OR-TAMISEMI yatangaza Wanafunzi waliochaguliwa Kujiunga na Kidato cha Tano katika Shule za Sekondari, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Elimu ya Ufundi vya Serikali Mwaka 2022

NA GODFREY NNKO

OFISI ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Baraza la Mitihani la Tanzania imekamilisha zoezi la uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Tano katika shule za sekondari, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Elimu ya Ufundi vya Serikali Mwaka 2022.

Zoezi hilo limefanyika kwa kuzingatia takwimu za matokeo ya wanafunzi waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne Mwaka 2021 kutoka Tanzania Bara.
Hayo yamesemwa leo Mei 12,2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Mhe. Innocent Bashingwa (MB) wakati akitangaza matokeo hayo ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam.

Amesema,watahiniwa katika mtihani wa Kidato cha Nne kwa mwaka 2021 waliopata Daraja la I hadi III walikuwa 173,422 wakiwemo wasichana 75,056 na wavulana 98,366.

Kati ya wanafunzi hao, wanafunzi wenye sifa ya kujiunga na Kidato cha Tano, vyuo vya Ualimu na vyuo vya Ufundi ni 167,515 wakiwemo wasichana 71,433.

"Idadi hiyo ya wanafunzi wenye sifa imejumuisha wanafunzi wenye mahitaji Maalum 508 wakiwemo wasichana 217 na wavulana 291. Hii ni ongezeko la wanafunzi 19,388 kwa kulinganisha na wanafunzi 148,127 waliokuwa na sifa kwa mwaka 2021.

Walikotoka

Mheshimiwa Bashungwa amesema, wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Elimu ya Ufundi mwaka 2022, ni kutoka Shule za Serikali, zisizo za Serikali, watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima waliokidhi vigezo na waliosoma Nje ya nchi ambao matokeo yao yamefanyiwa ulinganifu wa Baraza la Mtihani Tanzania (NECTA).

"Wanafunzi 153,219 wakiwemo wasichana 67,541 na wavulana 85,678 sawa na asilimia 91.8 ya wenye sifa, wamechaguliwa kujiunga na Shule za sekondari Kidato cha Tano, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Elimu ya Ufundi mwaka, 2022 katika mchanganuo ufuatao;

"Wanafunzi 90,825 wakiwemo wasichana 43,104 wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano katika Shule za Sekondari 499 za Serikali zikiwemo Shule mpya 22 za Serikali zilizoanza mwaka, 2022.

"Kati ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha Tano, wapo wanafunzi wenye Mahitaji Maalum 481 ambao kati yao wasichana ni 204. Kati ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano, wanafunzi 41,401 wakiwemo wasichana 17,390 watajiunga kusoma tahasusi za Sayansi na Hisabati na wanafunzi 49,133 wakiwemo wasichana 25,508 watajiunga kusoma tahasusi za masomo ya Sanaa, Lugha na Biashara;

Fani mbalimbali

"Wanafunzi 1,880 wakiwemo wasichana 757 wamechaguliwa kujiunga na fani mbalimbali katika Vyuo 03 vya Elimu ya Ufundi ambavyo ni Chuo cha Ufundi cha Arusha (ATC), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Chuo cha Usimamizi na Maendeleo ya Maji (WDMI),"amefafanua Mheshimiwa Bashungwa.

Amesema,wanafunzi 2,294 wakiwemo wasichana 1,127 wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Afya ngazi ya Stashahada;

Pia amesema,wanafunzi 2,674 wakiwemo wasichana 1,366 wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Ualimu ngazi ya Stashahada ya Sayansi, Hesabu na TEHAMA.

Wanafunzi 6,457 wakiwemo wasichana 3,168 wamechaguliwa kujiunga na Astashahada ya Elimu Maalum, Awali, Michezo, Msingi na Ualimu wa Shule zinazofundisha kwa kutumia Lugha ya Kiingereza (English Medium).

Amesema,wanafunzi 49,089 wakiwemo wasichana 18,019 wamechaguliwa kujiunga na kozi mbalimbali za Astashahada na Stashahada (Certificate and Ordinary Diploma) katika Vyuo vya Elimu ya Ufundi vinavyosimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTVET).

Ongezeko

"Kwa kuangalia takwimu za mwaka 2022, kumekuwa na ongezeko la wasichana 7,555 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi ukilinganisha na mwaka 2021.

"Hata hivyo idadi hii bado ni ndogo kulinganisha na wavulana,"amesema Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Bashungwa amesema,ili kukabiliana na changamoto hii, wizara inaendelea kuboresha miundombinu ya shule ili kuhakikisha wasichana wengi zaidi wanajiunga na Kidato cha Tano.

"Aidha, tunachukua nafasi hii kumshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwezesha ujenzi wa shule za wasichana kumi (10) za mikoa ambapo kila shule itachukua wanafunzi wapatao mia tatu (300) kuanzia mwaka 2023.

14,254 wakosa nafasi

"Pamoja na kuwepo kwa ongezeko la wanafunzi waliojiunga na Kidato cha Tano, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Elimu ya Ufundi kwa mwaka 2022, jumla ya wanafunzi 14,254 wakiwemo wasichana 3,901 na wavulana 10,353 wamekosa nafasi.

"Kati yao, wanafunzi 12,876 wana sifa ya kujiunga na kidato cha Tano. Hali hii imetokana na ongezeko kubwa la wanafunzi waliofaulu na waliokuwa na sifa ya kujiunga na Kidato cha Tano na vyuo vya ufundi pamoja na ufinyu wa nafasi za Kidato cha Tano na Vyuo vya Elimu ya Ufundi (NACTVET).

"Wanafunzi hao wanatarajiwa kujiunga na kidato cha Tano katika awamu ya pili baada ya ukamilishaji wa baadhi ya miundombinu ya shule na vyuo,"amesema.

Wito

Mheshimiwa Waziri Bashungwa amesema, muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano utaanza Juni 13, 2022.

Hivyo, wanafunzi wote waliopangwa kujiunga na Kidato cha Tano kwa mwaka 2022 wanapaswa kuanza kuripoti katika Shule walizopangwa kuanzia tarehe 13 Juni, 2022.

"Siku ya mwisho ya kuripoti itakuwa tarehe 30 Juni, 2022. Endapo mwanafunzi atachelewa kuripoti nafasi yake itachukuliwa na mwanafunzi mwingine aliyekosa nafasi.

"Na kwa kuzingatia kuwa Uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Elimu ya Ufundi umefanyika kwa kuzingatia ufaulu na nafasi zilizopo katika shule hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya shule kutokana na ukosefu wa nafasi kwenye shule husika,"amesema.

Wakati huo huo, Waziri Bashungwa amesema fomu za maelezo ya mahitaji ya kujiunga na Kidato cha Tano (Joining Instructions) kwa shule zote za Kidato cha Tano zinapatikana kwenye tovuti ya OR-TAMISEMI kupitia kiunganishi cha www.tamisemi.go.tz na kwa wale waliopangwa kwenye Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi watapokea maelekezo ya namna ya kujiunga kutoka katika Vyuo walivyopangwa. Aidha,

"Orodha ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Elimu ya Ufundi mwaka, 2022 inapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya Rais -TAMISEMI ya www.tamisemi.go.tz na Baraza la Taifa la Elimu ya Mafunzo ya Ufundi ya www.nacte.go.tz.

"Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza walimu, wazazi na walezi wote kwa juhudi walizozifanya katika ufundishaji na kuwezesha wanafunzi kufaulu vizuri. Naomba wazazi/walezi wote tuendelee na moyo huu wa kusimamia na kufuatilia maendeleo ya watoto wetu,"amesema.

Pongezi

"Aidha, nawapongeza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Elimu ya Ufundi. Napenda kuchukua fursa hii, kuwahimiza kuendelea kufanya bidii katika kujifunza ili waweze kufanikiwa kujiunga na mafunzo ya elimu ya juu baada ya kuhitimu Kidato cha Sita na Vyuo vya Elimu na ya Ufundi.

"Ninawashukuru Viongozi na Watendaji wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na Wananchi kwa ujumla kwa kushiriki kikamilifu katika kuimarisha miundombinu ya shule ikiwemo mabweni na majengo mengineyo yaliyowezesha baadhi ya shule kupokea wanafunzi wa Kidato cha Tano kwa mara ya kwanza mwaka 2022,"amesema Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Pia ametoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa azma ya Serikali ya kuwa na Shule za Sekondari za Kidato cha Tano katika kila halmashauri inatekelezwa ili kuwezesha wanafunzi wote wanaofaulu Mtihani wa Kidato cha Nne kupata nafasi ya kuendelea na masomo ya Kidato cha Tano na Sita.

Amesema, mikoa ihakikishe inakuwa na tahasusi zote za msingi katika shule zinazoanzishwa ili kuwapunguzia wazazi na walezi gharama za usafiri kwenda shule za mbali.

Aidha, kutokana na ongezeko la ufaulu wa masomo ya Sayansi, "ninaelekeza shule zitakazoanzishwa za Kidato cha Tano ni lazima ziwe na Tahasusi za Sayansi. Pia, shule ambazo zina tahasusi za sanaa pekee ziongeze tahasusi za sayansi.

"Pamoja na maelekezo haya, kwa mwanafunzi, mzazi na mlezi atakayekuwa na suala linalohitaji maelekezo au ufafanuzi zaidi aende katika Ofisi za Elimu za Mikoa na Halmashauri au apige simu kwenye namba ya Kituo cha Huduma kwa wateja cha OR-TAMISEMI kwa namba za simu 026 2160210 au 0735 160210,"amesema Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news