Waziri Mkuu atoa maagizo nane kwa TARURA

NA MWANDISHI MAALUM, OR-TAMISEMI

WAZIRI Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amesisitiza mambo nane kwa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) ikiwemo ya kuhakikisha hawatoi kazi kwa wakandarasi wasio na uwezo. 

Mhe. Majaliwa ametoa maagizo hayo wakati wa kutoa hotuba ya kuahirisha Mkutano wa Sita wa Bunge la 12 jijini Dodoma leo Februari 18,2022.
Amesema, Serikali inatambua umuhimu wa barabara katika kuboresha maisha ya watanzania vijijini na mijini kiuchumi na kijamii pamoja na kukabiliana na changamoto katika usimamizi wa mtandao wa barabara za wilaya. 

Hivyo,Mhe.Majaliwa amewasisitiza watendaji wa TARURA wasimamie kwa karibu na kwa umakini kazi zinazofanywa na wakandarasi kwa ajili ya kubaini mapema na kuchukua hatua stahiki za kisheria kwa mujibu wa mikataba iliyopo. 

"Ufuatiliaji ufanywe mara kwa mara ili miradi ikamilike katika muda uliopangwa na kwa ubora stahiki,"amesema.

Mhe. Majaliwa amesema, TARURA ifanye tathmini ya kina ili kufahamu uwezo wa wakandarasi hususan uwezo wa kifedha, wataalamu walionao, vitendea kazi na ubora wa kazi walizokwisha kuzifanya kabla ya kuwapa kazi ili ujenzi wa barabara zetu ukamilike kwa wakati na kwa viwango. 

"Hapa nisisitize wakandarasi wasio na uwezo kutopewa mikataba na suala hili lisimamiwe ipasavyo kwa kuwa baadhi yao wanafahamika,"amesema.

Mhe. Majaliwa pia amesisitiza wakandarasi wanaofanya kazi vizuri kwa kuzingatia makubaliano ya mikataba walipwe fedha zao mapema bila urasimu ili waweze kukamilisha miradi wanayoitekeleza kwa wakati na kwa ubora uliokubaliwa bila kuzungushwa.

Amesema, pia asilimia 60 ya kazi za TARURA zitangazwe mapema, bila kusubiri mpaka mwaka wa fedha uanze. Mwaka wa fedha unapoanza iwe ni makandarasi kuanza kazi.

Waziri Mkuu Majaliwa pia amesisitiza watumishi wa TARURA kujiepusheni na kazi zenye mgongano wa maslahi. 

"Kwa mantiki hiyo, ikiwa unataka kufanya biashara na Serikali wakati wewe ni mtumishi wa umma ni vyema ukaacha kazi ili ufanye biashara yako kwa ufanisi,"amesema Waziri Mkuu.

Mhe. Majaliwa pia amewasiaitiza viongozi wa TARURA katika ngazi zote kufanya kazi kwa uwazi bila upendeleo na kutaka taarifa za maandalizi ya miradi zishirikishe halmashauri, wilaya na mikoa na pia zitolewe katika ngazi hizo.

Aidha, amesisitiza kuwa ujenzi wa barabara uende sambamba na kupanda miti kandokando ya barabara.

Mhe.Majaliwa pia ametaka Mtendaji Mkuu wa TARURA ahakikishe fedha zinazostahili kupelekwa mikoani zinatumwa kwenye mikoa husika ndani ya siku tatu huku akisistiza kuwa Mameneja watakaozembea kutekeleza majukumu yao ipasavyo waondolewe katika nafasi zao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news