Rais Dkt.Mwinyi aendelea kuhimiza amani, umoja na mshikamano

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewasisitiza wananchi kuendelea kuhubiri amani.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab (kulia kwa Rais) na (kushoto kwa Rais) aliyekaa katika kiti Sheikh Ahmad Mohamed Al Falasi, Kiongozi wa Taasisi ya Ahmad Mohamed Al Falasi,wakiitikia dua baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid Arafa Mombasa Wilaya ya Magharibi “B”Unguja leo Machi 25,2022.(Picha na Ikulu).

Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo katika salamu zake alizozitoa mara baada ya Sala ya Ijumaa huko katika Masjid Arafa, Mombasa Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema kwamba wakati wote yeye atasimama katika upande wa kuhubiri amani na kueleza kwamba wananchi wote wanadhima ya kuhakikisha nchi inakuwa salama.

Alieleza kwamba, hivi karibuni kumejitokeza baadhi ya watu kuanza kutoa maneno ya kuashiria kuvunja amani hivyo, aliwataka wananchi kuendelea kukumbushana umuhimu wa kuhubiri amani.

Amewataka wananchi wale wote wanaoguswa na maneno hayo kuwa na subira na kuwataka wale wanaoendeleza maneno hayo kutofanya hivyo kwani hawajengi na wala hawaitakii mema nchi hii.

Alhaj Dkt. Mwinyi amesisitiza amani kama inavyoelezwa katika Kur-an kwenye na kunukuu sura ya 25 Suratul Furkaan aya ya 63 na kueleza kwamba yeye anachotaka ni salama.

Amesema kwamba yeye ataendelea kusimama upande wa kuhubiri amani na kuhakikisha anakuwa mstari wa mbele ili amani iendelee kudumu nchini.

Amesema kwamba, umoja, mshikamano na amani katika nchi ni jambo la kuzungumzwa wakati wote kutokana na umuhimu wake katika maisha na maendeleo ya jamii.

“Mkisikia kuna vita katika nchi havianzi kwa bunduki huanza kwa maneno hivyo, ni wajibu wetu kama wananchi wanaoitakia mema nchi hii kuednelea kukumbushana kuhubiri amani na kuachana na maneno yenye kuweza kuvunja amani na kuleta machafuko,”alisisitiza Alhaj Dkt.Mwinyi.

Ameeleza kwamba watu wanaochafua nchi mara nyingi huwa makundi matatu ambayo ni wanasiasa, viongozi wa dini na waandishi wa habari na kueeleza kwamba machafuko ya nchi nyingi huanza kwa maneno na baadae kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Alhaj Dkt. Mwinyi ameeleza kufarajika kwake kwa msikiti huo kulenga makundi yote ya jamii ili kuwasaidia na kutimiza mambo ambayo misikiti inafanya na kuomba kuwa sehemu ya kusaidia kituo hicho katika ujenzi huo.

Alilipokea ombi la ujenzi wa kituo hicho na kuwataka wananchi wa eneo hilo kuwa wastahamilivu wakati ujenzi huo ukiendelea kutokana na usalama wao kwani eneo hilo litazungushwa mabati.

Alhaj Dkt. Mwinyi, alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Sheikh Ahmad Mohamed Al Falasi kwa misaada yake mbali mbali anayoitoa kwa jamii hapa Zanzibar.

Akitoa hotuba ya Sala ya Ijumaa, Imamu wa Masjid Arafa, Sheikh Ali Yunus alisisitiza haja ya kuendeleza umoja na mshikamano sambamba na kuwa na subira.

Sheikh Ali Yunus alisisitiza haja ya Waislamu kusaidiaana katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan unaokuja kwani waumini wote hawako sawa.

Mapema Profesa Hamed Rashid Hikmany akitoa maombi kwa Rais kwa niaba ya msikiti huo alisema kuwa msikiti wao umekuwa ni kituo cha maendeleo ya shughuli za kidini na kijamii ambapo umekuwa ukilenga kwenye kuendeleza maisha ya watu, kiroho na kiuchumi.

Amesema kuwa, dhamira yao ni kusaidia watu wanaozunguka msikiti huo ili waweze kuishi katika hali ya kuwa na kiwango cha juu cha imani ya kidini kama ilivyoanishwa kwenye Kur-an Tukufu na mfumo wa Mtume Muhammad (S.A.W) na kumuomba Rais ashirikiane nao katika kutimiza malengo yao ili wapate matunda endelevu.

Profesa Hikmany alieleza kwamba ili waweze kutimiza dhamira yao, msikiti huo umeasisi miradi mitatu muhimu inayowiana ajenda ya maendeleo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Uchumi wa Buluu.

Amesema kuwa, msikiti huo una Umoja wa Vijana ambao moja ya mafanikio yao ni kufanya kazi nao ambao awali walikuwa wamejiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya na kufanikiwa kuwabadilisha baadhi yao na kuwa wananchi wema wanaojitambua na wenye mwelekeo wa kidini.

Pia, alieleza kuwa msikiti huo una programu inayoendelea kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti ya kupima na kutoa ushauri nasaha kwa wanajamii kuhusu Ukimwi pamoja na kuchunguza maradhi ya sukari na shindikizo la damu ambapo pia, unafanya utafiti kwa wanawake, wasichana, wazee, mayatima, wajane na watu wenye mahitaji maalum ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika masuala ya familia, jamii na maendeleo ya taifa.

Alieleza azma ya msikiti huo kuanzisha kituo kitakachojumuisha harakati zote za kidini na kimaendeleo ya jamii, kikilenga masuala ya afya, vijana, wanawake na makundi yote yanayoweza kuathirika na kutennga eneo la ujenzi ambalo liko karibu na msikiti wao.

Akiwa msikiti hapo Alhaj Dkt. Mwinyi aligawa misahafu kwa waumini wote waliofika msikiti hapo iliyotolewa na Ahmad Mohamed Al Falasy kutoka Falme za Kiarabu (UAE) ambaye nae aliungana na Alhaj Dkt.Mwinyi kusali pamoja na waumini wa msikiti huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news