Diamond Platinum:Rais Samia ametuheshimisha wasanii

*Waziri Mchengerwa ashuhudia uwekezaji mkubwa wa Wasafi Media, aelezea mikakati ya Serikali

NA MWANDISHI WETU

MKURUGENZI Mkuu wa Wasafi Media na msanii maarufu ndani na nje ya Bara la Afrika, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platinum amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuwaunganisha wasanii ili sekta ya sanaa iweze kuwanufaisha.
Diamond amesema haya leo Machi 25, 2022 mbele ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa alipotembelea Kampuni ya Wasafi inayomiliki lebo ya Wasafi, Wasafi TV na Wasafi FM redio kwa lengo la kukagua kazi za sanaa.

Amesema, Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni imefanya mapinduzi makubwa katika sanaa kwa kubuni mikakati mbalimbali ya kuwaunganisha na kuwanufaisha wasanii.

Miongoni mwa mikakati aliyoitaja kuwa mizuri ya Serikali ni pamoja na kurejesha tuzo za muziki.

Kwa upande wake Waziri Mchengerwa amesema, Serikali imeshatenga fedha nyingi kwa ajili ya kuwekeza kwenye sanaa ili wasanii waweze kunufaika.

"Nimekuja hapa leo ikiwa ni mwendelezo wa ziara yangu ya kukutana na wadau wa sekta ninazozisimamia ili kuwaunganisha na Serikali yao, nimefurahi kuona Wasafi mnaibua vipaji na kutoa ajira kwa wasanii nchini,"amepongeza Mhe.Mchengerwa.

Amesema, Serikali itaendelea kuwasaidia wasanii wote bila kuwabagua na kwamba Serikali inathamini mchango mkubwa unaotolewa na wasanii nchini.

Akielezea kuhusu utoaji wa burudani wa vituo vyake Diamond amefafanua kuwa, vinajitahidi kwenda na teknolojia ya kisasa katika kuendesha vipindi vyenye maudhui ya kuelimisha na kuburudisha jamii.

Katika ziara hiyo, Mhe.Waziri amepata fursa ya kutembelea na kukagua shughuli za kampuni hiyo na kujionea uandaaji wa vipindi mbalimbali vya michezo na burudani vinavyotangazwa na vituo hivyo.

Mkurugenzi wa vipindi wa Wasafi, Nelson Kisanga amesema, Wasafi FM imekuwa na vipindi maarufu vya michezo vya Sports Arena na Sports Court ambavyo vimekuwa na wasikilizaji wengi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news