Waziri Dkt.Gwajima aguswa na juhudi za Rhobi Samwelly mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili, unyanyasaji Mara

NA FRESHA KINASA

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maluum, Mheshimiwa Dkt.Dorothy Gwajima amepongeza juhudi za mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni zinazofanywa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania la mkoani Mara hatua ambayo amesema ina tija katika kuiwezesha Serikali kutokomeza vitendo hivyo kwa maendeleo ya Taifa. 
Rhobi Samwelly ambaye ni Mkurugenzi wa Hope for Girls and Women in Tanzania (katikati) akifafanua jambo kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Dkt.Dorothy Gwajima.
Mabinti wa Kituo Cha Nyumba Salama wakiimba.
Waziri Gwajima akicheza ngoma ya Litungi na wasanii wa ngoma hiyo alipotembelea Kituo Cha Nyumba salama na viongozi mbalimbali wa wizara hiyo.
Rhobi Samwelly ambaye ni Mkurugenzi wa Hope for Girls and Women in Tanzania (katikati) akifafanua jambo kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Dkt.Dorothy Gwajima.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo Februari 8, 2022 alipotembelea Kituo cha Nyumba Salama kilichopo Kiabakari Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara ambapo alipata fursa ya kuzungumza na wananchi na wasichana waliokimbia vitendo vya ukatili wa kijinsia wanaopatiwa hifadhi na kuendelezwa kielimu na shirika hilo akasisitiza kuwa, Serikali inathamini juhudi hizo na inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kumaliza ukatili kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia, wasanii na wadau wa maendeleo kupitia makongano na utoaji wa elimu kwa Jamii. 

"Shirika mmeonesha kazi nzuri ya kizalendo katika kushirikiana na Serikali kupambana na ukatili, mabinti hawa bila huduma yenu wengine wangekuwa wameshaolewa na kuzaa na kupoteza tumaini la kufikia ndoto zao, wengine wangekuwa wamefariki kutokana na kutokwa damu nyingi wakati wa kukeketwa, kupata ulemavu, lakini ni Jambo jema na la faraja leo mnatumaini la kufikia ndoto zenu mkiwa katika kituo hiki, someni kwa bidii na kuwa na malengo ili kwa baadaye muoneshe mfano kwa jamii yenu na taifa pia,"amesema Waziri Gwajima.

Ameongeza kuwa, Jamii haipaswi kuwafanyia vitendo vya ukatili watoto wa kike kwa kuwaozesha na kuwakeketa kwani wanamanufaa makubwa kwa maendeleo ya jamii na taifa wakiwezeshwa kielimu. Ambapo pia ameviomba vyombo vinavyosimamia sheria kuwawajibisha kikamilifu kwa kuwapa adhabu kali wanaobainika kuhusika kufanya vitendo vya ukatili. 

Pia, Waziri Gwajima amewataka wasichana wanaohifadhiwa katika kituo hicho kutumia karama zao wakiwa katika umri mdogo kutengeneza uchumi bora katika maisha yao na Serikali itaendelea kuwafuatilia kwa karibu katika kuhakikisha wanafika mbali zaidi.
"Ni muhimu waliohudumiwa na shirika hili baada ya kukimbia ukeketaji na kuendelezwa hadi kupata mafanikio wajitokeza hadharani kutoa shuhuda kupitia vyombo vya habari, wapaze sauti kusudi watu wajue kuwa ukatili hauna faida. Wapo wamesoma na kufikia ngazi mbalimbali wamesomeshwa na shirika hili wakisema watu wakasikia watajifunza kusomesha mabinti hadi wanapofikia malengo yao na kuachana na ukatili,"amesema Waziri Gwajima.

Aidha, Waziri Gwajima ameitaka jamii kuwasomesha watoto wa kike na kuwaandaa kuja kuwa watumishi na viongozi wa Taifa la kesho, huku akisisitiza jamii kuachana na mila potofu zenye madhara. Na pia akahimiza juhudi madhubuti ziendelee kufanywa na kila mwananchi kwa nafasi yake kumaliza ukatili kwa kuwafichua wahusika na kuwaripoti katika vyombo vya sheria. 
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly akitoa taarifa ya ya shirika hilo kwa Waziri Gwajima, amesema tangu kuanza kwa shirika hilo 2017 limeweza kusaidia wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia wapatao 1,345 na kutoa elimu ya madhara ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watu zaidi ya 180,011 katika taasisi za elimu kwa wanafunzi, makanisani, mikutano ya hadhara na makongamano mbalimbali. 

Ameongeza kuwa, shirika hilo linaendelea kuwapa hifadhi wasichana waliopo katika vituo vinavyomilikiwa na shirika hilo, utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya Ukatili wa Kijinsia kwa kushirikiana na Ofisi za Madawati ya Jinsia, Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Jamii katika Kituo cha Nyumba Salama Mugumu na Butiama sambamba na kuwaendeleza kielimu wasichana katika vituo hivyo ili wafikie ndoto zao.
Rhobi ameongeza kuwa, vituo vya shirika hilo vinakabiliwa na ukosefu wa nyumba kwani katika vituo vyote wamepanga, baadhi ya wazazi kukataa kuwapokea watoto wao wanaporudi makwao baada ya msimu wa ukeketaji kuisha, gharama za kuhudumia matibabu wasichana waliopo katika vituo hivyo wanapougua. Huku akibainisha kwamba shirika hilo lina mkakati wa kujenga kituo cha kudumu kwa ajili ya kutoa hifadhi.
Waziri Gwajima akiagana na wacheza ngoma ya litungi mara baada ya kufanya ziara katika Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari Butiama mkoani Mara.

Post a Comment

0 Comments