Waziri Bashungwa awaachia habari njema wananchi wa Tembela jijini Mbeya

NA ANGELA MSIMBIRA, OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Tembela ili kutatua changamoto ya miundombinu ya barabara na madaraja katika eneo hilo.
Akikagua miundombinu ya barabara katika Kata ya ya Tembela iliyopo Halmashauri ya Jiji la Mbeya mkoani Mbeya leo Februari 15,2022, Mheshimiwa Bashungwa amesema, ujenzi wa Daraja la Tembela litasaidia kuunganisha wananchi wa Kata ya Mwasanga, Mwakibete, Tembela na Mbeya Vijijini.

Ni wananchi ambao walikuwa wakipata adha ya mawasiliano ya barabara tangu daraja hilo lilipobomoka mwaka 2019 na kusababisha vifo vya watu watano katika eneo hilo.

Waziri Bashungwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo na kusikiliza kilio cha wananchi wa kata hizo ili kutoa nafuu ya mawasiliano ya barabara katika eneo la Mbeya Mjini na Vijijini.

Amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Charles Mwita kuhakikisha mkandarasi anaanza ujenzi wa daraja hilo ifikikapo Machi Mosi, 2022 na kuhakikisha anatuma picha mnato na video zinazoonesha ujenzi huo umeanza kufanyika.

Waziri Bashungwa amemuagiza Meneja huyo kuhakikisha wanasimamia kikamilifu ujenzi huo ili thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali ziweze kutumika kwa ufanisi ili daraja hilo lijengwe katika ubora

Amesema kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha inatatua changamoto za miundombinu ya barabara kwa wakati na kurejesha mawasiliano katika kata husika ili kuinua uchumi wa kata hizo.

Pia amewashukuru wananchi kwa kuendelea kuunga mkono Serikali kwa kujitolea kuweka madaraja mbadala lengo likiwa ni kuhakikisha madaraja hayo yanapitika na wananchi wanaendelea kupata huduma.

Naye Diwani wa Kata ya Tembela, Fred Kibeso Mwasoke amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo ambalo linaunganisha maeneo ya Mwasanga, Mwakibete, Matembele na vijiji vinavyozunguka, kwa kuwa wanaamini kuwa uchumi utafunguka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news