Rais Samia:Serikali imesikia kilio cha wananchi kupanda bei ya bidhaa

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametangaza mkakati wa kubana matumizi ya Serikali katika bajeti ya matumizi ili kupata fedha za kupunguza makali ya ongezeko la bei ya mafuta linalosababisha kuongezeka kwa bei za bidhaa na huduma nchini.

Ameyasema hayo Mei 9, 2022 katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari akisema Serikali imesikia kilio cha wananchi cha kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Taifa tarehe 9 Mei, 2022 kuhusiana na suala la kupanda kwa bei ya Mafuta nchini akiwa Ikulu Jijini Dar es Salaam. (Picha na Ikulu).

“Katika mwaka wa fedha unaoanza Julai mwaka huu tutachukua hatua mbalimbali za kikodi kuweka ahueni kwa wananchi. Hata hivyo, kutoa nafuu za kupanda kwa bei za mafuta hakuwezi kusubiri hadi mwaka huu wa fedha, nimeamua kwa hiyo wananchi waanze kupata nafuu kuanzia tarehe Mosi Juni.

"Nimeelekeza kwamba, Serikali tujibane na tujinyime ili kupata fedha kutoka kwenye matumizi ya kawaida ya Serikali ili ziende kutoa nafuu za bei ya mafuta kuelekea mwaka wa fedha,” amesema Rais Samia.

Pia amemwagiza Waziri wa Nishati kutoa ufafanuzi leo Bungeni kuhusu hatua hiyo, huku akimwelekeza Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba kutoa ufafanuzi wa kodi katika mafuta.

Amesema, ongezeko la bei ya mafuta limetikisa nchi zote duniani, tajiri na masikini, zenye kuzalisha mafuta na zenye kuagiza na kwamba Tanzania haijasalimika.

“Novemba mwaka jana nilielekeza tupunguze tozo zinazotozwa na taasisi mbalimbali. Hatua hiyo ilisababisha Serikali kupungukiwa kwa mapato yake kwa kiasi cha shilingi bilioni 102.Pamoja na hatua hizo bado nafuu haikupatikana kutokana na kasi ya kupanda bei,”amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news