WANAOTAKA KUHAMA NGORONGORO KWA HIARI WAJITOKEZE-WAZIRI MKUU

*Ataka waende kujiandikisha kwa DC, asema Serikali itawahudumia

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema wakazi wa wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha wanaotaka kuhama kwa hiari yao wajitokeze na waseme wanataka kwenda wapi.

“Suala la idadi ya watu ni kubwa. Kumbe huko nyuma kulishakuwa na mapendekezo. Yeyote anayeona anaweza kuishi mahali pengine yuko huru kusema. Kama yuko mtu wa aina hiyo, awe huru kwenda kwa DC (Mkuu wa Wilaya) kajiandikishe na Serikali itakuhudumia vizuri. Hayo ni maamuzi ya mtu binafsi, kusiwe na mtu wa kumshinikiza fulani asifanye maamuzi yake. Kama yuko aachwe afanye maamuzi yake, aseme anataka kwenda wapi na sisi tutamhudumia.”
Mheshimiwa Majaliwa alitoa kauli hiyo jana jioni Februari 17, 2022 wakati akizungumza na viongozi na wananchi wa tarafa ya Ngorongoro kwenye kikao cha ndani kilichofanyika makao makuu ya zamani ya NCAA, wilayani Ngorongoro.

Alisema hata katika suala la ushoroba wa kilometa za mraba 1,500 kule Loliondo kumekuwa na ubishi wa muda mrefu juu ya eneo tajwa lakini hakuna anayejua mipaka halisi ya eneo hilo.

“Ubishiubishi wa eneo kwenye namba upo kati ya wenyeji na wahifadhi lakini hakuna anayejua kiuhalisia eneo linaanzia wapi na linaishia wapi. Haya ni maamuzi ya mwaka 2018 yaliyofikiwa kwenye kikao cha Ololosokwan. Ni vema tukaweka alama za kudumu ili iwe rahisi kubaini eneo hilo; kilometa za mraba 1,500 zijulikane zina ukubwa gani na zinagusa eneo lipi,” alisema.

“Hakuna jambo linataka kufanywa kwa trick kwa kutaka kumuathiri Mtanzania, hakuna Serikali ya namna hiyo. Kila jambo linalozungumzwa kwenu ni jema tu, linafanywa kwa nia njema.”

Aidha Waziri Mkuu ameziagiza mamlaka zote zinazoshughulikia suala la uwekaji wa alama hizo zihakikishe zinawashirikisha viongozi wa maeneo hayo katika hatua zote.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mawaziri wa Maliasili na Utalii, Mifugo na Uvuvi, TAMISEMI, Naibu Waziri wa Ardhi, Makatibu Wakuu wa wizara za Maji na TAMISEMI na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wadau wengine walioshiriki mkutano huo ni Mbunge wa Ngorongoro, Bw. Emmanuel Shangai, viongozi wa kimila (Malaigwanan), wenyeviti wa vijiji na vitongoji, Baraza la Wafugaji la Ngorongoro na viongozi wa dini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news