwa Serikali imeendelea kuratibu vyema na kuzingatia misingi katika kupeleka watanzania kufanya kazi katika maeneo mbalimbali ya nje nchi.

Pia alieleza kuwa, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikiratibu Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ambayo imekuwa ni chachu ya kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa fani mbalimbali zinazohitajika nchini pamoja na kwenye mataifa mengine.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akikabidhi zawadi Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Kazi ya Qatar Mhe. Mohamed Hassan al Obaidali mara baada ya kuhitimisha kikao hicho cha majadiliano kilichofanyika katika ukumbi wa Mkutano uliopo hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam Februari 18, 2022.(Picha na OWM-KVAWU).

Naye, Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Kazi Qatar, Mhe. Mohamed Hassan al Obaidali ameeleza kuwa kuridhishwa na mazingira yaliyopo nchini na Ukarimu wa Watanzania na kuahidi Serikali ya nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuangalia uwezekano wa kuwekeza kwenye miradi ya kiuchumi itakayoziletea maendeleo nchi hizo mbili.

Post a Comment

0 Comments