Watetezi watoa ushauri mzito mgogoro wa ardhi Ngorongoro

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WATETEZI wa haki za binadamu nchini wametoa ushauri ambao unalenga kupata suluhu ya kudumu kuhusu mgogoro wa ardhi wilayani Ngorongoro Mkoa wa Arusha.

Ushauri huo umetolewa leo Februari 12, 2022 kupitia taarifa ya pamoja iliyotolewa na watetezi hao ikiwemo taasisi ya ALPHA AND OMEGA RECONCILIATION AND PEACE BUILDING (AREPEB), CIVIC AND LEGAL AID ORGANIZATION (CILAO),FOUNDATION FOR COMMUNITY INVOLVEMENT (FCI-TANZANIA), GREEN COMMUNITY INITIATIVES, HAKI ARDHI, HAKIMADINI, LEGAL AND HUMAN RIGHTS CENTRE.

Wengine ni MEDIA AID FOR INDIGENOUS PASTORALIST COMMUNITY, NGURUKA DEVELOPMENT AGENCY (NDA),PASTORALIST WOMEN COUNCIL (PWC), PINGOs Forum, RESOURCES ADVOCACY INITIATIVE,RUJEWA INTEGRATED EFFORTS TO FIGHT POVERTY (RIEFP),SAKALE DEVELOPMENT FOUNDATION (SADEF).
Pamoja na TALA, TANZANIA HUMAN RIGHTS DEFENDERS COALITION,TANZANIA MEDIA WOMEN ASSOCIATION (TAMWA),UCRT, WOMEN AND CHILDREN WELFARE SUPPORT (WOCWELS) na WOMEN AND CHILDREN’S LEGAL AID ORGANISATION.

"Sisi Watetezi wa Haki za Binadamu tunaofanya kazi zetu katika maeneo mbalimbali ya Tanzania,tumekuwa tukifuatilia kwa karibu hali ya haki za binadamu katika mgogoro wa ardhi Wilaya ya Ngorongoro na baadhi yetu wamekuwa wakishiriki katika kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro huu. 

"Kwa takribani wiki mbili sasa kumekuwa na taharuki kubwa miongoni mwa wananchi wa Ngorongoro kutokana na kuenea kwa taarifa na mikakati ya kuwahamisha katika maeneo yao ya asili. Wananchi katika Wilaya Ngorongoro wamekuwa na hofu ya maeneo yao kutwaliwa na wengine kuhamishwa toka katika Tarafa ya Ngorongoro (Hifadhi ya Ngorongoro) kwenda maeneo mengine nje ya wilaya.

"Siku za hivi karibuni yameibuka malalamiko kutoka kwa wananchi wa Ngorongoro kuhusu baadhi ya vyombo vya habari na watu mbalimbali wanaopotosha na kutoa taarifa za uongo na zenye kutweza utu wa wananchi washio eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. 

"Madai mbalimbali potofu yameendelea kutolewa kwenye baadhi ya vyombo mbalimbali vya habari na hata baadhi wa wabunge na watu wenye mamlaka. Taarifa hizo zimeleta taharuki kubwa kwa jamii za kifugaji na hata kupunguza ushiriki wao katika kazi zao za kawaida za kujpatia vipato.
"Kwa sasa jamii hii ya kifugaji imejikuta katika mazingira ya kuhisi kutengwa na kunyanyapaliwa kutokana na wao kuamua kuishi katika utamaduni wao katika mazingira asilia.

"Wananchi wamelalamikia vyombo hivi vya habari kwa kuendelea kuwadhalilisha katika taarifa zao pengine kwa lengo la kutaka kushawishi taasisi za umma kuwa wale wananchi ni wakosaji na wanapaswa kuondolewa katika makazi yao. Wakati huo huo tumesikitishwa na taarifa za wandishi wengine ambao wanatafuta nafasi ya kuwasikiliza wananchi kusumbuliwa wakati wanafanya kazi zao huko Ngorongoro.

"Agizo la Waziri Mkuu la wabunge kupewa semina na Wizara ya Maliasili na taasisi zake kuhusu historia na hali halisi kuhusu Wilaya ya Ngorongoro, wakati taasisi hizo zinalalamikiwa ni kinyume na misingi ya upatikanaji wa haki, kwani wataendeleza propanganda na taarifa ambazo zinavutia kufanikiwa kwa mikakati yao ya siku nyingi.

"Tuhuma inayotolewa dhidi ya Asasi za Kiraia kuwa wanapata fedha kutoka nchi za jirani kwa ajili ya uchochezi hazina ukweli wowote na endapo kuna mtu au taasisi yenye ushahidi iweke hadharani. Kwa miaka mingi sasa aina hii ya propaganda kwa asasi za kiraia wilayani Ngorongoro imekuwa ikitumika kutisha kazi za AZAKI wilayani Ngorongoro.
"Tunashauri Serikali ikae na wananchi kujadili juu ya tatizo la mgorogoro unaondelea katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Loliondo ili kuondoa upotoshaji unaoenezwa na baadhi ya vyombo vya habari, watu wenye maslahi binafsi, na taasisi zingine ili kupata mwafaka wa pamoja.

"Wakati huo huo tunapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwagiza Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kukutana na wananchi wa Ngorongoro na Loliondo ili kuwasikiliza na pengine kutatua changamoto zilizopo kwa pamoja. 

"Pia tunampongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Tulia Akson kwa kuiagiza Serikali kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro huu wa ardhi. Tunaendelea kusisitiza kuwa mgogoro huu usuluhishwe kwa umakini na kwa kushirikisha wananchi ambao ndio waathirika wakuu wa mgogoro huu.

"Tunalaani vikali matamshi ya viongozi mbalimbali ambao wamezungumza hadharani kuwa wananchi hawa waondolewe kwa nguvu hata ikibidi kutumia silaha za moto na vifaru kuwaondoa. Matamshi haya yamewahukumu wananchi hawa wanyonge bila hatia yoyote kwani hakuna kosa walilofanya hadi sasa kwa kuwa wapo kwa mujibu wa Sheria ya NCA ya mwaka 1959 katika hifadhi hiyo ya Ngorogoro inayotambua matumizi ya ardhi mseto,"imefafanua kwa kina taarifa hiyo ya Watetezi wa haki za binadamu nchini.

Kuhusu Mgogoro wa Ardhi Wilaya ya Ngorongoro

Kwa mujibu wa Watetezi hao, mgogoro wa ardhi katika Wilaya ya Ngorongoro ni wa muda mrefu sasa huku juhudi zilizofanyika kupata suluhu ya kudumu zikionekana kushindwa kuzaa matunda. 
"Kabla ya kupata uhuru, jamii za kifugaji zilipoteza ardhi yao huko Serengeti na kuhamishiwa maeneo ya Tarafa ya Ngorongoro na Loliondo na kuahidiwa hawataondolewa tena katika maeneo yao. 

"Wilaya ya Ngorongoro ina jumla za kilomita za mraba zaidi ya 14,000. Zaidi ya asilimia 75 ya eneo la Ngorongoro kwa sasa hutumika kwa shughuli za utalii na uhifadhi. Kilomita za Mraba 4000 kwa sasa ndio zimebaki kwa matumizi ya makazi ya watu na shuguli za kijaamii, taharuki imekuwa ikiibuka mara kwa mara katika kipindi cha miaka kadhaa toka mwaka 1992.

"Matukio ya kutaka kuhamisha watu yamekuwa yakifanyika mara kwa mara na huku ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ukishuhudiwa. Mfano katika mikakati ya kutwaa ardhi ya vijjiji katika Tarafa ya Loliondo baadhi ya nyumba za wananchi zilichomwa moto, watu kupoteza maisha, mifugo kufa na mali za raia kuharibika.

"Jambo la kushukuru na kutia faraja ni kuwa miaka yote hii viongozi wa juu wa Serikali wamekuwa wakiingilia kati migogoro hii na kuondoa hofu kwa wananchi. Tunaamini pia sasa viongozi wa juu wa nchi yetu wataweza kutafuta suluhu ya kudumu. Kwa mfano mpango wa kuchukua eneo la vijiji vya Loliondo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1500 katika Tarafa ya Loliondo ulikwama baada ya aliyekua Waziri mkuu wa wakati huo, Mheshimiwa Mizengo Pinda kutoa amri ya kusimamisha mpango huo mpaka pale serikali itakapokuja na mpango mwingine utakaozingatia haki za wananchi kama wamiliki halali wa ardhi.
"Migogoro ya ardhi baina ya wananchi na wahifadhi au Mamlaka za Hifadhi na Wizara ya Mali Asili umeendelea kukua wilayani Ngorongoro pale mipango ya kuwahamisha wananchi wanaoshi na kuzunguka maeneo ya Hifaddhi ya Ngorongoro kuanza kuibuka tena mwezi Aprili 2021.

"Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ilitoa maelekezo ya kuwaondoa baadhi ya wananchi katika eneo la hifadhi kwa madai kuwa ni wahamiaji haramu, wengine kwa mamia kutakiwa kubomoa majengo yakiwemo shule za msingi za Serikali, vituo vya afya, vituo vya polisi, makanisa, misikiti na nyumba binafsi za wananchi. 

"Baada ya malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi zoezi hilo lilisitishwa hadi mwaka huu tena ambapo mikakati mingi na isiyoshirikishi imekuwa ikionekana kuelekeza baadhi ya watu kujiandaa kuondoka katika maeneo ya Wilaya ya Ngorongoro,"imefafanua taarifa hiyo.

Hoja za kuondoa watu katika maeneo ya Ngorongoro

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Watetezi hao imefafanua kuwa, "Kwanza tunatambua kwa kiasi kikubwa umuhimu wa uwepo na kuendelea kuilinda Hifadhi ya Ngorongoro na tupo tayari kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha eneo hilo linaendelea kuhifadhiwa. 

Hata hivyo, bado tunadhani hoja zinazotolewa ili kushawishi uhamisho wa watu katika maeneo ya Wilaya ya Ngorongoro zinahitaji utafiti shirikishi ili kufikia mamuzi ya pamoja na jamii. Baadhi ya hoja hizo ni hizi zifuatazo;

"Ongezeko la idadi ya watu. Madai kuwa kuna wananchi zaidi ya 100,000 Ngorongoro bila kuwa na rejea yoyote ya kisayansi yaweza kuwa potofu. Itakumbukwa kwamba hata sensa inayofanywa hujumuisha wafanyakazi wa idara mbalimbali za Serikali ambao siyo wafugaji. Mfano walimu, watumishi wa afya, wafanyakazi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), wafanyakazi wa hoteli za kitalii na hata madereva wanaoendesha magari ya kubeba watalii. 
Hata hivyo, ongezeko la idadi ya wananchi Ngorongoro siyo kosa kwa wananchi hawa kwa kuwa ni haki ya kila mtu kuzaliana. Tumeshudia kigezo hiki cha kuongezeka kwa watu kikitumiwa kama fimbo ya kuwananga wananchi kwa
bahati mbaya baadhi ya watu wamekuwa wakitumia ukosefu wa huduma hizi kupotosha umma wa Watanzania.

Ukweli ni kwamba hali duni ya maisha na ukosefu wa huduma muhimu umechangiwa sana na kushindwa kwa mamlaka husika ikiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kutimiza wajibu wake wa kusimamia malengo mahususi ya uanzishwaji wa hifadhi hii mseto. 

Wananchi hawa wamekuwa wakiwekewa vikwazo vingi ambavyo vimechangia kwa kiasi kikubwa uduni wa maisha wa watu wale kwa sasa. Changamoto hizi zilozosababishwa na sheria na usimamizi wa Hifadhi ya Ngorongoro usiozingatia usawa na haki za wananchi ndi leo unaonekaana kama sababu ya kuwaondoa watu wale.

"Changamoto za wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro zimekuwa kubwa zaidi kutokana na ugumu wa kutenda kazi katika maeneo hayo kwa watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari na wanasheria walio tayari kusaidia wananchi. Miaka ya nyuma wapo waliowahi kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kughushi pamoja na makosa ya uchochezi.

"Baadhi ya waandishi wa habari na vyombo vya habari navyo vimekuwa vikipata ugumu wa kupata taarifa sahihi kuhusu hali ya Ngorongoro. Itakumbukwa kuwa mnamo Februari 3, 2022, waandishi wa habari sita walizuiwa kwa muda na kuhojiwa kwa tuhuma za kuingia bila vibali kwenye eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Haya ni matukio yanayoongeza hofu miongoni mwa wananchi, Watetezi wa Haki za Binadamu na Waandishi wa Habari,"imeendelea kufafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Wito 

Watetezi wa Haki za Binadamu kupitia taarifa hiyo wamefafanua kuwa, "Kwa vile Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameagiza kufanyika kwa mchakato wa kuwashirikisha wananchi na baadaye mpango huo kuoneshwa kwa vitendo na Mheshimiwa Waziri Mkuu ili kupata mawazo huria kutoka kwa wananchi ni budi yafuatayo yazingatiwe.

"Mosi, tunamuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwapa nafasi wadau huru kama vile wananchi wa Ngorongoro, Watetezi wa Haki za Binadamu na wadau wengine kushiriki katika kutoa elimu kwa wabunge kuhusu hali halisi ya Wilaya ya Ngorongoro. 

"Hii inatokana na ukweli kwamba Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, TAWA na Wizara ya Maliasili na Utalii wanatuhumiwa na wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro kuwa na nia ya kuwahujumu. Tunamuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aone kwamba kitendo cha Wizara, NCAA na TAWA kupewa fursa ya kutoa semina kwa watoa maamuzi ikiwa ni pamoja na Bunge bila kuwapa wananchi fursa hiyo kunaweza kuchochea taarifa za upande mmoja wa makundi yanayovutana kuhusu Ngorongoro.

"Pili tunaikumbusha Serikali kuzingatia kwamba, mwaka 1958 Hifadhi ya Ngorongoro ilipoanzishwa ilikuwa na malengo makuu matatu ambayo ni Uhifadhi,Kulinda maslahi ya wenyeji walioondolewa Serengeti kwa mkataba na wakoloni na Utalii.

"Maslahi haya matatu yaliingizwa katika sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wakati wa wakoloni na yameendelea kuwepo katika sheria ya sasa ya mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. 

"Gavana wa Tanganyika, Richard Turnbull alisema, “...Endapo kutakuwa na mgogoro wa masilahi Ngorongoro kati ya masilahi ya wa Maasai na mifugo yao kwa upande mmoja na masilahi ya wanyamapori na watalii kwa upande mwingine, wa Maasai na mifugo wapewe kipaumbele.”
"Tatu,tunaisihi Serikali itambue kwamba ufukara uliopo Wilaya ya Ngorongoro na ukosefu wa huduma za jamii ni zao la mamlaka kushindwa kusimamia malengo ya uanzishwaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA). Serikali itambue kuwa kitendo cha kuwahamisha watu wa Ngorongoro na Loliondo kutasababisha madhara makubwa kwa jamii hizo ikiwa ni pamoja na kuwakosesha wananchi amani, uhuru na maendeleo katika vijiji vyao.

"Pia itabidi wananchi hawa wapewa fidia kubwa sana kwa kuwa wao wameshiriki kwa miaka mingi kulinda hifadhi hiyo na kuzuiwa kufanya shughuli zozote za kiuchumi. Fidia ya eneo hili ni tofauti kabisa na fidia zinazoangalia kilichopo kwenye ardhi.

"Nne, Serikali iunde tume huru itakayowahusisha wafugaji wenyeji wa Ngorongoro, wataalam wa uhifadhi, watetezi wa haki za binadamu, wadau wa utalii, wataalam wa mifugo, wadau wa haki za binadamu ili ifanyike utafiti jumuishi kuhusu hoja zinazobishaniwa na baadaye kuja na mapendekezo yatakayozingatia ulinzi wa hifadhi pamoja na haki za jamii ya Ngorongoro.

"Tano, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na NCAA ziachane na nia ya kuwahamisha wafugaji kutoka Ngorongoro na kuchukua ardhi ya vijiji vya Loliondo ili kulinda lengo la uwepo wa NCA na pia kulinda haki za wenyeji wanaoshi katika maeneo hayo kwa mujibu wa sheria. Ikumbukwe pia kuwa uhifadhi wa eneo la Ngorongoro unategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa wananchi wakaazi wa eneo hilo kama wahifadhi asili. 

"Pia watalii wengi wanakuja Ngorongoro kwa lengo la kujionea pia upekee wa matumizi ya ardhi mseto na tamadamu za jamii ya Kimasai.

"Sita,tunaliomba Bunge letu lisimamie mijadala ya wabunge kuhusu Ngorongoro kwa usawa na kukemea lugha zinazotweza utu wa wananchi wa Ngorongoro waliojitoa sadaka kwa miaka mingi kulinda rasilimali zile wilayani Ngorongoro.

"Itambulike kuwa wananchi wa Ngorongoro hawana kosa lolote kwani kuongezeka idadi ya binadamu na mifugo sio kosa lolote kisheria.

"Saba, sheria inayounda Mamlaka ya Uhifadhi ya Ngorongoro ipitiwe upya na kuboresha usisimamizi na ulinzi wa haki za wananchi pamoja na kuhakikisha hifadhi inalindwa na kuendelezwa.
"Nane, kudhibiti shughulizi zingine za kibinadamu zinazosababishwa na ongezeko la shughuli za kitalii katika Hifadhi ya Ngorongoro. Mfano kudhibiti ujenzi wa hoteli na wingi wa magari.

"Tisa,kuondoa nia ya kutaka kuchukua ardhi ya vijiji 14 vya Loliondo zenye kilomita za mraba 1500 na badala yake kuwe na makubaliano baina ya serikali na wananchi kuyalinda maeneo hayo kwa shughuli za mifugo na wanyama pori.

"Kumi,kuepuka nia ya kutaka kuwahamishia wafugaji wa Ngorongoro maeneo mengine kwa kuwa tayari maeneo mengi nchini yana migogoro ya wakulima na wafugaji.
"Kumi na moja,kupanga kwa pamoja na wananchi maeneo ambayo yatabaki pekee kwa shughuli za uhifadhi katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kuwaacha wananchi katika kata au kanda ambazo hazina mwingiliano mkubwa na shughuli za uhifadhi kwa kuwa Hifadhi ya Ngorongoro ina eneo kubwa la kilomita za mraba 8,400.

"Kumi na Mbili, kutoa uhuru wa kutosha wa wadau mbalimbali wakiwepo waandishi wa habari, watafiti na watetezi wa haki za binadamu kufuatilia kwa ukaribu mgogoro huu kwa lengo la kutoa nafasi ya kupata maoni ya wengi juu ya mgogoro huu.

"Kumi na Tatu, ikumbukwe kuwa wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa wa mgogoro huu kwani wamekuwa wakikosa makazi bora, elimu, maji na huduma ya afya. Hivyo ukweli halisi uzungumzwe kwa maslahi ya wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro,"wamefafanua kwa kina Watetezi wa Haki za Binadamu kupitia taarifa hiyo ya pamoja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news