Wawekezaji wavutiwa na uongozi wa Rais Samia, mikakati ya BoT

NA GODFREY NNKO

UONGOZI wa Kiwanda cha Marmo E. Granito Mines (T) Ltd kilichopo jijini Mbeya umeipongeza Serikali nya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa mipango, mikakati na jitihada za kizalendo za kuinua uchumi wa nchi ikiwemo uchumi wa viwanda.
Pongezi hizo wamezitoa leo Februari 16, 2022 wakati wa ziara katika miradi ya maendeleo iliyoratibiwa na Benki Kuu ya Tanzania ikiwa ni mwendelezo wa mafunzo kwa waandishi wa habari za uchumi na biashara yanayoendelea Ukumbi wa Benki Kuu tawi la Mbeya.

Mafunzo hayo ya siku tano ambayo yalianza Februari 14,2022 huku yakiwajumuisha waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini yanaratibiwa na BoT.
Meneja Utawala wa Kiwanda cha Marmo E.Granito Mines (T) Ltd, Binthony Kulliga amesema kuwa,uongozi thabiti wa Rais Samia umewezesha kiwanda hicho cha kukata, kung'arisha na kuuza bidhaa zinazotokana na mawe ya asili aina ya Marbe na Granite yanayopatikana hapa nchini kupiga hatua kubwa.
"Ifahamike kuwa mradi huu ni wa wazalendo kwa maana ya Watanzania, hivyo mipango, mikakati na jitihada za kizalendo za kuinua uchumi zinazotokana na uongozi thabiti wa Rais Samia umetuwezesha kupiga hatua. Pia tunaipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa mikakati yake ya kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari za biashara, uchumi na fedha.

"Kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuelimisha umma wa Watanzania kuhusiana na masuala ya uchumi na uwekezaji. Tunaamini kuwa, kupitia mafunzo hayo waandishi wa habari na vyombo vya habari vitatusaidia sana kuufahamisha umma wa Tanzania katika kuufahamu uwezekaji wetu na hivyo kufungua fursa zaidi za masoko ya bidhaa zetu za ndani na nje ya nchi,"amesema Bw.Kulliga.
Meneja Utawala huyo amesema, kiwanda hicho kilianza kufanya kazi mwaka 2004 na baadaye kampuni iliamua kuweka mpango wake wa miaka mitano ya upanuzi wa kiwanda na hatimaye mwaka 2008 kampuni iliweza kununua mitambo mipya na ya kisasa na kufungwa mpaka kukamilika.

Amesema, awali kiwanda hicho kilikuwa kidogo na chenye kutumia teknolojia ya kizamani na yenye uwezo mdogo wa kuzalisha mali.

"Hivyo kwa wakati huo kazi kubwa ilikuwa ni kusafirisha malighafi nje ya nchi.Lengo kuu la kupanua mradi huu lilikuwa ni kuthamanisha malighafi ili kukidhi hitaji la soko la ndani na nje ya nchi, hatimaye miaka minne baadaye (2012) uzalishaji ulianza rasmi kuchakata upande wa marble. Hata hivyo, kampuni yertu bado inao mpango mwingine wa kupanua zaidi mradi huu ambao ni wa kipekee hapa nchini na Kusini mwa Jangwa la Sahara.

"Kuwepo kwa mradi huu siyo tu tunautangaza mkoa wetu wa Mbeya katika ramani ya Dunia bali pia Taifa letu kwa kuzingatia kuwa bidhaa yetu bado inaendelea kuenea katika soko la ndani na Kimataifa na hivyo kutoa fursa ya kuongeza ari ya uzalishaji ili kukidhi soko la ndani ya nje ya nchi,"amesema.

Amesema, mradi huo wa kipekee nchini Tanzania kutokana na teknolojia yake ambapo vyuo vya hapa nchini havina mitaala katika silabi zao juu ya uzalishaji wake.
"Hata hivyo, kampuni yetu imethubutu na kuchukua jukumu la kuajiri na kufundisha wafanyakazi wazawa. Lengo likiwa ni kuiunga mkono Serikali yetu katika suala zima la kuzalisha ajira kupitia sekta binafsi na hivyo kuongeza ajira na kuongeza uchumi wa nchi yetu ambao kwa kiasi kikubwa unahitaji maendeleo ya uchumi wa viwanda kama ilivyo sera ya Serikali yetu ya Awamu ya Sita,"amesema Meneja Utawala huyo.

Pia amesema,mradi huo ulipokuwa ukianza ulikuwa na wafanyakazu wazalendo wapatao 35, baada ya ujenzi wa kiwanda tayari mradi umekuwa na wafanyakazi wazalendo wasiopungua 100 kwa sehemu ya kiwanda na migodini.

Amesema, kwa ujumla asilimia 80 ya walioajiriwa ni wazalendo na wanatarajia kadri uzalishaji utakavyoongezeka machimboni na viwandani kampuni itaongeza ajira zaidi.

Pia amesema kuwa, wamekuwa wakishiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii ikiwemo kuchonga barabara na kutengeneza madaraja kwa gharama zake yenye maeneo ya Nanyala barabara kuu iendayo Tunduma kuelekea machimboni Majimoto, Songwe barabara ambayo imewezesha kutumiwa na wawekezaji wengi Nanyala.
"Kampuni imeshiriki katika ujenzi wa zahanati ya Nanyala pamoja na nyumba ya daktari Mbozi, Zahanati ya Kijiji cha Itete Kata ya Isuto huko Mbeya Vijijini. Na kampuni imeweza kuchangia katika kuwakatia bima ya afya wazee wa Kata ya Nanyala wasiopungua 100 kwa miaka miwili kwa maana ya mwaka 2017 hadi 2018 na mambo mengine mengi,"amesema.

Ameongeza kuwa, kutokana na uwepo wa mazingira mazuri ya uwekezaji hapa nchini nao wanakiri kuna mwelekeo mzuri wa kiuchumi.
"Hivyo ni wito wetu kwa taasisi mbalimbali za Serikali, binafsi na wadau mbalimbali kutuunga mkono katika kununua bidhaa zetu bora za ujenzi zinazozalishwa hapa kiwandani mfano taasisi kama TBA, NHC, NSSF na hususani wakati huu ambapo Serikali imeamua kuhamia mkoani Dodoma.

"Niendelee kumpongeza tena Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kueweka sera nzuri hasa kwa wawekezaji wa ndani na nje na juhudi zake za kukuza uchumi tumeanza kuziona pia.
"Tunaushukuru uongozi wa BoT mkoani Mbeya kwa ushirikiano wanaotupatia na sasa wamekuja na mpango mpya wa kutembelea wawekezaji wa ndani ili kujua fursa zaidi za kiuchumi zilizopo nchini nasi tunaamini kuwa kwetu ni fursa nzuri yenye kukusudia kuendeleza wawekezaji wa ndani ya nchi,"amefafanua Bw.Kulliga.

Post a Comment

0 Comments