Uwekezaji mkubwa wabisha hodi Kwala, Dkt.Kijaji atoa rai kwa wananchi

*Manufaa ya uwekezaji huo ni uhakika wa soko la malighafi ambapo mikataba iloyosainiwa ni ya viwanda vya kuchakata mazao

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WATANZANIA wametakiwa kutumia eneo la uwekezaji la Kwala wilayani Kibaha mkoani Pwani kwa ajili ya soko la kuuza malighafi mbalimbali baada ya kuingia mikataba ya uwekezaji wa ardhi kwa ajili ya kujenga viwanda.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara,Mheshimiwa Dkt.Ashatu Kijaji wakati wa hafla ya kukabidhi kiwanja namba 1 kitalu B kwenye eneo hilo la Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kwa mwekezaji wa kampuni ya Sino Tan (Kibaha Industrial Park Ltd) kwa ajili ya Kongani ya viwanda.
Dkt.Kijaji amewataka wananchi kutumia fursa zilizopo kwenye eneo la uwekezaji la Kwala wilayani Kibaha mkoani Pwani baada ya kuingia mikataba ya uwekezaji wa ardhi kwa wawekezaji mbalimbali kwenye eneo lenye ukubwa wa hekari 2,500.

Amesema kuwa, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimevunja rekodi kwa kusajili miradi 266 katika kipindi cha mwaka mmoja ikiwa ni usajili wa miradi mingi ya uwekezaji kwa kipindi kifupi cha mwaka mmoja.

Pia amebainisha kuwa,wingi wa miradi hiyo haijawahi kusajiliwa kwa muda mfupi ndani ya mwaka mmoja tangu nchi imepata Uhuru ambapo uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umefanya hayo ndani ya mwaka mmoja ambapo mradi huo wa wawekezaji toka nchi ya China ni ushuhuda wa mkakati wa Taifa wa ajenda ya viwanda kufikia pato la kati ifikapo mwaka 2025.

"Manufaa ya uwekezaji huu ni uhakika wa soko la malighafi ambapo mikataba iloyosainiwa ni ya viwanda vya kuchakata mazao ambapo Watanzania wanakwenda kunufaika na soko, kwani kwa sasa liko hapa tuanze nyumbani tutambue umuhimu wa mradi hata kujifunza Kichina, madiwani wawape elimu akinamama na watoto juu ya umuhimu wa kutumia eneo hilo la uwekezaji la Kwala,"amesema Dkt.Kijaji.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara, Profesa Tobias Kaiyarara amesema kuwa, upatikanaji wa ardhi ni jambo kubwa kuliko kitu chochote ndiyo maana sheria zinabadilishwa ili ardhi ipatikane haraka ili mradi ufanyike kwa haraka.

Kwa upande wake Mwakilishi wa wa Sino Tan Kibaha, Jensen Huang amesema kuwa, mradi huo umegharimu dola za Marekani milioni 150 ikiwa ni gharama za upatikanaji ardhi, miundombinu na vifaa na utatoa ajira 100,000 za moja kwa moja.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Abubakar Kunenge amesema mkoa una viwanda 1,453 na 87 viwanda vikubwa na wanaendelea kutumia mikakati mbalimbali ya kuvutia wawekezaji wawekeze viwanda vikubwa na vya kati viwe vikubwa na Rais aliahidi kipaumbele kwa kutoa nishati ya umeme, gesi na miundombinu ya barabara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news