Waziri Mchengerwa afika Muhimbili kumjulia hali Profesa Jay

NA JOHN MAPEPELE

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe. Mohamed Mchengerwa amemtembelea aliyekuwa Mbunge wa Mikumi na Msanii wa Muziki wa kizazi kipya, Bw. Joseph Haule (Prof. Jay) anayetibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mhe. Mchengerwa amefika leo Februari 12, 2022 kumjulia hali msanii huyo na kuwasilisha salamu za Serikali kama msimamizi Mkuu wa Sekta ya Sanaa hapa nchini.

“Nimefika kumjulia hali mmoja wa wadau na miongoni mwa wasani ambao tunatambua na kuthamini mchango wa kazi zake za sanaa ambazo zimehamasisha vijana wengi kujiajiri kupitia Sanaa ya muziki hapa nchini,"amesema Mheshimiwa Mchengerwa.


Tayari Serikali kupitia Wizara ya Afya imesema itagharamia matibabu yake hadi hapo ataporuhusiwa kutoka hospitalini hapo.
Kwa upande wake mke wa Prof. Jay, Bi. Grace Mgonjo amemshukuru, Mhe. Mchengerwa kwa upendo wa kuja kumwona msanii huyo. 

Pia ameushukuru Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuwapokea na kuwahudumia vizuri.

Katika hatua nyingine Waziri Mchengerwa amewapongeza madaktari na wauguzi wa Hospitali hiyo kwa kazi nzuri wanayofanya ya utoaji wa matibabu ya kibingwa kwa Watanzania.

Post a Comment

0 Comments