Waziri Bashungwa:Tushiriki kikamilifu zoezi la Anuani za Makazi

NA MWANDISHI WETU, OR- TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Innocent Bashungwa amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia kwa karibu zoezi la anuani za makazi kwenye maeneo yao ili ifanyike kwa ufanisi.
Waziri Bashungwa ameyasema hayo jijini Dodoma alipokuwa akifungua Mkutano wa 12 wa Umoja wa Maboresho ya Serikali za Mitaa baina ya Tanzania na Osaka (TOA) ambao viongozi hao ni wanachama wa umoja huo.

Amesema, kama walivyofanya vizuri kwenye ujenzi wa madarasa ni vyema wakasimamia na kutekeleza kwa ufanisi operesheni hiyo.

“Nyie ndio wasimamizi wakuu na tuna deadline kwa hiyo muendelee kusimamia kwa karibu. Pia upande wa ukusanyaji wa mapato muendelee kusimamia ipasavyo,”amesema.

Aidha, amesema suala la kupatiwa mafunzo ya kujengewa uwezo wa utendaji kazi kwa mamlaka hizo ni muhimu kwa kuwa yanachangia ufanisi mahala pa kazi.

“Kupitia TOA ninaamini ni fursa muhimu ya kufanikisha hili niwaalike mje ofisini kwangu baada ya uchaguzi kufanyika ili tupitie mpango kazi uliopo na yale ambayo tunafikiria katika kuimarisha utendaji kazi wa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kujengeana uwezo,”amesema.
Pia amesema, kuna idara ambazo zinahitaji kujengewa uwezo hasa zile ambazo ni muhimu kwenye halmashauri ikiwemo rasilimali watu, mipango, manunuzi, waweka hazina na watendaji wa kata na vijiji.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo, Erick Mapunda, amesema katika kujengewa uwezo viongozi hao, wataalamu mbalimbali watatoa mada ambazo zitakuwa chachu kwenye masuala ya kiutendaji.

“Lengo ni kujiimarisha zaidi na kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma kwa wananchi, kuna mada za ukusanyaji wa mapato, sensa ya watu na makazi, maadili na itifaki, mapambano dhidi ya rushwa, majanga, masuala ya lishe na matumizi bora ya ardhi,”amesema.

Post a Comment

0 Comments