DC Ilemela akagua mradi wa maji Kiseke, azungumza na wananchi asisitiza uwajibikaji

NA SAMIR SALUM

MKUU wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Hassan Masalla ametembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa maji uliopo katika Kata ya Kiseke pamoja na kuzungumza na wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masalla (wa pili kulia) akiwa juu ya tenki la maji wakati akikagua mradi wa maji uliopo Kata ya Kiseke Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela leo Mei 9, 2022. (Picha na Langolahabari).

Masalla ametembelea mradi huo leo Mei 9, 2022 ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi katika kata zilizopo wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo, DC Masalla amesema kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha inamtua mama ndoo kichwani kwa kutatua kero za maji na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi milioni 365 ili kutekeleza mradi huo.

“Mwaka jana nlifanya ziara katika kata hii na kero kubwa kutoka kwa wananchi ilikuwa ni ukosefu wa maji, namshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kutoa shilingi 365, pia nimshukuru Mbunge wetu Dkt.Angeline Mabula kwa kufikisha kero hii,”amesema DC Masalla.
Muonekano wa tenki la maji ambao ni mradi wa maji uliopo katika Kata ya Kiseke mkoani Mwanza.

Amesema kuwa, Julai 17, 2022 Mwenge wa Uhuru utatembelea mradi huo hivyo amewataka Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili kufikia Mei 30, 2022 wananchi waanze kupata huduma ya maji.

Kwa upande wake Mhandisi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Yustas Karokora amesema kuwa, mradi huo unagharimu Shilingi Milioni 365 huku hadi sasa ukiwa umefikia asilimia 88 ukitarajiwa kukamilika mwishoni Mwa mwezi May 2022 na utahudumia wananchi zaidi ya 3500 wa Kata ya Kiseke.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masalla akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Kabambo leo Mei 9, 2022 alipofanya ziara yake katika Kata ya Kiseke Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

Aidha, Mkuu huyo wa wilaya amefanya mkutano wa hadhara katika Kata ya Kiseke kwa lengo la kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi wa kata hiyo ambapo wamelalamikia kutosomewa taarifa ya mapato na matumizi ya mradi wa maji ya matenki ya plastiki yaliyopo katika mtaa wa hali inayowapa mashaka.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masalla akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Kabambo leo Mei 9, 2022 alipofanya ziara yake katika Kata ya Kiseke Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Mhandisi Modest Apolinary akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Kabambo leo Mei 9, 2022 wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela katika Kata ya Kiseke Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

Akizungumzia kero hiyo mmoja ya wananchi Mtaa wa Kabambo, Lukombwe Ngariba amesema kuwa tangia mradi wa wa maji ya matenki ya plastiki uanzishwe hawajawahi kusomewa taarifa ya mapato na matumizi hali iliyopelekea kutoelewana baina ya wananchi na viongozi.

“Tangu huu mradi uwepo hatujawahi kusomewa taarifa ya mapato na matumizi hata siku moja, kila tukikaa vikao tunapigwa tarehe mara kamati iliyoteuliwa inasema haijajiandaa sasa tunabaki kulaumiana na viongozi,”amesema Ngariba.
Wananchi wa Mtaa wa Kabambo wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masalla leo Mei 9, 2022 wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela katika Kata ya Kiseke Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

Kutokana na changamoto hiyo, DC Massala amewataka viongozi wa Kata ya Kiseke na Kamati iliyokabidhiwa mradi huo kupeleka nakala ya taarifa ya mapato na matumizi ofisini kwake na kuhakikisha Mei 11, 2022 wanafanya mkutano wa hadhara na kuwasomea wananchi taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news