THRDC yampongeza Waziri Nape kwa kuyafungulia magazeti manne

NA MWANDISHI MAALUM

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) unampongeza Mhe. Nape Moses Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kufungulia magazeti manne yaliyokuwa yamefungiwa na kutoa leseni mpya. 

Pongezi hizo zimetolewa kupitia taarifa iliyotolewa na Afisa Habari wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THDRC) leo Februari, 2022 jijini Dar es Salaam huku ikiyataja magazeti hayo kuwa ni,Mseto,Mawio, MwanaHalisi na Tanzania Daima. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo,Mhe. Nape Nnauye ana rekodi nzuri ya kutetea uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania. 

"Aidha, tunampongeza Waziri kwa ahadi yake na utayari wake wa kushirikiana na wadau wa vyombo vya habari kujadili marekebisho ya Sheria ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016. Mhe. Waziri amefungulia magazeti hayo wakati akihutubia mkutano wa wahariri wa habari ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi na Jukwaa la Wahariri Tanzania,"imeeleza sehemu ya taarifa ya THRDC.

Kufungiwa kwa gazeti la Mseto

Aidha,kwa mujibu wa taarifa hiyo Gazeti la Mseto lilifungiwa tarehe 10 Agosti 2016, wiki moja baada ya kuchapisha habari kuhusu ufisadi wa kiwango cha juu uliomhusisha Naibu Waziri ndani ya serikali ya Tanzania.

Gazeti lilifungiwa kwa mujibu wa sheria ambayo ilimpa mamlaka Waziri wa Habari kufungia uchapishaji na usambazwaji wa gazeti endapo ataona ni kwa "maslahi ya umma, au kulinda amani".

"Hata hivyo, gazeti hili lilipinga uamuzi huo wa kufungiwa kwenye Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki tarehe 7 Oktoba 2016, kwa hoja ya kwamba amri hiyo ilikiuka haki ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari kinyume na kanuni za msingi zilizopo kwenye Ibara ya 6(d), 7(2) na 8(1)(c) ya Mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

"Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki iliamua kwamba uamuzi wa Waziri kufungia gazeti hilo ulikiuka haki ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari na hivyo basi Tanzania ilikiuka Mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

"Mahakama ilisisitiza kwamba Waziri alifungia gazeti hilo pasipo kuzingatia sheria na alilifungia gazeti hilo kwa maoni yake mwenyewe. Hivyo basi Mahakama ilimuamuru Waziri kubatilisha amri hiyo na kuruhusu gazeti hilo kuanza tena kuchapishwa,"imeongeza taarifa hiyo.

Kufungiwa kwa gazeti la Mawio

Gazeti la Mawio lilifungiwa kwa miezi 24 kuanzia tarehe 15 Juni 2017. Lilifungiwa kwa madai ya kuchapisha picha za marais wawili wastaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete katika toleo lake la tarehe 15 - 21 Juni, chapisho hilo liliwahusisha wastaafu hao na sakata la mchanga wa madini tofauti na maagizo ya serikali.

Kwa mujibu wa THRDC Gazeti la Mawio lilipinga kufungiwa kwake kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania. Tarehe 13 Desemba 2018 Jaji Benhajj S. Masoud alitoa uamuzi kwamba agizo la Waziri wa Habari lilikuwa kinyume cha sheria kwasababu hapakuwa na usawa wa kusikilizwa kabla ya kufungiwa gazeti hilo.

Kufungiwa kwa gazeti la MwanaHalisi

THDRC imeeleza kuwa, Gazeti la MwanaHalisi lilifungiwa kwa miaka miwili, kuanzia tarehe 19 Septemba 2017, kwa tuhuma za kuchapisha taarifa zisizo na maadili na zenye kuhatarisha usalama wa nchi, taarifa iliyochapishwa na gazeti hilo ilikuwa na kichwa Habari kwamba, 'Watanzania wamuombee nani, Rais au Tundu Lissu? ambaye ni Mwanasheria na Mwanasiasa wa upinzani ambaye alipigwa risasi mara kadhaa na watu wasiojulikana tumboni na miguuni tarehe 7 Septemba 2017.

Kufutwa kwa leseni ya gazeti la Tanzania Daima

Kwa mujibu wa mtandao huo, leseni ya gazeti la Tanzania Daima ilifutwa tarehe 23 Juni 2020. Leseni yake ilifutwa kwa madai ya kukiuka sheria mbalimbali za nchi na kufanya kazi kinyume na maadili ya uandishi wa habari. 

"Hata hivyo, sheria ambazo zilidaiwa kuvunjwa hazikuwekwa wazi. Leseni ilifutwa kwa mujibu wa Kifungu cha 6 (b) cha Sheria ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 ambacho kinatoa mamlaka kwa mkurugenzi wa habari kufuta leseni endapo mwenye leseni ameshindwa kuzingatia sheria na masharti ya leseni.

"Mtandao umefurahishwa na juhudi au jitihada za Wizara. Kufunguliwa kwa magazeti hayo ni kuimarisha upatikanaji wa habari na uhuru wa kujieleza. Pia ni dalili inayoonyesha kuheshimu haki ya uhuru wa kujieleza, upatikanaji wa habari kama inavyotakiwa kwenye ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria za kikanda na kimataifa,"imeeleza taarifa ya mtandao huo.

Ndugu Saed Ahmed Kubenea, Mkurugenzi mtendaji wa magazeti ya Mawio na Mseto akitoa salamu za shukrani kwa waziri, ameiomba serikali kuangalia namna ya kutoa ruzuku kwa vyombo vya habari binafsi kwa sababu hali ya kiuchumi kwa vyombo binafsi vya habari ni mbaya sana, magazeti yaliyofunguliwa yanaweza yasionekane mtaani maana yapo yaliyojifunga yenyewe kwa sababu za kiuchumi.

Marekebisho ya Sheria

Kwa mujibu wa THRDC, ikumbukwe kwamba vifungu kumi na sita vya Sheria ya Vyombo vya Habari viliamriwa kuwa vipo kinyume na Mkataba wa Kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kesi namba 02 ya mwaka 2017 iliyofunguliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Baraza la Habari Tanzania, pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu. 

"Uamuzi huo ulitolewa mnamo Machi 28, 2019 katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki. Vifungu hivyo vinatoa mamlaka makubwa kwa Waziri ikiwemo kufungia vyombo vya habari. Vifungu hivyo ni 7 (3) (a), (b), (c), (f), (g), (h), (i) na (j), 13,14,19,20, 21, 35, 36, 37, 38, 39, 40, 50, 52, 53, 54,58 na 59.

"Kupitia uamuzi uliotolewa na Mahakama hiyo serikali ya Tanzania iliagizwa kufanya marekebisho ya vifungu kumi na sita vya Sheria ya Vyombo Habari ili kuendana na viwango vya kimataifa vya uhuru wa kujieleza.

"THRDC inaiomba Wizara kufanya marekebisho ya sheria na kanuni zote zinazominya uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa habari nchini Tanzania. Sheria hizo ni Pamoja na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, Kanuni za Maudhui ya Kielektroniki na Posta (Kanuni za Maudhui ya Kimtandao) za mwaka 2020 n.k,"imefafanua taarifa hiyo.

Aidha, THRDC imebainisha kuwa, Serikali inaweza kuitisha mkutano na wadau wa habari nchini ili kujadili maboresho na kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha sheria zinazominya uhuru wa vyombo vya habari.

"Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania umefurahishwa na jitihada zilizochukuliwa na Mhe. Waziri. Huu ni wakati muafaka kwa serikali kurekebisha sheria na kanuni zote zinazominya uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa habari hapa nchini,"imeongeza taarifa hiyo.

Post a Comment

0 Comments