'Andikeni habari zinazochochea kasi ya ukuaji wa maendeleo mkoani Mara'

NA FRESHA KINASA

WAANDISHI wa habari mkoani Mara wametakiwa kuendelea kuandika habari zinazochochea maendeleo ya mkoa huo na wasiogope kuripoti maovu yanapobainika kwa kuzingatia sheria na Maadili ya kazi yao kwa masilahi mapana ya jamii na taifa ujumla.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mara,Langael Akyoo akizungumza katika mkutano

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 16, 2022 na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Langael Akyoo wakati akifungua Maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya habari mkoani humo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mativila Beach Uliopo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari nchini yaliadhimishwa Mei 3, 2022 jijini Arusha na kuhudhuriwa na Mheshimwa Samia Sulubu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo waandishi mbalimbali kutoka Tanzania na nchi mbalimbali za Afrika walihudhuria.

Akyoo amesema kuwa, wanahabari wana wajibu wa kuendelea kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, taratibu na maadili ya kazi yao bila kuogopa iwapo habari husika ina masilahi mapana kwa jamii na taifa hivyo wasiogope kutekeleza wajibu wao.

"Tasnia ya habari ni muhimu sana katika kuchochea maendeleo. Fikirieni kwamba ikitokea siku moja redio, magazeti televisheni zisiporipoti chochote kwa siku hata moja itakuwaje? Ukweli ni kwamba kutakuwa na giza. Ni Shirika gani, taasisi gani, ambayo itafanya kazi ikiwa na lengo la kujulikana ama kutambulika majukumu yake itafanikiwa kikamilifu isipohusisha wanahabari?. amehoji Akyoo na kusema.

"Endeleeni kuandika habari kwa ajili ya kuutangaza Mkoa wa Mara na kazi mbalimbali zinazofanywa na Serikali zizidi kujulikana zaidi kwa wananchi. Lakini pia msiache kusema pale mnapoona mambo hayaendi hii itaongeza uwajibikaji, toeni habari yoyote kama inamhusu mtu au taasisi bila kuogopa iwapo habari hiyo inazingatia maadili na sheria za nchi na kwamba haitakiuka sheria. na misingi iliyowekwa,"amesema Akyoo.
Aidha, Akyoo amesema kuwa, Chama Cha Mapinduzi mkoani Mara (CCM) kitaendelea kuwapa ushirikiano waandishi wote wa habari mkoani humo katika kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa ufanisi huku akiwahimiza kuendelea na umoja miongoni mwao pamoja na kushirikiana na wadau wote mkoani humo.

Katika hatua nyingine, amevitaka vyombo vya usalama mkoani humo kuhakikisha vinawalinda waandishi wa habari waendelee kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na iwapo watapata vitisho vyovyote wasisite kutoa taarifa haraka iwezekanavyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha DP mkoani humo, Chrisant Nyakitita akizungumza katika maadhimisho hayo, amewaomba waandishi wa habari kutangaza fursa mbambali za kiuchumi zinazopatikana mkoani Mara na kuandika makala mbalimbali na chambuzi kwa manufaa ya jamii.

"Waandishi wafike maeneo mbalimbali ya mkoa hasa Vijijini na kuona fursa zilizoko maeneo hayo wazungumze na wananchi kwa upana kujua fursa hizo zina manufaa gani kwa maendeleo yao waziangazie kwa kina na kuzitangaza, badala ya kusubiria kuambatana na viongozi tu ndipo waripoti,"amesema Nyakitita.
Boniphace Ndengo ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Kilimo na Wenyeviwanda Mkoa wa Mara (TCCIA) amesema, waandishi wa habari wanapaswa kuwa wabunifu katika kukusanya taarifa, kuandaa taarifa na kuripoti kwa ufanisi kwa kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwa wakati wa sasa sambamba na kujiendeleza kitaaluma wafike mbali zaidi.

Katika maadhimisho hayo, mada mbalimbali zimejadiliwa kwa maslahi mapana ya wanahabari mkoani humo ikiwemo kauli mbiu isemayo ya maadhimisho hayo isemayo "Uandishi wa Habari na Changamoto za Kidigitali".

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news