Rais Dkt.Mwinyi: Wana CCM jibuni hoja kwa vitendo, si maneno

*Aupongeza Umoja wa Wazazi Tanzania kwa kusimama kidete katika kuitafsiri kwa vitendo kaulimbiu yake ya 'Uchungu wa Mwana Aujuae Mzazi'

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujibu hoja kwa vitendo badala ya maneno, kwani wana dhima kubwa ya kuendeleza amani iliyopo nchini.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Machi 26,2022 huko katika ukumbi wa CCM Amani Mkoa, katika uzinduzi wa Kongamano la Maadhimisho ya Wiki ya Umoja wa Wazazi Tanzania, ambalo kitaifa mwaka huu linafanyika hapa Zanzibar.

Katika maelezo yake, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kwamba, hivi karibuni wametokea baadhi ya watu kuanza maneno maneno juu yake na Serikali anayoiongoza na kusema kwamba ni vyema watu hao wakajibiwa kwa vitendo badala ya maneno.

Rais Dkt.Mwinyi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, aliwataka wanaCCM kuwa na subira huku Serikali anayoiongoza ikitekeleza majukumu yake ipasavyo sambamba na chama chao kikiendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025 kwa vitendo.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa, Serikali zote mbili zinathamini kazi nzuri inayofanywa na Umoja wa Wazazi Tanzania, kwani wakati wote wameonesha kuguswa na hatua za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuifuatilia na kutoa ushauri kila unapohitajika.


Pia jumuiya hiyo imekuwa ikiendeleza jukumu la kusimamia elimu na maadili kwa watoto, malezi na utamaduni wa Taifa kwa mujibu wa Sera na Ilani ya CCM kote Tanzania Bara na Zanzibar.

Ameupongeza Umoja wa Wazazi Tanzania kwa kusimama kidete katika kuitafsiri kwa vitendo kaulimbiu yake ya “Uchungu wa Mwana Aujuae Mzazi”, kwa kuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na Serikali zote mbili katika mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa watoto na wanawake pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.

“Kwa namna mbalimbali mmeendelea kutukumbusha wazazi wajibu wetu wa kuwapa watoto wetu malezi bora yanayoendana na maadili yetu, silka na utamaduni wetu ili kukipa kizazi chetu urithi sahihi utaowajenga kuwa wazalendo na raia wema wa nchi hii,”amesema Rais Dkt.Mwinyi.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amepongeza kwa kuwepo mada inayohusiana na Uchumi wa Buluu na kutoa wito kwa washiriki wa Kongamano hilo kufuatilia kwa umakini taaluma itakayotolewa na wataalamu kuhusu Uchumi wa Buluu ili wakitoka hapo wakawe walimu wa wananchi wengine waliokosa fursa ya kuwepo katika kongamano hilo.

Pia, alisisitiza katika kufanikisha malengo ya kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni lazima kuendeleza utaratibu wa kufanya ziara katika ngazi za chini walioko wanachama wao ili kuweza kuzifahamu changamoto zao na hatimae kuzipatia ufumbuzi.

Ametoa wito kwa wananchi kushiriki katika zoezi la sensa wakati utakapofika kwa kutoa ushirikiano na kuwapa taarifa sahihi maofisa watakaohusika na zoezi hilo.

Nae Mwenyekiti wa Wazazi Taifa, Edmund Mndolwa alitoa shukurani kwa Rais Dkt.Mwinyi kwa juhudi kubwa anazozichukua katika kuiletea maendeleo Zanzibar na kuahidi kwamba Umoja wa Wazazi utaendelea kumuunga mkono.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdalla Juma Mabodi ametoa pongezi kwa jumuiya hiyo kwa kufanya kongamano hilo ambalo lina umuhimu mkubwa katika kukiendeleza chama hicho huku akisisitiza suala zima la kuendeleza amani nchini.

Katika kongamano hilo mada mbalimbali zimetolewa ikiwemo Uchumi wa Buluu, historia ya Umoja wa Wazazi pamoja na udhalilishaji wa kijinsia.

Sambamba na hayo, Rais Dkt.Mwinyi alikabidhiwa zawadi yake na jumuiya hiyo pamoja na kukabidhiwa zawadi ya Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambayo alipokea kwa niaba yake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news