IGP Sirro afanya mabadiliko ya makamanda

*Nafasi ya Kamanda Nyigesa inachukuliwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP William Mwampagale 

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

JESHI la Polisi nchini limemrudisha makao makuu ya jeshi hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Wankyo Nyigesa ili kupisha uchunguzi kutokana na matamshi aliyoyatoa Machi 26, 2022 katika sherehe za kumuaga wakati akihamishwa kutoka mkoani Pwani kwenda Kagera.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro.

Awali Wankyo Nyigesa alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani baadae akahamishiwa Mkoa wa Kagera.

Machi 26,2022 akizungumza katika sherehe za kumuaga wakati akihamishwa alisema kuwa, anatamani siku moja Rais Samia amuote na kumtamka kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) ili akafanye kazi kubwa ya kuleta mabadiliko.

“Mimi naomba nifanye miaka mitatu tu, halafu baadaye nimwambie mama... ‘mimi nakukabidhi naondoka, unaonaje hapo,’” alisema Nyigesa huku watu waliohudhuria hafla hiyo wakiangua vicheko.

Pia alisisitiza kwamba IGP aliyepo madarakani, Simon Sirro hajafanya makosa, anafanya mambo mazuri lakini yeye atafanya mazuri zaidi.

“Unajua binadamu lazima 'utarget' (ulenge) ya mbele, kuwa na ndoto kubwa, sasa huwezi kuwa na ndoto kwamba nitaendelea kuwa kamanda, mimi nataka kuwa nafasi hizo, kamishna, IGP ili baadaye nifanye makubwa ambayo nimeyafanya,”alisema Kamanda Nyigesa siku hiyo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 29, 2022 na msemaji wa jeshi hilo, David Misime imeeleza kuwa, Mkuu wa Jeshi hilo, Simon Sirro amesema nafasi ya Kamanda Nyigesa inachukuliwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), William Mwampagale.

Aidha,taarifa hiyo inaeleza kuwa matamshi aliyoyatoa yanaonesha kuwepo na ukiukwaji wa nidhamu kulingana na miongozo ya Jeshi la Polisi nchini.

“Suala hilo limeanza kufanyiwa kazi na matokeo ya uchunguzi huo yatafikishwa katika mamlaka za kinidhamu kwa hatua zaidi,” imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Msemaji wa jeshi hilo.

Wakati huo huo aliyekuwa Afisa Mnadhimu Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Theopista Mallya anakuwa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo anachukua nafasi ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), William Mwampagale ambaye amehamishwa kwenda kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera.

Pia taarifa imeeleza kuwa, aliyekuwa Mkuu wa Operesheni mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Mashenene Mayila anakuwa Afisa Mnadhimu wa Mkoa wa Rukwa.

Post a Comment

0 Comments