Saudi Arabia yavutiwa kuwekeza katika Mwendokasi nchini

*Uwekezaji huo unalenga uendeshaji wa mabasi,teknolojia pamoja na mifumo kutokana na uzoefu wa miaka mingi

NA MWANDISHI MAALUM

WAWEKEZAJI kutoka nchini Saudi Arabia imeonesha nia ya kufanya uwekezaji mkubwa katika mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) nchini.
Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Mhe.Ally Mwadini (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) katika ukumbi wa Wakala Ubungo Maji jijini Dar es Salaam baada ya kikao baina ya wakala na wawekezaji kutoka Saudi Arabia, Machi 28, 2022.

Uwekezaji huo unalenga katika uendeshaji wa mabasi,teknolojia pamoja na mifumo kutokana na uzoefu wa miaka mingi walio nao katika sekta hiyo, lakini pia kutokana na Tanzania kuwa na mazingira mazuri na tulivu kwa ajili ya uwekezaji.

Akizungumza na Menejimenti ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka pamoja na wawakilishi wa makampuni ya uwekezaji kutoka Saudia Arabia, Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Mhe. Ally Mwadini amesema, ujumbe huo umeonesha nia ya kuja kuwekeza katika sekta ya usafirishaji hasa katika mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka kutokana na mazingira wezeshi yaliyopo Tanzania ambayo yanawahakikishia wawekezaji uhuru wa kuwekeza.

“Leo tumekuja kwa ajili ya kuona ni namna gani Saudi Arabia inaweza kushiriki katika mradi huu wa Mabasi Yaendayo Haraka maarufu kama mwendokasi, hii inatokana na nchi ya Saudi Arabia kuwa na uzoefu katika uendeshaji wa miradi kama hii, lakini pia kwa kuwa Tanzania ni nchi ya amani na utulivu na yenye watu wakarimu pamoja na mazingiza wezeshi yaliyopo katika uwekezaji,”amesema Balozi Mwadini.
Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Mhe.Ally Mwadini akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) katika Ukumbi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Ubungo Maji jijini Dar es Salaam baada ya kikao baina ya wakala na wawekezaji kutoka Saudi Arabia, Machi 28, 2022.

Amesema, Tanzania ina umuhimu mkubwa sana kibiashara na uwekezaji katika ukanda huu wa Afrika kwani imepakana na nchi nyingi ambazo hutegemea huduma na bidhaa zake kupitia hapa nchini suala ambalo linawafanya wawekezaji kuona fursa hiyo na kuvutiwa kuja kuwekeza.

“Nimeambatana na wawakilishi wa Kampuni ya Saudi Arabia Public Transport Company (SABTCO) pamoja na Taasisi ya Uwekezaji ambayo inahusika na kuwekeza nchini Saudi Arabia pamoja na nje ya nchi, lengo kubwa ni kuja kuona na kutathmini namna watakavyoweza kuja kujiunga na Tanzania katika kuendeleza sekta ya usafirishaji pamoja na sekta nyingine ambazo watavutiwa nazo,”amesema Balozi Mwadini.

Balozi Mwadini amesema , Saudi Arabia ni nchi iliyoendelea na yenye mahusiano mazuri na Tanzania hivyo wameamua kuja kuunga mkono Juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe.Samia Suluhu Hassan za kuwaletea Watanzania maendeleo.

Kwa upande wake mwakilishi wa Kampuni ya SABTCO, Bw.Hassan Abduljawad alisema wameona mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka ni eneo sahihi kwa wakati huu kutembelea na kuona namna wanavyoweza kuwekeza kwa kuwa kuna awamu sita za mradi huo katika Jiji la Dar es Salaam jambo ambalo linahitaji uwekezaji wa watu wengi na wa fedha nyingi.

“Sisi tuna uzoefu wa kuendesha miradi kama hii kwa miaka mingi tumeona kwa awamu zote za mradi hapa Tanzania tunawez na sisi kuja kuwekeza katika moja ya awamu ili tuweze kutoa mchango wetu na uzoefu wetu kwa ajili ya watanzania” amesema Bw.Abduljawad.

Ujio wa wawekezaji kutoka Saudi Arabia ni moja ya juhudi zilizotokana na ziara ya Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan katika nchi za Ulaya na Falme za kiarabu za kutafuta wawekezaji kwa ajili ya kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali hapa nchini.

Aidha, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimekuwa mstari wa mbele katika kutafsiri maono ya Rais Samia ya kutaka kuona Tanzania inayokua kiuchumi kupitia uwekezaji wenye tija kwa kuendelea kuratibu na kuleta wawekezaji katika sekta mbalimbali ili kutumia fursa nyingi zinazopatikana nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news