Wabunge CCM wampa kura zote Mheshimiwa Zungu kuwania Unaibu Spika

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamempitisha kwa asilimia 100 Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu kuwania nafasi ya Naibu Spika wa bunge hilo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumpitisha Mbunge Zungu kukiwakilisha chama hicho kugombea unaibu Spika.
Awali Mheshimiwa Zungu amehaidi kushirikiana na wabunge wenzake endapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo katika uchaguzi utakaofanyika Februari 11, 2022.

Zungu ameyasema hayo leo Februari 9, 2022 baada ya wabunge hao kumpitisha kwa asilimia 100 katika uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa bungeni.

Mbunge huyo amechaguliwa na wabunge wa CCM baada Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kupitisha jina lake kati ya wagombea 11 waliochukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.

“Namshukuru Mungu muumba wa mbingu na nchi na Rais Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) ambaye ni mwenyekiti wa chama yeye na wajumbe wa Kamati Kuu (ya CCM) wote kwa kurudisha jina langu na kupigiwa kura na wabunge upande wa Chama cha Mapinduzi,”amesema.

Pia amewashukuru wabunge wa chama chake kwa kumpa kura za kishindo na ameahidi kufanya kazi nao ambapo amesema jukumu lake litakuwa ni kutekeleza maagizo ya Spika wa Bunge kwa kuwa ndiye bosi wake wa kwanza ndani ya Bunge.

Kabla

Nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Mheshimiwa Dkt.Tulia Ackson ambaye kwa sasa ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walimchagua, Mhe.Dkt. Tulia Ackson kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa Naibu Spika wa Bunge la 11 baada ya kumshinda mpinzani wake kutoka Chama cha Wananchi (CUF) Mhe. Magdalena Sakaya.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Mhe. Dkt. Ackson kushinda kwa kura 250 ambazo ni sawa na asilimia 71.2 za kura halali dhidi ya mpinzani wake Mhe. Sakaya aliyepata kura 101 ambazo ni sawa na asilimia 28.8 ya kura halali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news