Steve Nyerere ashukia njiani kabla ya uamuzi wa BASATA

*Asema hana kinyongo na mtu yoyote, ameachia nafasi hiyo kwa roho safi

NA GODFREY NNKO

MSEMAJI wa Shirikisho la Muziki Tanzania (SMT), Steve Mengele maarufu kama Steve Nyerere ameamua kuachia nafasi hiyo.

Uamuzi huo unakuja ikiwa ni siku chache baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kubaini hali ya kutoelewana miongoni mwa wasanii wa muziki kuhusu uteuzi wa Steve Nyerere.

Kutokana na hali hiyo, BASATA walisema pande zote mbili zina hoja na hivi karibuni watalitolea majibu sakata hilo ambalo lilionekana kutawaliwa na vuta ni kuvute ikiwemo kurushiana vijembe mitandaoni.
Steve Nyerere ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo ya usemaji leo Machi 25,2022 kwenye ofisi za BASATA akisema kuna mambo mengi yenye tija ambayo Taifa inapaswa kuyashughulikia badala ya kuendeleza sakata la kuteuliwa kwake.

Amesema, ataendelea kuwepo kwenye maisha ya wasanii, kwani bado ana nafasi za uongozi sehemu mbalimbali na ataendelea kuendesha matamasha yanayowahusu wasanii.

Pia amesema kwamba, hana tatizo na msanii ambaye pia ni Mbunge wa Muheza mkoani Tanga, Mheshimiwa Hamis Mwinjuma maarufu kama MwanaFA.

"Hatuna tofauti na Mwana FA hata kidogo, alileta 'challenge' zake tukazipokea, akajibiwa kwa 'challenge', sina tofauti nae, ni kijana wangu, nimemzidi mpaka dhambi, nataka nimuombe popote alipo isitoke dhana ya kumchukia mtu yeyote hapa, kwenye mpira tuna Simba na Yanga, lakini tukikutana baa tunakunywa pamoja, tunazikana pamoja ndio mfumo wa sanaa duniani kote sio kinyongo,"amesema Steve Nyerere.

Machi 23, 2022 Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, Matiko Mniko muda mfupi baada ya BASATA kumaliza kikao na viongozi wa shirikisho hilo kilichoketi kwa saa tano jijini Dar es Salaam alisema, waliziita pande zote mbili za uongozi na wakawasikiliza na kugundua kila upande una hoja na BASATA watatoa uamuzi wa jambo hilo hivi karibuni.

"Moja ya majukumu tuliyopewa BASATA ni kushughulikia pia migogoro inapotokea kwa wasanii nasi tulichofanya leo ni moja ya jukumu hilo kwa kuwaita na kuwasikiliza kila upande na hoja zao,"alisema Mniko.

Alisema kuwa, baada ya kumaliza kupitia hoja zao baraza hilo litatoa majibu mapema iwezekanavyo katika kumaliza mgogoro huo.

"Lengo sio kuona wasanii wanafarakana bali tunataka wafanye kazi kwa kushirikiana na kuipeleka sanaa mbele," alisisitiza Katibu huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news