TARURA KUANZA UKUSANYAJI USHURU WA MAEGESHO KIELEKTRONIKI MKOANI TANGA

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) utaanza kukusanya malipo ya ushuru wa maegesho kwa kutumia mfumo wa kielektroniki (TERMIS) mkoani Tanga kuanzia Machi Mosi, mwaka huu.

Akifungua semina ya kujengewa uwezo kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama na viongozi wa Mkoa wa Tanga, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mheshimiwa Hashim Mgandilwa amewataka wananchi mkoani humo kupokea mabadiliko hayo na kuhakikisha wanalipa wenyewe ushuru wa maegesho ili kuepuka adhabu na faini zisizo za lazima.
Mh. Mgandilwa ambaye katika semina hiyo alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima, amesema mfumo huo wa ukusanyaji mapato yatokanayo na maegesho ya vyombo vya moto (parking fees) na matumizi ya hifadhi za barabara, malipo yote yatafanyika kwa kutumia kumbukumbu namba ya malipo (control number) na malipo hayo yatapokelewa serikalini moja kwa moja.
Aidha, ametaja faida ya mfumo huo ni kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato ya serikali yatakayosaidia maboresho na maendeleo ya miundombinu ya barabara, utasaidia wateja kufanya maombi na kulipia huduma kwa njia ya mtandao bila kufika ofisi ya TARURA.

Faida nyingine ni kumpa mteja fursa ya kuamua kulipia ushuru wa maegesho kwa namna anayotaka kuanzia saa moja na zaidi, kwa siku, wiki au kwa mwezi.
"Lakini pia mfumo huu wa ukusanyaji ushuru wa vyombo vya moto utatumika kwa vyombo vilivyoegeshwa kwenye maeneo ya maegesho tu ni mfumo rafiki, rahisi na salama, mtumiaji atatumia mtandao wowote wa simu ya mkononi, Benki ya NMB na CRDB au kupitia kwa mawakala," amesema Mheshimiwa Mgandilwa.
Awali, akielezea utekelezaji wa mfumo huo, Mkuu wa Kitengo cha Tehama kutoka TARURA, Ndg. Stanley Mlula amesema makusanyo hayo yatafanyika kwa maegesho yote yaliyopo pembezoni mwa barabara kuu na kuomba wananchi na wadau kuhakikisha wanafanya malipo hayo kwa wakati kwa sababu njia inayotumika ni rahisi hasa ya simu za kiganjani ambapo wengi wanakuwa nayo mahala popote wanapokuwa.

Post a Comment

0 Comments