SHANTA KUANZA UZALISHAJI WA DHAHABU SINGIDA 2023

NA STEVEN NYAMITI-WM

MGODI wa Kati wa uchimbaji wa madini ya Dhahabu wa Shanta wa Singida unatarajiwa kuanza rasmi uzalishaji mwanzoni mwa mwaka 2023 mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya mgodi huo.
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa akikagua maendeleo ya Mgodi wa Kati wa Shanta Mkoani Singida unaotarajiwa kuanza uzarishaji Mwaka 2023.

Meneja Mkuu wa mradi huo, Mhandisi Jiten Divecha ameyasema hayo Mei 13, 2022 kwa Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa wakati alipotembelea na kukagua Maendeleo ya Mradi wa Mgodi wa Kati wa Dhababu wa Singida (Singida Gold Mine) unaomilikiwa na Kampuni ya Shanta Mining Company Limited uliyopo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Divecha amesema, kwa sasa mgodi umeendelea kutoa fursa mbalimbali za ajira kwa Watanzania pamoja na kununua bidhaa za Kitanzania.

Akizungumza, mara baada ya kukagua maeneo ya uchimbaji katika mgodi huo, Dkt.Kiruswa ameagiza uongozi kuhakikisha wanamaliza changamoto zote zinazokwamisha kuanza kwa mradi huo ili uchimbaji uanze kwa haraka.

Amesema, wananchi wa Ikungi na wakazi wa Singida wanatarajia kuona mgodi huo unaanza kazi ili wananchi waweze kunufaika na uwepo wa mgodi katika jamii yao.
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa akizungumza wakati alipotembelea Mgodi wa Kati wa Shanta Mkoani Singida.

Pia, Dkt.Kiruswa ameipongeza Kampuni ya ya Uchimbaji Madini ya Shanta kwa uwekezaji mkubwa wanaoendelea kuufanya katika mgodi huo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya mgodi, ajira zinazotolewa, afya na miradi mbalimbali ya maendeleo.

Vile vile, Dkt. Kiruswa ameuagiza mgodi wa Shanta kuandaa na kutekeleza mpango wa uchangiaji wa kampuni yao kwenye jamii (CSR) kwa mujibu wa Sheria.

Amesema, wanatakiwa kuhakikisha kama wawekezaji jamii inayowazunguka inanufaika na mradi husika huku akifurahishwa na Sheria ya Local Content inavyotekelezwa na mgodi huo.
Muonekano wa Mitambo katika mgodi wa Kati wa Shanta wa madini ya dhahabu mkoani Singida.

"Nimefurahishwa na mpango wa Local Content, nimetembea hapa sijaona hata mgeni mmoja, wanaofanya kazi hapa wote ni Watanzania, lakini pia mnatumia rasilimali zinazopatikana hapa hapa, nimesikia hata maharage yanatoka hapa,"amesema Dkt. Kiruswa.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu amemueleza Dkt.Kiruswa kuwa, wananchi wa Singida wanatamani mradi huo uanze mara moja ili waweze kunufaika na mradi huo.
Meneja Mkuu wa mradi Mhandisi Jiten Divecha akiwasilisha taarifa fupi ya Mgodi wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini Dkt. Kiruswa mara baada ya kutembelea mgodi huo.

Amesema, mradi utakapoanza utaleta maendeleo kwa jamii inayozunguka pamoja na kuongeza mapato kwa Serikali.
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa akikagua maendeleo ya Mgodi wa Kati wa Shanta Mkoani Singida unaotarajiwa kuanza uzarishaji Mwaka 2023.

Wengine waliohudhuria ziara ya Naibu Waziri wa Madini ni viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Ikungi, viongozi wa vijiji na kata wanaozunguka eneo la mradi na wadau wa Sekta ya Madini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news