Puma Energy Tanzania kuingiza sokoni gesi ya majumbani (LPG),yatoa tuzo

*Utekelezaji kuanza mwaka huu, kuongeza mtandao wa vituo vya mafuta nchini

NA GODFREY NNKO

KAMPUNI ya mafuta ya Puma Energy Tanzania inatarajia kuzindua bidhaa mpya ya gesi ya majumbani (Liquefied Petroleum Gas-LPG) ikiwa ni sehemu ya mipango yake ya kuhakikisha Watanzania wanaendelea kupata bidhaa bora wanazobuni kila wakati.
Uzinduzi wa gesi hiyo ambayo huwa inahifadhiwa ikiwa katika hali ya kimiminika kwenye mitungi ya ujazo tofauti huku ikiwa katika mgandamizo unatarajiwa kufanyika ndani ya mwaka huu, ambapo itawafikia watumiaji wote kupitia vituo vya Puma vilivyosambaa maeneo mengi nchini.

Hayo yamesemwa usiku wa Machi 24,2022 na Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Bw.Dominic Dhanah wakati akiwahutubia mawakala, wafanyakazi na wageni wengine waalikwa katika hafla maalum iliyofanyika Ukumbi wa Golden Jubilee jijini Dar es Salaam.

Hafla hiyo ililenga kutambua juhudi za mawakala na wafanyakazi katika vituo mbalimbali vya mafuta ya Puma vilivyopo hapa nchini ambapo walitunukiwa vyeti, tuzo na fedha taslimu kutokana na kazi ambazo wamekuwa wakizifanya, hivyo kuifanya kampuni hiyo kuendelea kuwa kinara katika utoaji wa huduma bora ya mafuta na vilainishi nchini.

"Tunayo furaha kujumuika na mawakala wote wa Puma Energy kwa mwaka 2022. Lengo sio tu kufurahia mafanikio yetu, lakini kutambua juhudi kubwa iliyowekwa kwenye maeneo mbalimbali nchini, kampuni yetu imeendelea kuongoza kwa ubunifu wa bidhaa mbalimbali ikiwemo kidigitali.
"Mwaka huu wa 2022 tunatarajia kuzindua bidhaa mpya ya gesi za majumbani maarufu kama LPG, bidhaa yetu hiyo wakati ukifika itapatikana katika vituo vyetu vyote vya mafuta hapa nchini, hivyo niwaahidi wateja na wadau wetu kuwa, watarajie bidhaa bora na zenye viwango kutoka Puma Energy Tanzania,"amesema.

Bw. Dhanah amesema kuwa, wanajivunia kuona kampuni yao ambayo ina ubia na Serikali inaendelea kuongoza Tanzania kwa kutoa bidhaa bora ikiwemo mafuta safi ambayo yameendelea kuwapa heshima kubwa na kujenga uaminifu mkubwa kwa wateja wao.

Amesema, kampuni hiyo imeendelea kupiga hatua kubwa, kwani tangu mwaka 2018 walikuwa na vituo 52 vya mafuta hapa nchini, lakini hadi sasa wamefikisha vituo vya mafuta 80 hapa nchini na wanatarajia ifikapo mwaka 2025 wawe wamefungua zaidi ya vituo 100 ili kuendelea kuwafikia wateja wengi zaidi.

Pia Bw.Dhanah ametoa raia kwa wafanyakazi, wadau wake na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19, kwani afya njema ndiyo nguzo ya kuimarisha uzalishaji na kutoa huduma bora kwa wateja wao.

"Kwa hiyo, tuendelee kuchukua tahadhari kwa sababu janga la Corona (UVIKO-19) tunaishi nalo.Tunaendelea kutoa pongezi na shukurani za kipekee kwa wadau wetu kwa kazi nzuri, tumekusanyika hapa kwa lengo la kutoa motisha kwenu ili muongeze bidii ya kutoa huduma bora zaidi huko mlipo.Lengo la tuzo hizi ni kutoa hamasa na kuwapa changamoto waendesha vituo hawa kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wetu kote nchini,"amesema.

Aidha, Bw.Dhanah amesema, hizo ni tuzo za pili kufanyika hapa Tanzania ambapo za kwanza zilifanyika mwaka 2020, lakini mwaka 2021 ilishindikana kutokana na changamoto za UVIKO-19.

Mgeni rasmi

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika hafla hiyo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Puma Energy Tanzania, Dkt. Selemani Majige amesema kuwa, ifikapo mwaka 2025 wanatarajia kuona angalau kampuni hiyo ina vituo zaidi ya 150 vya mafuta nchini ili kuwafikishia huduma za mafuta na vilainishi safi wateja wengi.

Dkt.Majige amesema kuwa, mpango huo unapaswa kwenda sambamba na ufunguaji wa vituo vidogo vidogo vya mafuta katika maeneo mbalimbali huko vijijini.

"Pia nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini na kunipa nafasi ya kuendelea kuiongoza Bodi ya Wakurugenzi ya Puma Energy Tanzania, nimuahidi kuwa, nitaendelea kushirikiana na wenzangu ili kuhakikisha kampuni hii inaongeza ubunifu na kutoa huduma bora.
"Huduma bora zitatuwezesha kuongeza wateja wengi ambao watachangia kukuza pato la kampuni na hatimaye kuwezesha gawio la Serikali kuongezeka, brand (chapa) ya Puma ina jina kubwa, na kila mteja anatamani kutumia bidhaa zetu, hivyo tutahakikisha tunalinda heshima ya brand hii na kutoa huduma bora ikiwemo mafuta safi katika vituo vyetu vyote nchini,"amesema.

Washindi

Kwa nyakati tofauti baadhi ya washindi wa tuzo, vyeti na fedha taslimu wameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, siri ya mafanikio yao ni ukarimu kwa wateja.

"Ukarimu ndiyo silaa pekee katika hii biashara ya mafuta, kadri unavyowapokea wateja kwa unyenyekevu na kuwasikiliza bila bughda utashangaa yule aliyekuja leo anamleta mwingine kesho, yule wa kesho naye anamleta mwingine.

"Hapo unaona unatengeneza 'connection' kubwa ya wateja, hivyo wanavyoambizana kuwa pale kituo fulani cha Puma wanatoa huduma bora, unajenga heshima, idadi ya wateja inaongezeka na unaendelea kuuza bidhaa kwa wingi, ukiuza bidhaa kwa wingi, hayo ndiyo matarajio ya kampuni na hitaji la kila mfanyabiashara. Hivyo, siri ya kipekee ni ukarimu hapo hamna cha uchawi wala sala,"amesema mmoja wa wafanyakazi wa kituo cha mafuta cha Puma mkoani Pwani katika mahojiano na DIRAMAKINI BLOG.

Puma ni nani?

Puma Energy Tanzania ni kampuni ya mafuta iliyosajiliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku ikiwa inamilikiwa kwa pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Msajili wa Hazina pamoja na Puma Investments Limited kwa hisa za asilimia 50 kila moja.

Hii ni kampuni ya Kimataifa ya kuuza mafuta inayojishughulisha na uhifadhi na usambazaji mkubwa wa bidhaa za petroli na dieseli.
Puma Energy Tanzania inatajwa kuwa ndiyo inayoongoza hapa nchini kwa kumiliki soko huku ikiwa na uwezo wa kuhifadhi mafuta zaidi ya lita milioni 94.

Kampuni hiyo inaendesha vituo 80 vya mafuta nchini huku ikitoa huduma ya mafuta ya ndege katika viwanja mbalimbali vya ndege.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news