KARAGWE WAPATA SHULE YA PILI YA SEKONDARI KIDATO CHA TANO NA SITA

*Aahidi kumaliza changamoto ya upungufu wa walimu wa sayansi, hisabati na sanaa katika shule hiyo

NA OR- TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala na bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari Kituntu ili mwakani (2023) ianze kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita.
Mheshimiwa Bashungwa ameyasema hayo leo Machi 28, 2022 wakati akiongea na wanafunzi, walimu na uongozi wa shule katika ziara ya kukagua maendeleo ya uanzishwaji wa kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Kitutu iliyopo Halmashauri ya Wilaya Karagwe mkoani Kagera.

Amesema, mchakato wa usajili na uanzishwaji wa kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Kituntu ulianza tangu mwaka 2015 ikilenga kuanzisha tahasusi za HGL na CBG.
Aidha, Waziri Bashungwa ameahidi kumaliza changamoto ya upungufu wa walimu wa sayansi, hisabati na sanaa katika shule hiyo wakati Rais atakapotoa kibali cha ajira za walimu 7,000 zinazosubiriwa, hatua itakayoenda sambamba na kufanyia kazi changamoto ya nyumba za walimu.
Pia, amemuelekeza Mkurungenzi wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe kushughulikia changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo katika shule hiyo kwa kutoa kipaumbele kupitia fedha za ndani ya Halmashauri ya Wilaya Karagwe.

Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kituntu, Mwalimu Muganyizi Katatumba amesema kuwa, kiu ya wananchi wa Kata ya Kituntu na wilaya kwa ujumla ni shule yao kuwa na kidato cha tano na sita maana wamejitoa kuchangia michango yao kwa ajili ya kuongeza vyumba vya madarasa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news