Mtwara wakabiliwa na changamoto ya matumizi hafifu ya mbolea

*TFRA yapongezwa kwa uhamasishaji matumizi sahihi ya mbolea

NA NURU MWASAMPETA 

IMEELEZWA kwamba Mkoa wa Mtwara umekuwa ukitumia wastani wa tani 997 za mbolea ambacho ni kiasi kidogo ukilinganisha na mahitaji ya lengo la mkoa la kutumia kiasi cha tani 2,000 kwa mwaka.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dunstan Kyobya akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti mbele ya umati uliohudhuria katika Maadhimisho ya Siku ya Mkulima yaliyofanyika Aprili 13, 2022 katika Kijiji cha Lilido Kata ya Kitere Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara.

Hivyo uwepo wa mashamba darasa ya kuhamasisha matumizi ya mbolea yanayosimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) yamekuja wakati muafaka kwani mkoa upo katika utekelezaji wa mkakati wake wa kuongeza uzalishaji na tija.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dunstan Kyoba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti alipokuwa akitoa hotuba wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mkulima yaliyofanyika katika Kijiji cha Lilido Kata ya Kitere mkoani Mtwara tarehe 13 Aprili, 2022.
Dunstan D. Kyobya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara akizungumza na wananchi (hawapo pichani) wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mkulima yaliyofanyika katika Kijiji cha Lilido Mkoani Mtwara tarehe 13 Aprili, 2022.

Kyobya alisema, baada ya kujionea utofauti wa shamba la Mpunga uliopandwa kwa kutumia mbolea na ule usiotumia mbolea katika mashamba darasa yaliyopo kwenye Skimu ya Kitere amewataka wakulima kufanya kwa vitendo kwenye mashamba yao yale waliyojifunza kupitia mashamba darasa hayo ili kuongeza tija, uzalishaji na kipato.
Wananchi waliohudhuria katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Mkulima wakitanguliwa na Kikundi cha Wakulima cha Tupendane.

“Na ni kweli, nimetembelea lile shamba kwenye Skimu ya Kitere niwapongeze sana TFRA na Kikundi cha Wakulima Tupendane, mmefanya kazi kubwa sana hongereni sana, nimeambiwa kile kipande kimoja cha shamba darasa kilichopandwa kwa mbolea unaweza ukatoa gunia 25 ukienda unaona kabisa lakini lile ambalo halikupandwa kwa mbolea unaona kuwa hakuna kitu kabisa,”Kyobya alikazia.

Pamoja na hayo, Kyobya aliwaasa wakulima kuepuka kununua mbolea na pembejeo za kilimo kwenye maduka yasiyo rasmi kwani ikitokea bidhaa iliyonunuliwa ni feki itakuwa ngumu kwa wataalamu kumpata muuzaji na kumchukulia hatua kwa mujibu wa sheria.
Claudia Kita, Mkuu wa Wilaya ya Masasi akisalimia umati uliofurika kuadhimisha Siku ya Mkulima katika Halmashauri ya Mtwara, Kata ya Kitere tarehe 13 Aprili, 2022.

Pia, aliwataka wakulima kuepuka kununua mbolea za kupima kutokana na mbolea hizo kupoteza ubora na hivyo kusababisha hasara na kuwataka wanunue zile zilizofungwa vizuri kama inavyoelekezwa na wataalamu wa kilimo na mwisho wa siku wapate matokeo chanya.

Kufuatia changamoto ya upatikanaji wa maji katika Skimu ya Kitere, Kyobya aliielekeza Halmashauri ya Mtwara wakishirikiana na Mamlaka ya Maji Safi Mtwara kuhakikisha maji yanapatikana muda wote katika skimu hiyo ili kuwaondolea wakulima changamoto ya upatikanaji wa maji kama walivyoomba katika risala yao.
Alhaji Kundya, Mkuu wa Wilaya ya Newala akizungumza na wananchi wa Kitere.

Akitoa maelekezo kwa TFRA Kyobya aliitaka mamlaka kuhakikisha inawasimamia kikamilifu wafanyabiashara wa mbolea na kuhakikisha mkoa wa Mtwara unakuwa na wauzaji na wasambazaji wenye sifa pamoja na kudhibiti bei za mbolea ili kuwawezesha wakulima kumudu bei ya mbolea na kuitumia kama walivyoelimishwa.

Aliwaagiza maafisa ugani kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na kusimamia usambazaji wake kwa kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo za kilimo kwenye maduka rasmi na wanapewa risiti kuthibitisha manunuzi yao.

“Maafisa ugani mnapaswa kuwa karibu na wakulima ili kuwawezesha kufuata kanuni zote za kilimo ikiwa ni pamoja na kuchagua shamba, kuandaa shamba kwa wakati, kupanda kwa kutumia mbolea sahihi ya kupandia na kwa wakati, kuweka mbolea ya kukuzia na kupalilia kwa wakati.
Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Mariam Chaurembo akizungumza na wananchi wa Kata ya Kitere.
Alisema shamba likifuata kanuni zote za kilimo huwa na matokeo mazuri na hivyo kuongeza tija na mapato kwa mkulima, halmashauri na taifa kwa ujumla.

Akihitimisha hotuba yake, Kyobya alisema mfumo uliotumiwa na TFRA wa kutumia mashamba darasa ni mzuri kwani unawafikia wadau wengi kwa muda mfupi na kukiri mkoa wa Mtwara umedhamiria kuongeza uzalishaji wa mazao ya mpunga na mahindi hivyo utakuwa karibu na wakulima wakati wote wa kilimo kwa lengo la kuwaongoza katika kufikia tija.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephani Ngailo aliwatoa hofu wananchi na wakulima nchini kuwa matumizi ya mbolea yanaharibu udongo na kuwataka wazingatie matumizi sahihi ya mbolea kwa hivyo hakutakuwa na athari yeyote kwenye afya ya udongo.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania akiwasilisha taarifa ya namna mpango wa uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima wa Mtwara ulivyotekelezwa mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Gaguti aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Danstun Kyobya wakati wa maadhimisho ya siku ya Mkulima mkoani humo.

Alisema, TFRA itaendelea kushirikiana na sekretarieti za mikoa na halmashauri kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza tija katika uzalishaji.

Aidha, aliwashukuru wadau wote waliowezesha kufanikishwa kwa shughuli ya uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea ikiwa ni pamoja na uongozi wa Mkoa wa mtwara, wakurugenzi wa halmashauri zilizopo katika mkoa huo na maafisa kilimo husika, makampuni ya usambazaji wa mbolea hususan ETG, Premium, OCP pamoja na Yara kwa kutoa mbolea kwa vikundi vya wakulima na kuwezesha wakulima kujifunza kwa vitendo.
Dunstan D. Kyobya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara (wa nne kutoka kulia) akieleza alichojifunza mara baada ya kukagua mashamba darasa ilipo scheme ya mpunga ya Kitere kijiji cha Lilido Mkoani Mtwara tarehe 13 Aprili, 2022. Wa pili kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news