KUMBUKIZI YA MWALIMU 1:Utu alithaminisha, Tanzania na dunia

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

HIVI karibuni Watanzania walifanya maadhimisho ya kuenzi miaka 100 ya kuzaliwa kwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kilele cha maadhimisho kilifanyika kijijini kwake Butiama mkoani Mara, eneo alipozaliwa miaka 100 iliyopita na kuzikwa miongo miwili iliyopita.

Alizaliwa Aprili 13,1922 Butiama Tanganyika wakati huo ambapo kwa sasa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,alikufa akiwa na miaka 77 na kuzikwa katika Kijiji cha Mwitongo Butiama.

Wageni mbalimbali walihudhuria maadhimisho hayo yaliyokuwa na lengo la kuenzi mchango wa kiongozi huyo wa kitaifa ambaye utendaji wake na sifa zake zilitambulika ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Pia ndiye aliyefanikisha Uhuru wa Tanganyika 1961 dhidi ya ukoloni wa Mwingereza bila kumwaga damu, jambo alilosifiwa kama mmoja wa viongozi waliokuwa wana imani ya kijamaa.

Pande zote za Ulaya na Afrika sifa zake zilifana baada ya kuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania ikiwa ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Aidha, hivi karibuni katika Kongamano la Kumbukizi ya Miaka 100 ya Kuzaliwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere katika mtazamo wa kiuchumi chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na uchambuzi wa vitabu lililofanyika kwenye ukumbi wa benki hiyo jijini Dar es Salaam, wasomi walimueleza Hayati Baba wa Taifa kuwa ni miongoni mwa watu ambao walikirimiwa vipawa vya kipekee katika uongozi.

Katika kongamano hilo, ilielezwa kuwa,ni vigumu kutenganisha historia ya Tanzania na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwani kabla na baada ya Uhuru alifanya mambo mengi ambayo yamebaki katika kumbukizi muhimu kwa Watanzania na mataifa ya kigeni.

Mbali na hayo falsafa za Mwalimu Nyerere za Utu, Usawa, Haki na Ujamaa zimetajwa kuwa ni nyezo muhimu za kuimarisha na kujenga amani hapa nchini na Bara la Afrika na zisipozingatiwa kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Ili kujifunza zaidi, mshairi wa kisasa Bw.Lwaga Mwambande anakukaribisha kujifunza mambo muhimu kupitia ushairi ufuatao hapa chini;

>Huwezi kutenganisha, Nyerere na Tanzania,
Alifanya ya maisha, kabla ya Tanzania,
Tena lituimarisha, ile huru Tanzania,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

>Mengi ya kufurahisha, yale alitufanyia,
Wakoloni kufurusha, mikono twamwinulia,
Hakusema yameisha, lizidi tutumikia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

>Falsafa lianzisha, bado tunazitumia,
Kwani nyingi za maisha, haziwezi kuishia,
Ari hizo zaamsha, Tanzania na dunia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

>Umoja liimarisha, Kiswahili kutumia,
Nchi aliunganisha, kote kimetufikia,
Hatuna jitambulisha, kikabila nakwambia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

>Utu alithaminisha, Tanzania na dunia,
Lifanya kuimarisha, hizi zetu jumuia,
Mataifa kuwezesha, uhuru kuufikia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

>Usawa litumezesha, sisi wote Tanzania,
Unyang’au likomesha, hakutaka kusikia,
Pazuri litufikisha, kweli tunafurahia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

>Mwalimu alifundisha, Ujamaa Tanzania,
Na pia ilimkosha, tujitegemee pia,
Hapo angetufikisha, tungetesa Tanzania,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

>Nyenzo lizothaminisha, ndizo zinasaidia,
Amani kuidumisha, Afrika na dunia,
Wale tunu zawakosha, makwao wametulia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

>Wasomi watukumbusha, hapa tulipofikia,
Kama ngekuwa maisha, ngefika miaka mia,
Yalitoweka maisha, mema twayakumbukia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

>Kile kinafurahisha, vile wametuambia,
Njia hatujafupisha, hapa kwetu Tanzania,
Ya Mwalimu twafwatisha, amani twajivunia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news