Leteni maoni ya maboresho Sheria ya Ununuzi wa Umma-WFM

NA SAIDINA MSANGI-WFM

WIZARA ya Fedha na Mipango imetoa wito kwa wadau wa sekta ya ununuzi wa umma nchini kutoa mawazo kuwezesha maboresho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ili kuleta tija kwa Serikali.
Wadau wa ununuzi wa umma na ugavi nchini wakifuatilia mawasilisho katika kongamano la Wiki ya ununuzi wa umma, lililolenga kutoa fursa kwa washiriki hao kubadilishana mawazo na uzoefu pamoja na kuonesha huduma zao, jijini Arusha.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM).

Rai hiyo imetolewa na Kamishna wa Idara ya Sera ya Ununuzi wa Umma Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Frederick Mwakibinga, wakati akitoa elimu kuhusu sera, Sheria, kanuni na miongozo ya ununuzi wa umma kwa washiriki waliotembelea banda la wizara hiyo, katika wiki ya ununuzi wa umma, jijini Arusha.

Alisema kuwa kuna Sheria ya ununuzi wa umma sura 410 na kanuni zake ambayo kwa mara ya mwisho ilipitiwa mwaka 2013 na kanuni zake kutoka mwaka 2016.
Kamishna wa Idara ya Sera ya Ununuzi wa Umma Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Frederick Mwakibinga, akitoa elimu kuhusu sera, sheria, kanuni na miongozo ya ununuzi wa umma kwa washiriki waliotembelea banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Wiki ya ununuzi wa umma, jijini Arusha.

‘’Tunaendelea kukusanya maoni kutoka makundi mbalimbali na watu wote ambao wanadhani nini kifanyike ili Sheria iweze kutekelezeka na iweze kunufaisha nchi, hili ni jukumu letu kuhakikisha kuwa eneo la ununuzi wa umma lina sera, Sheria, kanuni na miongozo inayokuwa na tija kwa Taifa’’ alisema Dkt. Mwakibinga.

Alisema Sheria ya ununuzi wa umma inalinda maslahi ya Taifa kwani inawapa wananchi pamoja na wafadhili imani na Serikali katika matumizi ya fedha hivyo matumizi ya sheria hayapaswi kuingiliwa na mashinikizo.

Dkt. Mwakibinga alisisitiza maafisa manunuzi nchini kusimama katika sheria, kufanya kazi kwa nidhamu, kuheshimu taratibu za ununuzi na kuepuka kukiuka matumizi ya sheria kutokana na shinikizo lolote na kuwasiliana na wizara endapo watakutana na changamoto ya shinikizo la aina yoyote.

Aidha, Dkt. Mwakibinga alisema kuwa Wizara imetoa kanuni za maadili kwa wote wanaoshiriki katika ununuzi wa umma ili kuweza kuwajumuisha wote wanaoshiriki katika ununuzi wa umma kwa kuwa maamuzi yao huathiri ununuzi wa umma.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lusius Mwenda na Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Boaz Ntembanda, wakimsikiliza Afisa Ugavi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Vailet Mwakajisi, alipokuwa akitoa maelezo kuhusu utekelezaji wa sera, sheria, kanuni na miongozo ya ununuzi wa umma, jijini Arusha.

Akizungumza kuhusu wiki ya ununuzi wa umma alisema kuwa wiki hiyo ni ya muhimu katika kuelimisha umma katika masuala mbalimbali ya ununuzi wa umma ili kufahamu umuhimu wake.

Alisema kuwa matumizi ya teknolojia katika ununuzi wa umma yanahakikisha eneo hilo linaendeshwa kwa kujali maslahi ya Serikali na kushauri watendaji wote kuzingatia sheria, kanuni na kuzingatia maadili.
Kamishna wa Idara ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. John Mboya, akichangia mada wakati wa mawasilisho ya mada mbalimbali katika Wiki ya ununuzi wa umma inayofanyika jijini Arusha.

Kwa upande wao washiriki waliotembelea banda la Wizara hiyo walipongeza elimu inayotolewa katika wiki ya ununuzi wa umma na kutoa rai elimu kutolewa zaidi katika ngazi zote ili kuwezesha elimu hiyo kuongeza tija katika sekta ya ununuzi wa umma nchini.

Kongamano la Wiki ya Ununuzi wa Umma limeandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango na taasisi zinazosimamia ununuzi wa umma nchini ambazo ni Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA), Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA) na Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news